BINADAMU ni
kiumbe ambaye ameumbwa na tabia nyingi. Miongoni mwa tabia hizo ni kutoridhika
na hali aliyokuwa nayo, au kile anachopata.
Siku zote binadamu akiwa mnene atatamani
apungue na kuwa mwembamba, mwembemba atamani unene. Maskini atatamani kuwa
tajiri. Lakini, hali ni tofauti kwa binadamu anayeitwa Peng Shuilin, mkazi wa
kitongoji cha Hunan, China.
Shuilin mwenye umri wa miaka 39,
amepoteza sehemu kubwa ya mwili wake; amebaki na mikono, tumbo na kichwa tu,
lakini anaishi maisha ya raha na kukubali kila ambacho Mungu amemjaalia.
Shuilin alipoteza viungo vyake katika
ajali mbaya ya gari iliyotokea mwaka 1995, akiwa kwenye kitongoji cha Shenzhen,
ambapo tairi za gari hilo kubwa lililokuwa na mizigo lilipita kwa bahati mbaya
kiunoni mwake na kufyeka viungo vyote na kubaki nusu. Ndio maana mwenyewe
anajiita 'binadamu nusu.'
Baada ya ajali hiyo mbaya hakuna
aliyeamini kama Shuilin angeweza kuendelea kuwa hai, na alilazimika kukaa
hospitali iliyopo Shenzhen, Kusini mwa China, kwa miaka miwili ili kupatiwa
matibabu ya karibu zaidi kutokana na upasuaji mkubwa aliofanyiwa kurekebisha
mawasiliano ya mwili wake na viungo vilivyosalia.
Hivi sasa Shuilin kwa kutumia sehemu ya
mwili wake uliobaki, anaweza kufanya mazoezi, anaweza kutumia mikono yake
anayoitegemea kwa shughuli zake ndogo ndogo kuanzia mwanzo wa siku hadi
anapoingia kitandani kujipumzisha.
Ni miaka 19 sasa imepita tangu alipopata
ajali hiyo mbaya, Shuilin ameongezewa viungo vingine bandia vya mwili wake
ambavyo anaendelea kuvifanyia mazoezi akiwa na madaktari wake.
“Tumemfanyia uchunguzi, yupo imara kama
ilivyo kwa wanaume wa umri wake" anasema mmoja wa madaktari wanaomtibu
Shuilin.
Kutokana na nafuu aliyopata, Shuilin
amefungua duka lake kubwa la kuuza bidhaa mbalimbali ambalo lina utaratibu
tofauti na mengine; dukani kwake kila kitu kinauzwa kwa nusu ya bei ya kawaida
na anaruhusu mapatano ya bei. Duka hilo amelipa jina la "binadamu nusu,
bei nusu."
Shuilin mwenye sentimita 78, amekuwa
maarufu nchini mwake na hata nje ya China, amekuwa mfano wa kuigwa kwa watu
wengi. Kwa kutumia baiskeli yake maalumu inayotumiwa na watu wenye ulemavu
'wheel chair' anaweza kuhudumia wateja wake bila wasi wasi na muda wote
anaonekana mwenye furaha na asiyejali matatizo makubwa yaliyomkuta.
Watu wengi wanashangaa kumuona akiwa
katika hali hiyo, jambo ambalo limewabadilisha mitazamo yao hasa kwa wale
waliokuwa wamekata tamaa ya maisha huku wakiwa wamekamilika viungo.
Ni baada ya watu hao kujiuliza, kama
mlemavu aliyekatika sehemu kubwa ya mwili wake anaishi maisha ya furaha na
amefanikiwa kimaisha, kwanini wao wasio na kasoro washindwe? Simulizi ya Peng
Shuilin inasikitisha, lakini inafundisha.

0 comments:
Post a Comment