Monday, August 11, 2014


SIKU chache baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda (CHADEMA), kudaiwa kukisaliti chama hicho na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo linaendelea na vikao vyake Mjini Dodoma, mbunge huyo ameibuka na kutangaza rasmi kuachana na chama hicho.
Alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na matusi dhidi yake, kuitwa msaliti, mnafiki hivyo matusi yanayotolewa juu yake sasa yanatosha.



Bw. Shibuda aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Baraza la Wazee wilayani humo ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi uamuzi wa kuachana na CHADEMA.
Alisema tangu amejiunga na CHADEMA, amekuwa akitukanwa, kuitwa masaliti na kunyimwa ushirikiano kutoka uongozi wa juu katika chama hicho ili kuchochea maendeleo na wananchi wake.
 

Aliongeza kuwa, chama hicho kimeshindwa kumpa heshima aliyonayo hivyo hawezi kuendeshwa kama mtoto na wala kupelekwa kama viongozi wa chama hicho wanavyotaka.

"Tangu nimejiunga na chama hiki, kila siku natukanwa hata na watoto wadogo ndani ya chama hiki...sasa nimechoka na siwezi kuvumilia hali hii, nimekuwa mvumilivu kwa muda mrefu hivyo natangaza kuwa, sitagombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA kwani chama hiki si baba wala mama yangu," alisema.


Kuhusu kurudi kwake bungeni
Akizungumzia madai ya kurudi kwake katika Bunge Maalumu la Katiba, alisema si ya kweli na hajawahi kuingia ndani ya Bunge hilo tangu lianze vikao vyake Agosti 5 mwaka huu bali alipita Dodoma wakati akitokea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Alisema wakati akitokea Dar es Salaam, afya yake ilikuwa mbaya pamoja na kuvimba miguu hivyo alilazimika kupita kwa madaktari walioko katika viwanja vya Bunge ili aweze kupatiwa dawa.

"Wakati nikiwa njiani kuja Maswa kwenye msiba, afya yangu ilikuwa mbaya hivyo nililazimika kumpigia simu daktari wa Bunge na kumueleza juu ya afya yangu akaniambia nipite akanicheki.
"Nilipofika bungeni, nikapewa maelekezo ili niweze kupata dawa na kuangaliwa afya yangu, lazima nijiandikishe na mimi nilifanya hivyo na baada ya kujiandikisha, nilipewa dawa na kuangaliwa afya yangu sasa watu waliponiona wakasema nimekisaliti chama na UKAWA jambo ambalo si kweli," alisema.

Bw. Shibuda aliongeza kuwa, baada ya kupatiwa dawa aliendelea na safari yake ya kwenda jimboni kwa ajili ya msiba hivyo alishangaa kusikia anaendelea na vikao bungeni wakati yuko msibani.

Azungumzia UKAWA
 

Akiuzungumzia UKAWA, Bw. Shibuda alisema umoja huo hauna masilahi kwa Watanzania ambao asilimia kubwa ni wakulima na wafugaji kwani tangu watoke bungeni na yeye akiwa mmoja wa waliotoka, hajawahi kujulishwa jambo lolote kuhusu mazungumzo kati yao na CCM.

Alisema kitendo cha kutojulishwa lolote, kinampa shida ya kuamua kuendelea na Bunge la katiba au kususia vikao kwani hapewi taarifa za mchakato wa maridhiano lakini wajumbe wengine wamekuwa wakipata taarifa hizo na yeye kubaguliwa.
"Mimi si mkokoteni na siwezi nikaota juu ya maamuzi ya UKAWA ambayo wamekuwa wakiyajadili katika vikao vya maridhiano, wajumbe wengine wamekuwa wakipewa taarifa kila siku juu ya kinachoendelea hadi sasa lakini mimi nabaguliwa kwa nini," alihoji Bw. Shibuda.

Aliuponda umoja huo na kusema hauna dhamira ya kuwasaidia wakulima wa pamba na wafugaji ambao ndiyo wapiga kura wake na ndio walimtuma bungeni kujadili kero zao.

Atangaza kurudi bungeni
 

Katika hali isiyo ya kawaida, Bw. Shibuda alitangaza rasmi kurudi bungeni ili kuendelea na vikao vya Bunge la Katiba akisema anaenda kuzungumzia kero za wakulima wa pamba na wafugaji ili ziwekwe katika Katiba Mpya.
"Siko tayari kupelekwa na chama chochote cha siasa nchini wala viongozi wake, nitaenda bungeni wiki hii kuendelea na vikao ili niweze kuwatetea wakulima wangu wa pamba na wafugaji ambao ni maskini sana," alisema.

Juu ya viongozi CHADEMA
 

Akiwazungumzia viongozi wa juu wa chama chake, alisema wamekuwa wakitumia ubabe, vitisho na ubaguzi kukiendesha chama hivyo ni wazi wamekosa hekima na busara.
"Viongozi wa CHADEMA ni wababe, hawana hekima wala busara, wanataka kuendesha chama watakavyo kama cha kwao lakini mimi nimekataa, nataka niwaambie kuwa, waliposikia nimetoka CCM, wao ndiyo walinifuata nijiunge na chama chao," alisema.

Atangaza vita na Lissu
 

Bw. Shibuda alidai kukerwa na Mwanasheria wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu, akidai amekuwa akimuandama bila ya sababu na kumtaka aache mara moja.
 

Alisema amemvumilia kwa kiwango kikubwa kwani amekuwa akimsingizia mambo ya uongo na kutangaza vita dhidi yake.
 

"Amenituhumu mambo mengi na mimi nimemvumilia vya kutosha na sasa, ndani ya siku chache nikirudi Dar es Salaam tutaonana maana siwezi kutukanwa na mtoto mdogo kama Lissu," alisema.
Bw. Shibuda mbali na kutangaza kuachana na chama hicho, hakuwa tayari kuzungumzia chama anachotarajia kuhamia bali alisema chama atakachohamia ni siri yake akisema kitakuwa chama kipya nchini.

Wazee wamuunga mkono

 

Baada ya wazee hao kumsikiliza Bw. Shibuda, walimuunga mkono kwa uamuzi wake wa kukihama chama hicho na kumtaka arejee bungeni ili kuwatetea wananchi wa Maswa ambao ni wakulima na wafugaji.

"Sisi kama wazee, tunakuunga mkono na tunawataka wabunge wengine kurejea bungeni ili kujadili matatizo ya Watanzania ambayo hayahusiani na muundo wa Serikali...tunataka wakulima na wafugaji wadhaminiwe," Alisema Mohamed Mangasiri ambaye ni Mwenyekiti Baraza la Wazee jimboni humo.

Chanzo: Majira

0 comments:

Post a Comment