Sunday, October 26, 2014


 PG4A6747
WAFANYABIASHARA wa Poland wameiomba Serikali ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kufunguakituo cha biashara katika bara la Ulaya.
Wametoa ombi hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kikao kilichowashirikisha wafanyabiashara wakubwa 30 na wamiliki wa makampuni 20 wa hapa Poland kwenye mkutano uliofanyika katika ofisi za Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Poland (Polish Chamber of Commerce) jijini Warsaw.
Walisema kuwepo kwa kituo hicho barani Ulaya kutawasadia wao kupata taarifa kuhusu Tanzania kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambao wanalazimika kwenda London, Uingereza.
Akijibu maombi yao, Waziri Mkuu alisema ombi lao ni la msingi na atawasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe kuona ni nchi gani kituo hicho kinaweza kuwekwa.

Kwa upande wake, Kaimu wa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Bw. Christopher Mvula ambaye alimwakilisha Balozi Philip Marmo, alisema ili kituo hicho kiweze kuanza kazi, ni lazima pawe na jengo la ofisi za ubalozi, ofisi za kituo cha biashara na watumishi mahsusi. Balozi wa Ujerumani ndiye anayeiwakilisha Tanzania nchini Poland.
“Lazima kuwe na watumishi wa kituo lakini vilevile kuwe na Afisa Biashara, Afisa Utalii na Afisa Uhamiaji ili kuharakisha baadhi ya mambo. Siyo kila afisa wa ubalozi anaweza kuendesha kituo cha biashara,” alisema.
Alisema zitahitajika pia fedha za kulipia matangazo kwenye vyombo vya habari vya nchi husika pamoja na vipeperushi na taarifa nyingine za kuitangaza nchi kupitia kituo hicho.
Waziri Mkuu alimaliza ziara yake ya siku tatu nchini Poland jana mchana ambapo asubuhi alikutana na Watanzania waishio Poland na baadaye kukutana na baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la Warsaw.

0 comments:

Post a Comment