![]() |
| Atupele aliibukia Yanga B |
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
SIMBA
SC imeonyesha bado haiko tayari kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
baada ya jioni leo kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Huo
ni mchezo wa kwanza kwa Simba SC kupoteza katika msimu huu baada ya
mechi nane, lakini imeshinda mechi moja na kutoa sare sita awali, hivyo
inabaki na pointi zake tisa.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, hadi mapumziko
Kagera Sugar walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na
mshambuliaji wa zamani wa Yanga B, Atupele Green.
Atupele
alifunga bao hilo kwa shuti akimalizia mpira wa kurushwa na Benjamin
Asukile, ambao kabla ya kuingia nyavuni ulimbabatiza beki wa Simba SC,
Hassan Isihaka.
Kipindi
cha pili, Kocha wa Simba SC Mzambia Patrick Phiri alianza na mabadiliko
akimpumzisha kiungo Ramashani Singano ‘Messi’ na kumuingiza
mshambuliaji Elias Maguri.
Baada
ya kuona mambo hayaendi kama alivyotarajia, kocha Phiri akafanya
mabadiliko mengine dakika tano baadaye, akiwapumzisha Awadh Juma na Dan
Sserunkuma na kuwaingiza Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Said Ndemla.
Kocha
wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja alifanya mabadiliko ya kwanza dakika
ya 70, akimpumzisha Benjamin Asukile aliyeumia na nafasi yake kumuingiza
Victor Hussein.
Ndemla
alikaribia kuifungia Simba SC bao la kusawazisha dakika ya 77 baada ya
kupata pasi nzuri ya Hassan Ramadhan Kessy, lakini akapiga mpira juu ya
lango.
Kagera
Sugar ilipata pigo dakika ya 88 baada ya mchezaji wake Babu Ali Seif
kuumia na kupoteza fahamu kiasi cha kusababisha mchezo kusimama kwa
dakika tatu, kabla ya kutolewa na nafasi yake kuingia Simon Lucas.
Mayanja akafanya mabadiliko mengine dakika ya 89, akumuingiza Juma Mpola kuchukua nafasi ya Daud Jumanne.
Kikosi
cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Ramadhan Kessy, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude,
Ramadhani SIngano ‘Messi’/Elias Maguri dk46, Awadh Juma/Shaaban Kisiga
‘Malone’ dk50, Dan Sserunkuma/Said Ndemla dk50, Simon Sserunkuma na
Emmanuwl Okwi.
Kagera
Sugar; Agaton Anthony, Salum Kanoni, Abubakar Mtiro, Erci Kyaruzi,
George Kavilla, Malegesi Mwangwa, Paul Ngway, Babu Ali Seif, Atupele
Green, Daud Jumanne na Benjamin Asukile.

0 comments:
Post a Comment