Saturday, November 29, 2014

Tunapoendelea kufuatilia bunge letu, ambalo kwa kweli limekuwa tukufu sana katika saga hili la Escrow, naomba tuzingatie mambo matatu yanayojitokeza:


i) Bunge letu limewekewa mipaka mikubwa sana kikatiba katika kuiajibisha serikali. Kikatiba, Bunge halina uwezo wa kumfukuza mtu yeyote kazi zaidi ya Rais, Waziri Mkuu na Spika. Bunge lina mamlaka ya kuwafukuza hawa kwa sababu bosi wa wananchi ni Rais na hivyo Bunge linaweza kumfukuza Rais kwa niaba ya wananchi. Bunge linaweza kumfukuza Waziri Mkuu kwa sababu ndilo lilimthibitha katika uteuzi wake. Kwa hiyo, technically, Waziri Mkuu anateuliwa na mihimili miwili-Rais na Bunge. Bunge linaweza kumfukuza spika kwa sababu ndilo lililomchagua. Kwa hiyo, tunapowakomalia wezi wetu wafukuzwe ni muhimu pia kuanza kufikiria namna ya kulipa meno zaidi Bunge katika Katiba. Kwa hiyo tuisome katiba pendekezwa vizuri na kama haina mambo haya hiyo itakuwa sababu nyingine ya kuikataa. Hii ndilo lile ambalo rafiki yangu Mimi Mwanakijiji amelikazania kwamba tuwekeze katika kufix mfumo pia badala ya kuhangaika na watu tu! Lakini mie namwambia rafiki yangu huyu kwamba huu mfumo haurekebishiki bila kwanza kuifukuza CCM madarakani!! Wakati hatujafanikiwa kuitoa CCM madarakani inabidi tuendelee na kuhangaika na wabaya wetu zaidi ndani ya mfumo huu.

ii) Ni wazi kwamba wabunge hawana imani tena na waziri jeuri Profesa Muhongo kutokana na kiwango alichowadanganya. Hata Profesa mwenzake Mwandosya amekiri waziwazi kwamba kulikuwa na pesa ya umma katika akaunti ya Escrow. Na katika hitimisho lake Zitto ameonyesha tena kiwango ambacho Muhongo amelidanganya Bunge kwa kutumia takwimu za kijiolojia katika kuchambua takwimu za kiuchumi hasa pale alipojaribu kuonyesha kwamba eti Tanesco haina hela kwenye Escrow kwa sababu tu inadaiwa sana. Hili Zitto amelieleza kwa ufasaha mno kwa kiwango ambacho Muhongo alipaswa kukiri hadharani kwamba alichemsha. Sasa serikali ina hiari iendelee kubaki na Muhongo ambaye wabunge hamwamini kwa kiwango hicho. Na akiendelea kubaki katika nafasi yake ya uwaziri, ni mbunge gani atakayeamini majibu ya Muhongo bungeni? Ndiyo kusema kwa serikali kumng'ang'ania Muhongo maana yake inajiweka katika mazingira ya kuzidi kutokuaminiwa na wabunge na inajiweka kwenye mtego wa kuanzishiwa mchakato wa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Rais.

iii) Tusiwakatisha tamaa majemadari wetu pale wanapoteleza. Tusiwe wepesi wa kuhukumu. Raha ya majadiliano ni kwamba kuwe na hoja kinzani. Nalisema hili kwa sababu nimeona kuna watu walikwazika sana na kitendo cha Zitto Z Kabwe kuunga mkono phrasing ya Chenge. Kimsingi Zitto alikuwa mbele yetu katika kufikiri pamoja na kwamba baadaye alisema alikuwa amechoka. Kama ile phrasing ingeenda kama ilivyopendekezwa na Zitto ina maana kwamba ingemgusa hadi waziri mkuu ambaye wabunge wa CCM hawataki kabisa aguswe. Ndiyo maana Spika Makinda ghafla akabadili azimio ambalo tayari lilishapigiwa kura. Rafiki yangu mwingine Ezekiah Wenje alilishtukia hili. Kwa vyovyote vile tusiwachukulie majemadari wetu kama malaika ambao hawatafanya makosa. Watafanya makosa lazima na tuwakosoe inapokuwa wamekosea, lakini tuache tabia ya kuitana majina.

0 comments:

Post a Comment