………………………………………………………………………….
Na Kibada Ernest-Katavi
Serikali imesema ni aibu kubwa na jambo la fedheha kwa Taifa kuendelea kukabiliwa na janga la udumavu linalotokana na ukosefu wa lishe bora na matunzo sahihi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza katika hotuba yake iliyosomwa siku ya Chakula Dunian kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Rajab Rutengwe .
Amesema ni jambo lisilovumilika kuendelea kupoteza maisha ya zaidi ya watoto 130 na mama wajawazito kila siku kwa ukosefu wa lishe bora na ukuaji wa kiakili wa watoto , kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na kupunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima.
Amewaasa wadau kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha uboreshaji wa lishe miongoni mwa familia na taifa kwa ujumla,Akaongeza kuwa kwa mujibu wa viwango vya ulaji wa mazao ya mifugo Nchini ni wastani wa kilo 12 za nyama , lita 45 za maziwa na mayai 75 za mayai kwa mwaka.
Amesema bado viwango hivi vipo chini ukilinganisha na viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ambavyo ni wastani wa kilo 50 za nyama, lita 200 za maziwa na mayai 300 kwa mwaka,lakini kwa Mkoa wa Katavi hali ni mbaya.
Awali Mwakilishi wa Shirika la Chakula duniani nchini Tanzania Diana Tempelman amesemakuwa wakulima wa kaya hasa wazalishaji wadogo wadogo ni sehemu ya asilimia 70 ya wakazi duniani wasio na chakula cha kutosha ambao wanaishi katika maeneo ya vijijini.
Akaongeza kuwa familia za wakulima zina nafasi kubwa ya kupiga hatua iwapo zitawezeshwa kwa wakati na kutatua changamoto zinazowakabili.
Templeman alisema kuwa watu wanaokaribia milioni 75 ambao hawana chakula cha kutosha hivyo jitihada zaidi zinahitajika,nchi 63 zinazoendelea tayari zimefikia malengo ya millennia katika kukabiliana nautapiamlo mkali ifikapo 2015.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chakula Kilimo na Ushirika Mhandisi Raphael Daluti akitoa salamu za wizara ameeleza kuwa wakati ikiazimishwa siku ya chakula duniani nchi imezalisha chakula cha kutosha mahitaji na kupata ziada kubwa.
Tathimini za awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2013/2014 na hali ya chakula kwa mwaka 2014/2015 inaonesha uzalishaji ni tani milioni 16.02 kati ya kiasi hicho tani milioni 9.8 ni za mazao ya nafaka na tani milioni 6.2 ni za mazao yasiyo nafaka. Kauli mbiu mwaka huu kilimo cha kaya lisha dunia Tunza Mazingira.
0 comments:
Post a Comment