HATIMAYE mvutano kati ya Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) na Serikali umefikia kikomo baada ya pande mbili
hizo kukubaliana na Rais Jakaya Kikwete kuboresha Katiba ya mwaka 1977
na kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.
Hatima hiyo ilifikiwa jana kwenye kikao
kilichofanyika kati ya Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) kinachoundwa na vyama vyenye wabunge ambavyo ni CCM, Chadema,
NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, UDP na UPDP inayowakilisha vyama visivyo wa
wabunge, kilichofanyika Ikulu ndogo mjini Dodoma.
Mkutano wa awali wa viongozi hao
ulifanyika Agosti 31, mwaka huu, katika Ikulu ya Kilimani, mjini Dodoma
ambapo walipeana majukumu ya kufanya ili kuangalia namna bora ya kufikia
mwafaka.
Katika mkutano wa jana, chanzo cha
habari kutoka ndani ya mkutano huo kilieleza kuwa viongozi hao
walikubaliana kuwa kutokana na mazingira ya sasa, ni vigumu kupata
Katiba mpya ambayo itatumika mwakani.
Kutokana na hali hiyo, viongozi hao
walikubaliana kuwa ni vyema vyama hivyo vikakaa na kuangalia mambo
muhimu ya kuwekwa kwenye Katiba ya sasa.
“Vyama vinatakiwa vikae na kuangalia ni
nini cha kuchukuliwa na kuwekwa kwenye Katiba hii ya sasa, baada ya
kumaliza Uchaguzi Mkuu ndiyo sasa turudi kwenye mchakato wa kuandika
Katiba mpya,” alisema.
Alisema kuwa baada ya vyama hivyo kukaa
na kukubaliana kitu cha kuweka kwenye Katiba inayotumika sasa,
watayapeleka mapendekezo hayo serikalini kisha muswada wa marekebisho ya
Katiba utapelekwa bungeni.
Kwenye suala la kuahirishwa kwa Bunge, chanzo kingine kilisema kuwa halikuzungumziwa, lakini busara inatarajiwa kutumika zaidi.
Mwenyekiti TCD
Akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo,
alisema kuwa wamekubaliana kindugu.
Waandishi wa habari walipotaka afafanue
kauli yake na kama kukubaliana huko kunamaanisha kusitisha Bunge ama
Ukawa kurudi bungeni, Cheyo alisema: “Mimi naongea kama mwenyekiti wa
vyama vyote, tumekubaliana kindugu, mazungumzo yalienda vizuri na kesho
nitatoa taarifa kamili.”
Mwanasheria Mkuu
Agosti 16, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Frederick Werema, alizungumzia ugumu wa rais kuvunja Bunge
la Katiba na kusema Katiba mpya ikishindwa kupatikana, iliyopo sasa
itafanyiwa marekebisho.
Jaji Werema alikuwa akizungumzia hatima
ya upatikanaji wa Katiba mpya na mwenendo wa vikao vya kamati za Bunge
Maalumu vinavyoendelea sasa Dodoma, ambavyo vimesusiwa na wajumbe
wanaounda Ukawa.
Alisema tathmini iliyofanyika ya
mwenendo wa vikao hivyo, imeonyesha kuwa theluthi mbili inayohitajika
ili kupitisha vifungu vinavyojadiliwa inapatikana, isipokuwa wasiwasi
umebaki kwenye kupitisha vifungu hivyo wakati wa vikao vya pamoja vya
wabunge wote.
Jaji Werema alisema kwa kutambua hilo,
iwapo akidi ya theluthi mbili ya wajumbe haitapatikana wakati wa
kupitisha Katiba iliyopendekezwa, baadhi ya vifungu vitakavyopitishwa
vitachukuliwa na kupelekwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili
ya kuingizwa kwenye Katiba ya sasa ya mwaka 1977.
“Kwa sasa akidi kwenye kamati inatosha,
tukifikia Bunge kuja na Katiba inayopendekezwa na kama hakuna theluthi
mbili, tutarudi kwenye Bunge la kawaida (Bunge la Jamhuri ya Muungano)
na kukubaliana, yaliyokuwa hayana ubishi tutayaweka na kuyatumia kwenye
Katiba ya sasa, likiwamo suala la mgombea binafsi,” alisema Jaji Werema.
mtanzania
0 comments:
Post a Comment