Abdallah Gama
ABDALLAH GAMA MPIGA RYTHM MWENYE HISTORIA NDEFU
SINA-shaka wale mashabiki wa DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ Ngoma
ya Ukae’ ambao ni vijana wa zamani, watakuwa wanakumbuka mbali kila pale
linapotajwa jina la mwanamuziki Abdallah Gama.
Gama ni mkung’utaji mahiri wa gitaa la kati, Rhythm, aliyepata kusumbua
akili za wapigaji magitaa wengine wengi enzi zile, hususan alipokuwa
katika bendi hiyo ya Sikinde.
Nguli huyo ni mmoja miongoni mwa wanamuziki 12 ambao mwaka 1978
walijiengua kwenye kundi la Dar International kwa madai ya kupinga
uongozi mbovu wa mmiliki wao, Zachariah Ndabameiye na kuanzisha Sikinde.
Baadhi ya wanamuziki wengine waliochomoka Dar International na kwenda
kuanzisha Sikinde wakati huo, walikuwa ni Cosmas Chidumule, Abel
Bartazal, Joseph Mulenga, Michael Enock, George Kessy, Machaku Salum,
Haruna Lwali na Ibrahim Mwinchande.
Akiwa Sikinde, Gama aliweza kujipatia umaarufu mkubwa, hasa kwa umahiri
aliokuwa nao katika kulicharaza ipasavyo gitaa la Rhythm kwenye vibao
vingi vya bendi hiyo.
Kadhalika, ni mwanamuziki aliyegusa nyoyo za mashabiki wengi kutokana na
tungo zake kadhaa zenye ujumbe mzito, kama vile; ‘Hadija’, ‘Dar es
Salaam Airport’, ‘Maudhi ya Nyumbani’, ‘Linda’ na ‘Nawashukuru Wazazi’.
Kwa upande wa Dar International aliyoitumikia kuanzia mwaka 1977, Gama
alishiriki kupiga Rhythm kwenye vibao vingi, baadhi yake vikiwa ni
‘Sikitiko’, ‘Mwana Rudi Uoe’ na ‘Mwalimu Nyerere’.
Tulimtafuta Gama na kuzungumza nae kwa faida ya wasamomaji, ambapo
mwenyewe anaanika mambo mengi kuhusiana na historia yake kimuziki na
maisha kwa ujumla.
“Baba yangu aliyekuwa fundi cherahani, ndiye aliyenivuta kwenye muziki
kwani alikuwa akipiga gitaa lisilitumia umeme, Galaton kujifurahisha na
wakati mwingine akiburudisha rafiki zake,” anasema Gama.
Gama anasema kuwa, akiwa na umri wa miaka 28, alikuwa tayari anafahamu
barabara kukung’uta gitaa nabendi yake ya kwanza ilikuwa ni Safari
Trippers aliyojiunga nayo mwaka 1973.
Akiwa na Safari Trippers, Gama anasema kuwa, alishiriki kupiga Solo
kwenye vibao kadhaa, vikiwamo ‘Ooh Lila’ na ‘Mateso’ ambavyo vyote ni
makucha ya marehemu Marijani Rajab.
Gama asiyependezwa na tabia ya wanamuziki kuhamahama makundi, anasema,
mwaka 1975 alijiunga na bendi ya Tanzania Stars ambayo maskani yake
ilikuwa ni katika hoteli ya Margot, iliyokuwa mtaa wa Independence (siku
hizi mtaa wa Samora) jijini Dar es Salaam.
Ifahamike pia kuwa, mwaka 1984 Gama aliwahi kuitumikia Bima Lee kwa
mwaka mmoja akitokea Sikinde, ambapo hata hivyo alitoka na kurejea tena
Sikinde mwishoni mwa mwaka 1985.
“Nikiwa Bima Lee nilitunga kibao ‘Fungua Macho’, pamoja na kushiriki
kucharaza gitaa kwenye vibao kama vile; ‘Makulata’ na ‘Tujemaso’,”
anasema Gama.
Mwishoni mwa mwaka 1985 aliingia nchini Kenya kwa kupitia bandari ya
Tanga na kujiunga na bendi ya Super Mazembe iliyokuwa ikitumbuiza kwenye
ukumbi wa Garden Square, jijini Nairobi.
Wengi wanaamini kibao ‘Gama Unisamehe’ cha Sikinde amekitunga yeye, kama
nawe u mmoja kati ya watu hao, basi umekosea, kwani Gama mwenyewe
anaeleza hivi:
“Kibao kile kimetungwa na Tshimanga Kalala Asossa, tukiwa Zanzibar
kwenye shoo, mimi nilikuwa Kiongozi wa Jukwaa, sasa kabla hatujaanza
kutumbuiza nilipanda jukwaani na kuwaita wanamuziki kwa kutumia mlio wa
gitaa langu.”
Gama anaendelea kueleza kuwa, ghafla alimuona Asossa aliyekuwa anapenda
kutembea na redio ndogo ya kurekodi sauti, na kurekodi kipande
alichokuwa anakipiga kisha akaondoka.
Waliporudi Dar es Salaam, kwenye mazoezi Asossa alikuja na mashairi ya
wimbo na kile kipande alichokipiga Gama kule Zanzibar kuanzia muziki wa
wimbo huo alioamua kuupa kumbukumbu kwa kuuita ‘Gama Unisamehe’.
“Mafanikio niliyokwishayapata kwenye muziki ni kutembea nchi nyingi
duniani, jambo ambalo sikutarajia hapo kabla,” anasema Gama huku
akikumbuka ziara yake na bendi ya Malembe Stars nchi za nje.
Gama anayejivunia kusomesha watoto wake wote hadi chuo kikuu,
anazikumbuka nchi hizo kuwa ni kama vile; Japan Malaysia, Ufilipino,
Pakistan na Misri.
Kwa sasa Gama ambaye ni baba wa watoto wanne; Mgeni, Pili, Hadija na
Maimuna, yuko katika bendi ya Excel ya jijini Dar es Salaam, huku akiwa
na malengo ya kuanzisha bendi yake binafsi.
Mpango mwingine alionao Gama, ni kurudia kuvirekodi upya vibao vyake vya
zamani, alivyovitunga akiwa na bendi za Sikinde na Bima Lee, kutokana
na shinikizo la mashabiki wake.
Mwisho. - Source JF
|
0 comments:
Post a Comment