SAKATA la ubadhirifu wa bilioni 40
katika halmashauri ya jiji la Mwanza limechukua sura mpya baada ya
maofisa wa ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)
walioibua sakata hilo kudai kutishiwa maisha.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab
Mohammed Mbarouk wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yao mkoani hapa
ambacho hakikuendelea kufanyika kutokana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Hawa Ghasia au mwakilishi wake kutofika katika majumuisho
hayo.
“Tumepokea taarifa ya kutishiwa amani
kwa baadhi ya wakaguzi, tunasema ofisi ya CAG ipo kisheria na kikatiba
na wanafanya kazi kwa kufuata sheria na Katiba,” alisema Mbarouk na
kuongeza kuwa, kama wabunge watahakikisha wanatunga sheria na
kuzisimamia na kwamba wakaguzi waendelee na kazi yao bila ya hofu.
Mbarouk alimpongeza Mkaguzi Mkazi pamoja
na timu yake kwa kuwa na uzalendo wa kitanzania wa kutaka kuokoa uchumi
wa Mwanza ambao kwa asilimia 90 unahujumiwa.
Alisema uchumi wa Mwanza unatokana na
mapato na miradi ya maendeleo ambapo maeneo hayo yakifanyiwa kazi
isiyoridhisha CAG anawajibu wa kutoa taarifa.
Alisema kama Mkaguzi Mkazi ameweza
kuwasilisha taarifa yake kwa Bunge pamoja na kwa Rais. Awali, Mjumbe wa
kamati hiyo, Kange Lugora alisema kamati hiyo iliishauri wizara husika
kushirikiana nao pamoja tangu mwanzo wa ziara yao katika majumuisho ya
kamati hiyo ili kubaini yanayotendeka katika miradi ya maendeleo.
“Kitendo cha wizara kutoshiriki katika
majumuisho ya kamati hii ni kuendelea kuhalalisha ubadhirifu unaoendelea
kwenye halmashauri, tunaonyeshwa miradi hewa na serikali ngazi ya
wizara ilipaswa wajionee wenyewe,” alisema.
Aliongeza kuwa, ili waweze kuwatendea
haki Watanzania na wana Mwanza, kamati iliagiza kuwa hawawezi kuendelea
na mahesabu ya halmashauri ya jiji la Mwanza hadi wizara itakapomrudisha
Mkurugenzi wa zamani wa jiji hilo, Wilson Kabwe ambaye kwa sasa
amehamishiwa Dar es Salaam.
Alisema kwamba wizara haijafanya
jitihada za kumrejesha mkurugenzi huyo na kudai kuwa mazingira hayo
yanawafanya washindwe kuwatendea haki Watanzania.
Alisema ili kamati ilinde heshima yake
na kwa mazingira hayo hawataweza kufanya majumuisho kwani kwa kufanya
hivyo ni kuwasaliti Watanzania.
Grace Chilongola, Mwanza

0 comments:
Post a Comment