Posted by Williammalecela.com on Sunday, July 27, 2014
Sita washtakiwa kwa ugaidi Arusha
WATUHUMIWA sita wanaodaiwa kurusha bomu katika mgahawa wa Vama
Tradition jijini Arusha, Julai 7, mwaka huu, na kusababisha watu wanane
kujeruhiwa huku mmoja wao akikatwa mguu, wamepandishwa kizimbani na
kusomewa mashtaka manne.
Watuhumiwa hao ambao walikamatwa juzi kwa nyakati tofauti, walifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana chini ya ulinzi mkali wa
polisi, majira ya saa 7:30 mchana.
Baada ya kufikishwa mahakamani hapo, washtakiwa hao, Shabani Mmasa,
Athumani Huseini, Mohamedi Nuru, Jafari Lema, Abdul Salum na Saidi
Temba, walisomewa mashtaka manne na Mwanasheria wa Serikali, Augustino
Kombe.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Rose Ngoka, washtakiwa wote walisomewa shtaka la
kwaza la kupanga njama za kufanya ugaidi kinyume na sheria ya ugaidi ya
nchi.
Washtakiwa hao walidaiwa kuwa Februari na Julai mwaka huu, walipanga
njama za kufanya ugaidi katika mgahawa wa Vama uliopo maeneo ya Gymkhana
jirani na Mahakama Kuu jijini Arusha na kujeruhi watu wanane
waliokuwemo ndani ya mgahawa huo.
Waliojeruhiwa katika kadhia hiyo ni Deepack Gupta aliyekatwa mguu wa
kushoto, Manisha Gupta, Prateek Javey, Manci Gupta, Mahish Gupta, Ray
Rajin, Ritwik Khandehral na Vinpd Suresh.
Katika kosa la pili, washtakiwa wanadiwa kufanya ugaidi ambapo
mwanasheria Kombe alisema mnamo Julai 7, mwaka huu, walirusha bomu
katika mgahawa huo na kusababisha
kujeruhi watu wanane waliokuwamo ndani ya mgahawa huo.
Kosa la tatu lilitajwa kwa washtakiwa Lema na Huseini ambao walidaiwa
mahakamani hapo kuwa walihusika kutoa silaha ambazo ni bomu zilizohusika
katika shambulio hilo.
Shtaka la nne liliwahusisha washtakiwa wote sita wakidaiwa kutoa
ushirikiano katika kufanikisha kutendeka kwa kosa la ugaidi na kukiuka
vifungu kadhaa vya sheria ya ugaidi vinavyokataza mtu yeyote kujihusisha
na masuala ya ugaidi.
Hakimu Ngoka mara baada ya kutajwa kwa mashtaka hayo, aliwazuia wasijibu
chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Aidha, mwanasheria wa serikali, Kombe aliiambia mahakama hiyo kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamailika, hivyo kuiomba ipange tarehe
nyingine ya kutaja kesi hiyo.
Baada ya maombi hayo, hakimu Ngoka aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6,
mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa tena, huku washtakiwa
wakipelekwa rumande.
0 comments:
Post a Comment