RAIS Jakaya Kikwete ameanza ziara ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China huku akiwalilia Meja Jenerali Herman Lupogo (76) na Kapteni mstaafu John Barongo (72), ambao wamefariki dunia baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Kikwete ametuma salamu za rambirambi na pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kuomboleza kifo cha Meja Jenerali Lupogo ambaye aliaga dunia Oktoba 19, 2014, katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, ambako alikuwa anapata matibabu.
Rais Kikwete alimweleza Meja Jenerali Lupogo kama mzalendo halisi, ofisa mtiifu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyeitumikia nchi yake kwa moyo wote na wakati wote.
Pia Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kufuatia kifo cha Kapteni mstaafu Barongo kilichotokea Oktoba 20, 2014 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Chama kimempoteza mtumishi wake wa muda mrefu na muaminifu, ambaye amefanya kazi zake bila kuchoka na hata baada ya kustaafu amebakia kuwa muaminifu na mwanachama imara,”alisema.
Rais aliongeza kuwa marehemu amekuwa mtumishi hodari katika jeshi, chama na serikali, hivyo mchango wake utathaminiwa siku zote.
Marehemu Kapteni mstaafu Barongo alizaliwa Desemba 1, 1942 katika kijiji cha Katoja,Wilaya ya Bukoba Mjini mkoani Kagera. Alianza utumishi wake katika Chama cha TANU mwaka 1963 na kuendelea hadi CCM katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Mara, Manyara, Shinyanga, Dar es Salaam na Dodoma.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana ameanza ziara ya siku sita nchini China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping, ikiwa ni ziara yake ya pili nchini humo akiwa Rais wa Tanzania.
Taarifa ya Ikulu imesema kuwa baada ya China, Rais Kikwete atafanya ziara ya siku tatu nchini Vietnam kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo.
Wakati wa ziara yake nchini China, Rais Kikwete atatembelea majimbo matatu ya nchi hiyo, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu, atashuhudia utiaji saini mikataba muhimu ya shughuli za maendeleo, atatunukiwa shahada za heshima na atashiriki katika sherehe za miaka 50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na China.
Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Xi Jinping; Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Zhang Dejiang.
Pia atashuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maendeleo ya Tanzania ambayo inasaidiwa ama inagharimiwa na fedha kutoka China na pia atakutana kwa mazungumzo na wakuu wa taasisi muhimu zinazogharimia baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo katika Tanzania zikiwamo China-Africa Development Fund (CADB) na China Development Bank(CDB).
Chanzo: Tanzania Daima
Mwili wa aliyekuwa Meja Jeneral Herman Corner Lupogo aliyefariki 19 mwezi huu wa kumi unatarajiwa kuagwa kesho katika eneo maalumu la Hospitali kuu ya jeshi lugalo jijini Dar es salaam.
Marehemu lupogo alijiunga na jeshi la ulinzi la wananchi wa tanzania julai 23 mwaka 1965 na hivyo kuweza kutunukiwa kamisheni januari 21 mwaka 1966.
Katika utumishi wake enzi za uhai wake alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya mkurugenzi wa mafunzo makao makuu ya jeshi 1971 hadi 1974, katibu msaidizi makao makuu ya chama (ulinzi na usalama) 1974 hadi 1976, mkuu wa chuo cha taifa cha uongozi (monduli) 1976 hadi 1978.
Marehemu meja jeneral lupogo nimzaliwa wa mkoa wa ruvuma na amezaliwa desember 12 mwaka 1938 wilayani mbinga mkoani ruvuma, na katika elimu yake aliyoipata aliweza kuhitimu stashahada ya ualimu na shahada ya kwanza ya sanaa katika chuo kikuu cha makerere nchini uganda mwaka 1958 hadi 1964.
Katika utumishi wake alihudhuria kozi mbalimbali ikiwemo ukamanda na unadhimu nchini canada 1969 na international strategic studies nchini uingereza 1985,na amelitumikia jeshi kwa muda wa miaka 28.
Marehemu amefariki akiwa mstaafu ameacha mke na watoto, Mwenyezi mungu ailaze roho ya Meja Jenerali Hermani Corneli Lupogo (mstaafu) Roho mahali Pema Amina.
Wednesday, October 22, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments:
Post a Comment