Add caption
|
Staa wa filamu Bongo Jacqueline Wolper Massawe akisalimiana na Sista wa Kanisa Katoliki la Msimbazi, jijini Dar.
STAA Jacqueline Wolper Massawe, ambaye ni muigizaji mahiri wa filamu, amewapiku nyota wenzake wa tasnia hiyo baada ya kufanya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa Jumamosi iliyopita kwa namna tofauti kabisa, kwani badala ya kuita marafiki kwenye pati kubwa inayoambatana na vyakula na vinywaji, yeye alikwenda kuwatembelea wazee wanaolelewa katika Kanisa Katoliki la Msimbazi, jijini Dar.
Katika kituo hicho kinachowalea wazee wa kike na kiume, Wolper aliyeambatana na rafiki yake Kajala Masanja na wale aliowatambulisha kama Wolper Family, muigizaji huyo alitoa zawadi ya mchele mifuko miwili ya kilo 50 kila moja, sukari mifuko miwili ya kilo 50, sembe kilo 50 pia, sambamba na mafuta ya kupikia madumu mawili, vitu ambavyo alikataa kutaja thamani yake.
“Siku hizi nimekuwa mtu mzima, nimeachana na mambo ya sherehe kwa sababu nimeona ninakuwa napoteza pesa kwa mambo yasiyo ya muhimu, ni jambo la heri kwangu kuwasaidia wazee kwani nawapenda na naamini hata wao wanatupa sapoti kubwa sana kwenye kazi zetu, japo kuna watu walitarajia waone nini kitafanyika kwenye siku yangu hii ya kuzaliwa kuhusu sherehe,”alisema Wolper.
Marafiki zake kutoka Wolper Family walisema ni wao ndiyo waliomshauri staa huyo kufanya kitu hicho ili kuwa tofauti na wenzake ambao kumbukumbu ya kuzaliwa kwao hufanywa kwa matumizi makubwa ya fedha yasiyo ya lazima.
Baada ya kukabidhi msaada wa vyakula hivyo, mmoja wa wazee hao Bibi Rachel Christopher, alimpa somo Wolper kuwa ni vema wakaishi vizuri na mashabiki wao na kuachana na mavazi ya ajabu kwani yanawashushia hadhi zao.
0 comments:
Post a Comment