MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, kurudisha mifuko 700 ya saruji ambayo alimkabidhi ikiwa ni mchango wake katika ujenzi wa maabara za shule za Sekondari.
Akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani kilichofanyika juzi wilayani hapa, Mahiza alisema alimkabidhi Kipozi mifuko ya saruji 1,000 kwa ajili ya ujenzi wa maabara, ambako Mkuu huyo wa Wilaya aligawa mifuko 300 pekee katika baadhi ya Kata huku 700 haijulikani ilipo.
“Katika Mkoa wangu niligawa kila Wilaya mifuko ya saruji na Kipozi nilimkabidhi mifuko 1,000 cha kushangaza aligawa 300 katika baadhi ya kata sasa 700 iko wapi? nakupa siku mbili hiyo mifuko uwe umeshairudisha huko ulikoipeleka,” alisisitiza Mahiza.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ulikula kiapo na ukaahidi unaweza kazi, nitasikitika kama agizo hili litakuwa limepokelewa kisiasa, sitaki kuamini kwamba Tanzania kuna mwananchi ambaye hajui umuhimu wa elimu, na msidhani Serikali ni Kikwete pekee, Serikali ni wewe na mimi tusioneane haya kuambizana ukweli tunapokubaliana jambo, niwapende kiasi gani? Alihoji.
Katika hatua nyingine, Mahiza alimwagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shukuru Mbato, kusitisha vikao vya mara kwa mara kwa madiwani ili wasimamie ujenzi wa maabara kwenye kata zao.
Alisema ni jambo la aibu Mkoa wake umekuwa wa mwisho katika utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete, la kujenga maabara tatu katika kila Kata yenye shule ya Sekondari.
“Nimekubali nabii hathaminiwi kwao, agizo limetolewa na Mheshimiwa Rais Novemba mwaka jana, leo hii Wilaya anayotoka ndio wanalijadili na kuanza kupanga mipango yake hii ni aibu, mwenyekiti sitisha vikao vyote na kila diwani abaki kwenye kata yake kusimamia ujenzi wa maabara,” alisema Mahiza.
Aidha aliwasihi madiwani kuwatumia wawekezaji waliopo katika Wilaya hiyo kuhakikisha wanawasaidia katika mradi huo, kwani kuchelewa kuanza ujenzi huo ni kutokana na kukosa muongozo thabiti wa kusimamia kazi hiyo.
“Kuanzia leo nimeamua kuhamia Bagamoyo kuhakikisha zoezi hili linaanza haraka na kukamilika mapema, kila Mkuu wa Idara aende kwenye kata moja awe mlezi na ahamie huko kuanzia kesho, mimi mwenyewe nasitisha kazi zangu nimekuja huku wewe Mkuu wa Idara unakaa ofisini kufanya nini wakati huku nje mambo hayaendi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Halmashauri hiyo, ililazimika kusaini mkataba wa sh bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi wa maabara 17 na Kampuni ya Mzinga iliyo chini ya Wizara ya Ulinzi ambayo imeahidi kujenga ndani ya mwaka mmoja.
FREEMEDIA
0 comments:
Post a Comment