Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Gambo akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuahirishwa kusikilizwa Shauri lake mbele ya Baraza la Maadili.
Afisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Filotheus Manula akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu yaliyojiri katika Baraza la Maadili katika siku yake ya pili ya kusikiliza mashauri yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Na. Ally Mataula – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Wakati
Vikao vya Baraza la Maadili vikiendelea siku yake ya pili kusikiliza
mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya
1995, Baraza hilo likiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Balozi Jaji
(Mst.) Hamisi Msumi limetoa onyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe.
Mrisho Gambo kwa kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza hilo kujibu
tuhuma zinazomkabili.
Kwa
mujibu wa maelezo kutoka kwa Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga ambaye alilieleza Baraza kuwa wao
kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamejiridhisha kuwa
wito wa kuitwa mbele ya Baraza hilo ulimfikia Mlalamikiwa zaidi ya wiki
tatu kabla ya kuanza vikao vya Baraza na hivyo Mhe. Gambo amelidharau
Baraza kwa kitendo chake cha kutofika tarehe 9/10/2014. Hata hivyo, Bw.
Mayunga aliliomba Baraza hilo kuahirisha shauri hilo mpaka Jumatatu
tarehe 13 Oktoba, 2014.
Naye
Mhe. Gambo alipopewa nafasi ya kujitetea kwa kitendo chake cha kukaidi
wito wa kufika mbele ya Baraza alisema kuwa wito wa kumtaka yeye kufika
mbele ya Baraza haukumfikia kutokana na yeye kuwa nje ya kituo chake cha
kazi na badala yake alipata taarifa ya kutakiwa kukamatwa kupitia
vyombo vya habari. Mhe Gambo aliendelea kulieleza Baraza kuwa hakuwa na
sababu ya yeye kukaidi wito huo na kwamba baada ya kupata taarifa
kupitia vyombo vya habari aliwasiliana na Katibu Muhtasi wake ambaye
alimuagiza afungue barua zote zilizofika ofisini kwake kwa jina lake na
kama kuna barua kutoka Tume ya Maadili amtumie kwa njia ya fax. Mhe.
Gambo alisema kuwa baada ya kutumiwa barua hiyo alianza safari ya kuja
Dar es Salaam kuitikia wito wa Baraza.
Akitoa
hitimisho kuhusu shauri hilo, Mhe. Jaji Msumi alisema kuwa amri ya
kukamatwa mlalamikiwa imefutwa. “Mlalamikiwa amepewa onyo la kumtaka
kutii amri ya kisheria ya Baraza. Shauri litasikilizwa tarehe 13/10/2014
saa tatu asubuhi” alisema Mhe. Jaji Msumi.
Kuhusu
Shauri linalomhusu Mbunge wa Kishapu Mhe. Suleiman Masoud Nchambi
Suleiman ambaye analalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kwa kutowasilisha Tamko la Mali na Madeni kwa kipindi cha mwaka
2012 halikusikilizwa kutokana na Mhe. Nchambi kutofika mbele ya Baraza
hilo. Mhe. Nchambi ambaye shauri lake liliahirishwa kusikilizwa katika
vikao vya Baraza vilivyofanyika mwaka jana 2013 katika Manispaa ya
Tabora hakuweza kufika katika vikao vya Baraza vinavyoendelea kufanyika
katika Ukumbi wa Karimjee bila taarifa rasmi ya maandishi.
Kwa
Mujibu wa Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Bibi Mwanarabu Talle ambaye aliliambia Baraza kuwa Mlalamikiwa
anaonekana kuwa ni mkaidi hivyo alipendekeza Baraza kutumia fungu la 24
(4) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya 1995 ambalo
linatoa mamlaka kwa Mwenyekiti kutoa hati ya kukamatwa Mlalamikiwa na
Afisa wa Polisi na kufikishwa mbele ya Baraza.
Akihitimisha
Shauri hilo Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Jaji Msumi alisema kuwa hii
ni mara ya pili kwa Mlalamikiwa kuomba usikilizwaji wa lalamiko lake
kuahirishwa.
“Baraza
lina wasiwasi kuwa huenda Mlalamikiwa ametumia mbinu za kuchelewesha
lalamiko hili. Hata hivyo tunaona ni busara tutoe muda mwingine ambao
utakuwa ni wa mwisho. Hivyo lalamiko linahairishwa hadi kikao kijacho.
Mlalamikiwa afahamishwe kuwa Baraza halitakubali sababu yeyote tena ya
kuahirisha lalamiko hili” Alifafanua Mhe. Msumi.
Kwa
upande mwingine, Baraza la Maadili limeweza kusikiliza mashauri mengine
yanayowahusu viongozi watatu ambao ni Bw. Venance Kenneth Ngunga –
Mhasibu Mkuu, Taasisi ya Technoloji Dar Es Salaam (DIT), Mhe. Mohamed
Ally Chambuso – Diwani Kata ya Mzimuni na Bibi Florence Sastony Masunga –
Diwani Viti Maalum, Kinondoni, wote walikuwa wanalalamikiwa na
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushindwa kuwasilisha
Tamko la Mali na Madeni kwa mujibu wa Sheria.
Pia,
Mhe. Msumi ametoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya Baraza hilo
Bibi Sarah Kinyamfura Barahomoka ambaye ni Mkurugenza Msaidizi – Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukaidi wito wa kufika mbele ya
Baraza kujibu tuhuma zinazomkabili. Kwa mujibu wa ratiba, vikao vya
Baraza la Maadili vitaendelea tena siku ya Jumatatu tarehe 13 Oktoba,
2014.
.jpg)
.jpg)
0 comments:
Post a Comment