Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiendelea na kazi ndogo ndogo wakati
akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Johns Hopkins huko
Baltimore Maryland nchini Marekani
MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), kwa mara nyingine tena,
jana alinusurika kichapo kutoka kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF),
baada ya kuwapasha kwamba wanatibiwa nchini India, kwanini wanahoji
Rais Jakaya Kikwete kutibiwa Marekani.
Kessy alizua kizaazaa hicho wakati Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
alipokuwa akijibu miongozo mbalimbali ya wabunge, ukiwemo wa Kessy.
Mbunge huyo ambaye sasa ni mara ya tatu kukwaruzana na wabunge wa CUF
kutoka Zanzibar, aliomba mwongozo wa Spika na alipopata nafasi alihoji
sababu ya wabunge wa Zanzibar kuhoji matibabu ya Rais Kikwete
aliyefanyiwa upasuaji nchini Marekani wakati wao wamekuwa wakitibiwa
India kwa gharama za Serikali.
“Mheshimiwa Spika, hawa Wazanzibar wanaohoji Rais Kikwete kutibiwa
India, wanakosea sana, mbona wao wanatibiwa India, hatusemi kitu.
Nawajua wabunge zaidi ya sita waolitibiwa India, kuna kosa gani Rais
Kikwete kutibiwa Marekani, au mlitaka akatibiwe Zanzibar, kwendeni zenu
huko,” alimalizia kwa kusema Kessy na hivyo kuibua kizaazaa.
Kauli hiyo ya Kessy iliwaibua wabunge wote wa kambi ya upinzani ambapo
baadhi yao walipaza sauti kutaka atolewe bungeni, lakini wabunge wengine
wa CUF, wakiongozwa na Khatibu Said Haji (Kondo), walinyanyuka kwenye
viti vyao na kumfuata kwenye kiti chake.
Lakini kabla ya kufikiwa, Kessy alisimama na kuchomoka kwa kasi kutoka
nje, huku askari wa Bunge wakiwazuia wabunge wa CUF waliokuwa na jazba
wasimfuate.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), alifanya kazi kubwa
kumzuia mbunge wa Kondo, Khatib ambaye alionekana dhahiri kupania
kumtandika Kessy.
Kabla ya Kessy kuanzisha sarakasi hiyo, mbunge wa Viti Maalum, Rukia
Kassim Ahamed (CUF), aliomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge lisitishe
kujadili Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Taifa mwaka wa fedha
2015/2016 ili lipate nafasi ya kujadili deni la Serikali la zaidi ya sh
bilioni 100, linalodaiwa na Bohari ya Madawa nchini (MSD), na
kusababisha uhaba mkubwa wa dawa kwa wananchi nchini.
Mbunge huyo alisema hakuna sababu ya wao kuendelea kukaa bungeni na
kupigwa kiyoyozi huku Rais Kikwete akienda kutibiwa Marekani wakati
wananchi vijijini wakipoteza maisha kwa kukosa dawa, kauli ambayo
ilimuibua Kessy na kujibu mapigo.
Hii ni mara ya tatu kwa Kessy kutibuana na wabunge wa Zanzibar na kuzua
kizaazaa. Mara ya mwisho ilikuwa katika Bunge Maalum la Katiba ambapo
mbunge huyo alisema Zanzibar inabebwa katika masuala la Muungano na
kwamba haichangii chochote.
Kauli kama hiyo alishawahi kuitoa katika Bunge la Bajeti ambapo alisema
Zanzibar inainyonya Tanganyika na kwani haichangii chochote katika
masuala ya Muungano, kauli ambayo mara zote imekuwa ikimletea matatizo
na wabunge kutoka Zanzibar ambao wanadai ni ya kibaguzi.
Rais Kikwete, amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostate), katika
Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland,
Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva
Rweyemamu kwa vyombo vya habari juzi ilisema Rais Kikwete amefanyiwa
upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa
afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.
Inaelezwa kuwa upasuaji huo ulichukua kiasi cha saa moja unusu,
umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa na wananchi wataendelea
kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais kwa kadri zitakavyokuwa
zinapatikana.
Afya ya JK yaimarika
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, hali ya
Rais Kikwete inaendelea kuimarika na kuwa nzuri huku akiwa ameanza
kufanya mazoezi ya kutembea tangu juzi.
“Rais Kikwete ameanza kufanya mazoezi ya kutembea siku ya pili tu baada
ya kufanyiwa operesheni. Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
itaendelea kuwapatia wananchi habari sahihi kuhusu maendeleo ya afya
yake kadri habari hizo zitakavyokuwa zinapatikana,” ilisema taarifa
hiyo.
Pia, Ikulu iliwashukuru wote ambao wamekuwa wakimwombea Rais Kikwete ili
apone haraka na kurejea nyumbani kujiunga na wananchi wenzake katika
ujenzi wa taifa.
Habari kwa hisani ya Gazeti la Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment