
Dar es Salaam. Baada ya taji la Miss Tanzania kuvishwa kwa mshindi wa pili, utata mwingine umeibuka baada ya mrithi huyo, Lilian Kamazima kudaiwa kuwa si raia.
Jana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kulikuwa na taarifa zinazodai kuwa Lilian siyo raia wa Tanzania na kwamba anatokea Rwanda.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndiyo waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim ‘Uncle’ Lundenga alisema tuhuma hizo kuhusu Lilian siyo kweli.
“Sisi tunajua Lilian ni Mtanzania, tunaangalia cheti cha kuzaliwa alichotuletea kamati yetu ambacho kinaonyesha alizaliwa Tanzania, pia ni Mtanzania, hayo yanayosemwa kwamba Lilian siyo Mtanzania hatuyajui kabisa,” alisema Lundenga.
Pia Lundenga alisema kitendo cha Sitti Mtemvu kujivua taji la Miss Tanzania 2014 kumemnyima sifa ya kuendelea kushikilia taji la Miss Temeke na lile la Kitongoji cha Chang’ombe.
0 comments:
Post a Comment