MIMBA KUCHOROPOKA (MISCARRIAGE)
Tatizo la mimba kuharibika na kutoka (kuchoropoka) kabla ya umri wake
unaotakiwa kukamilika, limekua likiwasumbua wanawake wengi. Kutokana na
maombi ya wasomaji wetu, tutalijadili kwa kina tatizo hili ambalo
kitaalamu huitwa Miscarriage. MISCARRIAGE NI NINI? Kwa kawaida, ili mtoto azaliwe, ni lazima mwanamke afanye tendo la ndoa akiwa katika siku zake za kupata ujauzito
ambapo mimba hutungwa. Baada ya mimba kutungwa, mtoto hukaa tumboni kwa
muda wa miezi tisa mbapo hupitia hatua mbalimbali za mabadiliko hadi
kuwa binadamu aliyekamilika. Inapotokea kuwa kitoto kimetoka
tumboni kwa namna yoyote ile, kikiwa na umri wa chini ya miezi mitano
(wiki ishirini), tatizo hilo huitwa Miscarriage. Katika hali hii,
kitoto kinakuwa hakijakamilika na hakiwezi kujitegemea chenyewe kwa
mahitaji muhimu kama kupumua, jambo ambalo husababisha kifo. NB: Mtoto akitoka akiwa ameshapita umri wa miezi mitano, tatizo hilo huitwa pre-mature birth (kuzaa njiti). NINI HUSABABISHA MISCARRIAGE? Zipo sababu nyingi zinazosababisha ujauzito uchoropoke. Matatizo ya Vinasaba (Genetic Factors)
Hitilafu katika kromosomu (Chromosomal abnormalities) ambayo
husababisha vinasaba kuwa katika hali isiyo ya kawaida, inatajwa kuwa
sababu kubwa zaidi inayosababisha ujauzito uchoropoke ukiwa na umri wa
chini ya wiki 13. Matatizo haya husababisha damu ya mama ishindwe
kuendana nay a mtoto na kusababisha reactions ambazo humdhuru mtoto na
kumfanya ashindwe kuhimili hali ya tumboni kwa mama. Hivyo ujauzito
kuharibika. 2. Upungufu wa Homoni (Progesterone Deficiency)
Homoni ya Progesterone hufanya kazi kubwa kuanzia mamba inapotungwa
mpaka mtoto anapozaliwa. Progesterone ndiyo huchochea uimara wa ukuta wa
placenta ambao mtoto hujishikiza. Upungufu wa homoni hii husababisha
ukuta wa mji wa mimba kushindwa kuhimili uzito wa mtoto, hali ambayo
husababisha ujauzito kuharibika na kutoka kabla ya muda wake. 3. Umri Mkubwa
Kwa kawaida, mwanamke anapofikisha umri wa miaka 35 au zaidi, misuli
(sphincters) ya mji wake wa uzazi hulegea na kupungua nguvu za kuweza
kuhimili na kutunza kiumbe kinachokuwa ndani ya mji wa uzazi. Kulegea
kwa misuli hii husababisha mimba kuchoropoka kwa urahisi. 4. Magonjwa
Wanawake wanaosumbuliwa na magonjwa kama kisukari, unene kupindukia
(obesity), Polycystic Ovary Syndrome, malaria kali, magonjwa ya zinaa na
mengineyo huwa katika hatari kubwa ya mimba zao kutoka. 5. Hitilafu Katika Kizazi
Baadhi ya wanawake huwa na mfuko wa mimba (uterus) ambao muundo wake
siyo wa kawaida (T- Shaped Uterus). Wanawake wenye tatizo hili, huwa na
hatari kubwa ya mimba zao kuharibika kabla ya kutimiza umri wa miezi
tisa. 6. Maambukizi ya bakteria au fangasi Maambukizi ya
bakteria au fangasi husababisha misuli ya kizazi kushambuliwa na kisha
kupoteza uwezo wake wa kuhifadhi ujauzito, jambo ambalo husababisha
mimba kuchoropoka. Sababu nyingine ni pamoja matumizi ya pombe
kali, uvutaji sigara, matumizi ya dawa za kulevya, kemikali, matatizo ya
kurithi n.k DALILI ZA MIMBA KUCHOROPOKA (Symptoms of a miscarriage): 1. Kutokwa na damu sehemu za siri
Dalili kubwa za miscarriage ni mama mjamzito kutokwa na damu (nzito au
nyepesi) sehemu za siri kwa vipindi au mfululizo. Damu hizi hutoka kama
zile zitokazo mwanamke anapokuwa kwenye siku zake na huambatana na
maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu. 2. Maumivu makali ya viungo
Dalili nyingine za mimba inayotaka kuchoropoka ni maumivu makali ya
mgongo, kiuno, nyonga na tumbo chini ya kitovu. Maumivu haya huanza
taratibu lakini huongezeka kadiri muda unavyozidi kusonga mbele. Pia
huambatana na kutokwa na damu kama ilivyoelewa hapo juu. 3. Kutokwa na uchafu sehemu za siri
Dalili nyingine kubwa ya Miscarriage ni mama mjamzito kuanza kutokwa na
uchafu wenye rangi sambamba na mabonge ya damu sehemu za siri.
