Posted by Williammalecela.com on Monday, August 04, 2014
 |
Kikwete: Jengeni hoja kutetea Uraia pacha badala ya kupiga kelele mitandaoni tu!
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amewataka Watanzania waishio nje ya nchi na wanaotaka kuona
Tanzania inakubali kuanzisha mfumo wa uraia pacha kutumia muda wao
kujenga hoja za jambo hilo badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya
blogu na kulaumi watu wengine.
Rais Kikwete amewataka Watanzania hao kusema ili wasikike kwa sababu,
kimsingi, hoja ya uraia pacha haina nguvu miongoni mwa Watanzania
wanaoishi Tanzania bali hoja hii inatokana zaidi na msukumo wa
Watanzania wanaoishi nje ambao kwa bahati mbaya hawafanyi jitihada za
kutosha kutetea hoja yao.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati
alipokutana, akazungumza na kujibu maswali ya Watanzania wanaoishi
Marekani, hasa katika maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya
Virginia, Maryland, New York na hata California katika mkutano
uliofanyika katika Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tisa katika Marekani ambako
miongoni mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Marekani na
Afrika ambao shughuli zake zinaanza leo Jumatatu. Mkutano huo,
umeitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unahudhuriwa na viongozi
wa nchi 47 kutoka Afrika.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao kuacha kupoteza muda kujadili
mambo yasiyokuwa na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika
kujenga hoja yenye nguvu zaidi ya uraia pacha, jambo ambalo ni moja ya
mambo yatakayojadiliwa katika mchakato wa Katiba mpya.
“Mnashinda kwenye blogu mkijadili mambo ambayo wenzenu nyumbani
wana uwezo mkubwa zaidi kuyajadili kuliko nyie. Mnajiingiza katika mambo
ambayo sisi nyumbani tuna uwezo mkubwa nayo kuliko nyie. Kwa mambo
haya, sisi tunatosha zaidi. Mnaacha kujadili mambo yanayohusu maisha
yenu – kama hili la uraia pacha na mnajiingiza katika mambo
yasiyowahusu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa sasa upo huu mjadala wa uraia pacha ni hoja yenu. Nyie
badala ya kushiriki katika mjadala huu kwa njia zote, mnashinda kujadili
mambo ambayo hayana maana. Kwanza hoja ya uraia pacha siyo hoja ya watu
wengi nyumbani, siyo jambo linalowahusu. Hata rasimu sina uhakika kama
mmeisoma vizuri na kujua nini kimependekezwa – lakini hata huo muda
hamna. Kazi yenu mnashinda mnajadili mambo yasiyokuwa na maana – nani
kavaa nguo fupi, nani kafanya nini, haya ndiyo mambo yanayochukua muda
wetu.”
Rais Kikwete amesisitiza: “Ushauri wangu ni kwamba tumieni muda
wetu kusaidia kusukuma hoja yenu hii muhimu – ambayo kama mnavyojua
imeingizwa katika rasimu kwa mapendekezo ya CCM kwa sababu suala hilo
halikuwemo katika rasimu ya kwanza.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti, 2014
|
0 comments:
Post a Comment