Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari ya kusafiri nchini Uganda baada ya kuthibitishwa kuwa daktari mmoja amefariki kutokana na ugonjwa hatari wa Marburg unaosambazwa na popo.Kwa sasa Shirika hilo kwa ushirikiano na mamlaka za afya za Uganda wamemzuilia ndugu mmoja wa marehemu kwa hofu kuwa huenda naye aliambukizwa. Watu wengine zaidi ya 80, wakiwemo matabibu 38 waliokutana na mwenzao huyo siku kumi kabla ya kifo chake nao pia wanachunguzwa.
Kwa mujibu wa WHO na mamlaka za afya za Uganda, matokeo ya uchunguzi katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Virusi kufuatia kifo cha tabibu huyo tarehe 28 Septemba yanathibitisha kwamba alifariki kutokana na homa hiyo hatari ya Marburg. Waziri wa Afya wa Uganda, Erioda Tumwesigye, alisema kuwa wizara yake inathibitisha daktari huyo aliyekuwa mtaalamu wa vipimo vya mionzi, alikufa kwa Marburg.
Marehemu alikuwa tabibu katika Hospitali Kuu ya Wilaya ya Mpigi na alianza kuugua tarehe 17 Septemba akihudumu katika hospitali ya Mengo jijini Kampala, ambako alikuwa ameajiriwa mwezi mmoja uliopita. Inahofiwa kwamba katika kipindi cha wiki mbili kabla ya kifo chake alikutana na watu wengi wakiwemo matabibu wenzake pamoja na kwamba ni jamaa zake waliomzika.
0 comments:
Post a Comment