Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichomalizika jana, zilidai kuwa mpango huo wa Pinda ambaye hivi karibuni alitangaza nia ya kuomba kuwania urais, ulikuwa unasukwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma. “Ndiyo maana wakati wa kumchagua mgeni rasmi wa kufungua kikao chetu walimwita Pinda ili aweze kulainisha safari ya kwenda kumteua kuwa naibu kamanda,” kilisema chanzo kutoka katika kikao hicho.
Katika kikao hicho, Sadifa aliyekuwa akiungwa mkono na Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda na Katibu wa Uchumi wa UVCCM Zanzibar, Omary Suleiman, wajumbe walimkatalia kwa hoja kuwa Pinda ataleta mgawanyiko ndani ya umoja huo kwa sababu ni mmoja wa wagombea urais.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa sababu zilizotolewa na Sadifa ni kuwa, kwa sababu wameteua makamu wa pili wa Rais Zanzibar kuwa naibu kamanda Zanzibar, ni vyema upande wa pili wa Muungano ukawa na naibu anayefanana naye kicheo.
“Wajumbe wa kikao hicho walipendekeza Dioniz Malinzi awe naibu kamanda kwa sababu kwa nafasi yake kama mwanamichezo ana ushawishi mkubwa kwa vijana,” kilisema chanzo hicho.
Habari zilisema Sadifa alikataa kuteuliwa kwa Malinzi kwa sababu ana uhusiano na mmoja wa vigogo wanaotajwa kuwa katika mbio za urais. Hata hivyo, Sadifa aliwaomba wajumbe wa Baraza Kuu kukasimu mamlaka yake kwa Kamati ya Utekelezaji katika suala hilo, jambo ambalo pia lilipingwa vikali.
“Wajumbe walimtaka mwenyekiti kwenda kutafakari na kurejea na jina la Naibu Kamanda katika kikao kijacho,” alisema.
Wakati wa kufunga Baraza hilo jana, Sadifa alisema Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ameteuliwa kuwa Kamanda Mkuu wa umoja huo na Balozi Seif Ali Idd, kuwa Naibu Kamanda Mkuu wa Zanzibar na kuwataka wajumbe waendelee kuvuta subira wakati wakifanya mchakato wa kumpata naibu kamanda Bara.
Sadifa, Mapunda wazungumza
Akizungumzia sakata hilo, Sadifa akiwa ameongozana na Mapunda, alisema hakuna suala la uteuzi wa Pinda wala Malinzi lililozungumzwa katika kikao hicho.
“Kwanza mimi kikanuni nina mamlaka ya kuteua makamanda bila hata kuomba ushauri kutoka kwa mtu, lakini mimi kwa sababu ninaamini katika demokrasia shirikishi, nawaachia watu wa Bara wenyewe wachague, waniletee wanayemtaka,” alisema na kuongeza:
“Kwa upande wa Zanzibar hakuna neno, mimi nawafahamu wote kwa hiyo ndiyo maana nilikuja na jina la Balozi Seif.”
0 comments:
Post a Comment