ANGALIZO: Dalili hizi pekee hazitoshi kuashiria kuwa tayari ujauzito
umeharibika ila mama mjamzito anapoona moja kati ya dalili hizi au zote,
anashauriwa kuwahi hospitali kuonana na daktari haraka iwezekanavyo.
Endapo mama atachelewa, atakuwa anajisababishia matatizo zaidi kwani
sumu za kiumbe kilichoharibika huharibu mfuko wa uzazi na kusababisha
matatizo makubwa siku za mbeleni ikiwemo ugumba. JE, KUFANYA MAPENZI UKIWA MJAMZITO KUNA MADHARA?
Swali: Pole na kazi dokta, mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 22.
Nimeolewa na hivi sasa nina ujauzito wa miezi mitano. Tatizo
linalotusumbua mimi na mume wangu ni kuwa, tangu nipate ujauzito hamu ya
kushiriki tendo la ndoa imeongezeka sana lakini tunaogopa kufanya kwa
sababu tuliwahi kuambiwa kuwa tunaweza kumdhuru mtoto tumboni na
ujauzito kutoka. Tunaomba ufafanuzi wako daktari, je ni kweli kuna
madhara kufanyamapenzi ukiwa mjamzito? Msomaji, Hanang, Manyara
Jibu: Siyo kweli kwamba kufanya mapenzi ukiwa mjamzito kutasababisha
mimba kuharibika na kutoka. Jambo la kuzingatia ni kutotumia staili
zinazobana au kuumiza tumbo au kufanya mapenzi kwa muda mrefu. Tendo la
ndoa linalofanywa kwa wastani husaidia kulainisha njia ya uzazi hivyo
kupunguza matatizo wakati wa kujifungua. Inashauriwa kuwa ujauzito
ukifikisha miezi nane, wanandoa waache kufanya tendo hilo mpaka mama
atakapojifungua na kupona. KUZUIA MIMBA KUCHOROPOKA Hakuna
tiba ya moja kwa moja inayoweza kuzuia tatizo la mamba kuchoropoka ila
kwa kuzingatia vyanzo vya tatizo hili, ni rahisi kuliepuka. kuacha tabia hatarishi
Tabia kama ulevi wa kupindukia, matumizi ya dawa za kulevya na sigara
kwa wanawake wajawazito yakiepukwa, hupunguza hatari ya miscarriage. Kufanya mazoezi
Inashauriwa kuwa, mama mjamzito ajenga mazoea ya kufanya mazoezi mepesi
angalau mara tatu kwa wiki kwa muda usiopungua nusu saa. Mazoezi kama
kutembea na mengine mepesi husaidia kuimarisha misuli ya kizazi na hivyo
kupunguza hatari ya mamba kuchoropoka. Vyakula Inashauriwa
mama mjamzito kula vyakula vyenye madini ya Zinc, Magnesium, Vitamin B6
na Vitamin C kwa wingi ili kulinda ujauzito wake. Vyakula vitokanavyo
na nafaka, mimea jamii ya mikunde, karanga, kiini cha yai, mboga za
majani na matunda husaidia kuimarisha afya ya mama na mtoto hivyo
kuzuia tatizo hili. Kupata chanjo Akina mama wajawazito
wanashauriwa kuhudhuria kliniki mara kwa mara kwa ajili ya kupatiwa
chanjo za magonjwa hatarishi ambayo husababisha ujauzito kuharibika na
kutoka. Kupima afya mara kwa mara Akina mama wajawazito ni
lazima wajenge mazoea ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara na
kuangalia uwepo wa magonjwa kama ya zinaa na mwengineyo, na kama yapo
watibiwe haraka ili kulinda kiumbe kilichopo tumboni.
|
0 comments:
Post a Comment