Sunday, January 18, 2015
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira amesema
yeye ni waziri na ana haki zake, baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kumtaka aachie nyumba anayoishi ya Bodi ya Sukari kwa
kuwa haimuhusu kwa sasa.
Juzi,
PAC iliiagiza Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kumwandikia barua ya
kumtaka mwanasiasa huyo mkongwe aondoke kwenye nyumba ya bodi hiyo
iliyopo Masaki jijini hapa, aliyoishi tangu akiwa Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika na iwapo haitawezekana, aanze kulipia tozo ya pango.
Hata
hivyo jana, Wasira alisema kuwa hawezi kujibizana na PAC kwa kutumia
magazeti na mitandao kwamba kama kuna maagizo yoyote yametolewa, kipo
chombo kitakachoshughulikia.
“Mimi
ni waziri nina haki zangu, PAC haihusiki na mtu binafsi wala siyo ofisa
mahesabu. Kwa nini unaniuliza mimi, si uwaulize PAC?” alihoji Wasira.
Akijibu
maelezo hayo ya Wasira, mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema jana
kuwa kamati yake haina nia ya kumshambulia waziri huyo kwa kuwa ana haki
ya kupewa nyumba na Serikali.
Alisema
iwapo Serikali bado inataka waziri huyo aendelee kukaa kwenye nyumba
hiyo, ilipe kodi na kama ikishindwa wampe nyumba nyingine.
“Hapa
suala siyo mzee Wasira binafsi, ni Serikali kukaa kwenye nyumba ya umma
isiyolipia kodi,” alisema Zitto. Aliongeza kuwa Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndiyo iliyobaini kuwa nyumba
hiyo hailipiwi kodi na kuitaka irejeshwe kwa Bodi ya Sukari.
0 comments:
Post a Comment