Mwandishi wetu ametembelea
kijiji kimoja nchini Sudan Kusini ambapo watu wamelazimika kula mbegu na
majani kutoka mtoni, huku kukiwa na tishio kubwa la baa la njaa.
Ni
alfajiri katika kijiji cha Reke, makao ya takriban watui elfu tatu
waliofurushwa makwao kufuatia mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na
bvikosi vya waasi katika jimbo la Unity lenye utajiri mkubwa wa mafuta
Mvua
kubwa ilikuwa imenyesha usiku kutwa katika kijiji hicho kilicho
kilomita 650 ( maili 400) Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Juba.
Barabara hazipitiki ila tuu kutumia magari makubwa aina ya 'four-wheel.'
Watoto
kadhaa wanacheza katika eneo moja la kijiji. Katika eneo linguine,
kundi mmoja la wanawake linajenga nyumba ya muda, inayojulikana kama
Tukul, wakitumia vijiti waliyokusanya kutoka mto uliokaribu.
Kwingineko,
ajuza mmoja ameketi nje ya nyumba yake, inayofuka moshi kutoka ndani.
Anatabasamu tunapomkaribia kisha anatoa kiko na kukiwasha, anaivuta na
kutoa moshi huku akishangiliwa na baadhi ya majirani zake.
“ Sina
chochote cha kufanya, maisha yangu ni magumu, lakini hilo halitanizuia
kufurahia kiko chake,” ananiambia kupitia mkalimani.
Lakini tabasamu na vicheko hapa Reke vinaficha masaibu ya jamii hii.
'Wanakabiliwa na Njaa'
Wengi wao ni kutoka jamii ya Nuer, sawa na kiongozi wa waasi Riek Machar.
Rais Salva Kiir ambaye anatoka kabila la Dinka, amemshutumu kwa kutaka kupindua serikali mwezi Desemba.
Bwana Machar alikanusha madai hayo, lakini akakusanya kikosi cha waasi kupigana na Rais Kiir.
Zaidi
ya watu milioni 1.5 wamefurushwa makwao kufuatia vita hivyo na Umoja wa
Mataifa umeonya kuwa Sudan Kusini imo katika hatari ya kukabiliwa na
baa kubwa la njaaKatika msimu huu wa mvua, barabara nyingi zimeharibika
na hazipitiki.
Ni vigumu kupata au kusafirisha chakula.
Katika
kijiji cha Reke, watu wanategemea chakula cha msaada kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Chakula (WFP), lakini wanasema kupatikana kwake ni
nadra sana.
"WFP imekuwa ikiwasaidia sana watu hapa Reke, lakini
msaada huo huja mara moja kila baada ya miezi miwili.Ona jinsi watu hapa
wana njaa," jamaa mmoja ananielezea
Wakaazi wa Reke sasa
wanategemea magugu na mbegu wanayoyakusanya kutoka mto uliokaribu na
hapa. Hukusanya mbegu hizo, na kuyasaga kisha huyapika kwa kuchanganya
na maji.
Umoja wa Mataifa unasema takriban watu milioni nne wanakabiliwa na njaa baada ya wakulima kukosa kupanda katika msimu wa upanzi.
Wataalamu
wameonya kuwa huenda Sudan Kusini ikakabiliwa na baa kubwa la njaa
kufikia mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwaka ujao.
Sudan Kusini
ni taifa jipya zaidi duniani, na lilijitenga na kupata uhuru mwaka wa
2011, baada ya miongo kadhaa ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na
Upande wa kaskazini.
'Wanatembea kwa muda wa saa Sita'
Kilomita chache kutoka Reke, tunafika katika kliniki moja inayowashugulikia watotot wanaougua utapya mlo.
Tangu
mapigano kuzuka mwezi Disemba, kliniki hiyo inayoendeshwa na shirika la
misaada la International Rescue Committee limekuwa likiwatibu watoto 16
kila wiki.
Lakini idadi hiyo imekuwa ikipungua, anasema muuguzi Peter Manyang.
"Hivi
sasa kuna watoto sita waliolazwa hapa. Lakini hatujui iwapo ni hali
inaimarika au ni kutokana na mvua kubwa inayonyesha na kuharibu barabara
na hivyo kutatiza usafiri," Manyang ananieleza.
" Katika eneo
hili, miundo msingi ni mbaya sana, hakuna barabara kutoka maeneo ya
mashambani kuja katika eneo hili. Utapata kwamba kuna wale wanaotembea
kwa zaidi ya saa sita kuja katika kliniki hiki.
Sio wote walioweza
kufika, kuna akina mama walemavu, ambao hawakuweza, kwa hiyo ni wale
tuu walio na nguvu waliotembea na kufika hapa. Anasema Manyang
Mojawapo ya watoto wanaotibiwa katika kliniki hii ni Stephen Nyamod mwenye umri wa mwaka moja.
Mama yake,Veronica Nyamod, alitembea kwa zaidi ya saa nne kumleta hapa wiki mbili zilizopita.
Licha
ya matibabu ambayo amekuwa akipokea, afya yake haijaimarika. Madakitari
wanasema uzani wake umepungua tena. Kwa sasa ana kilo 5 tuu. Miguu yake
imekonda, na analia huku madaktari
wakimtibu. Mama yake mwenye umri wa miaka 33 anajaribu kumtuliza.
“
Kile ninachotaka tuu ni afya yake kuwa bora. Nina bahati nilifika
katika kliniki hii. Hatukuwa na chakula cha kutosha katika kijiji chetu.
Kuna watoto wengi wanaougua utapya mlo katika kijiji hicho, “ anasema
Shirika
la Umoja wa Mataifa la kushugulikia watoto UNICEF limeonya kuwa huenda
zaidi ya watoto elfu hamsini wakafariki kufikia mwishoni mwa mwaka huu,
iwapo hawatyapata msaada wa dharura.
Lakini kuna changamoto nyingi
sana zinazokabili juhudi za kutoa chakula na misaada katika maeneo kama
haya. Watu wengi wametoroka vita na sasa wanaisha katika vichaka na
misitu. Wakati huohuo, mashirika ya misaada yamo mbioni kutoa maelfu ya
tani za chakula na dawa kwa waliofuruishwa.
Na huku kukionekana kama hakuna suluhu au mwisho wa mapigano hayo, kuna hofu kuwa hali hii mbaya sasa itakuwa mbaya hata zaidi.
"Kuna
changamoto nyingi sana hassa kuhusu usalama na pia barabara hazipitiki.
Katika maeneo mengi, watu hawajapata msaada wowote tangu mapigano
yalipozuka," anasema msemamji wa Unicef Sudan Kusini, Doune Porter
0 comments:
Post a Comment