MIILI ya wasichana wawili, Bhoke Mwita Gisiri (16) na Matinde Kimoto Wambura (16) waliogongwa na gari na kufa papo hapo, imetekelezwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ikidaiwa ndugu hawawezi kuichukua kwa kuwa wasichana hao walikeketwa.
Kutokana na hali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Sweetbert Njewike amewataka ndugu kujitokeza kuichukua miili ya wapendwa wao, huku akiitaka jamii ya Wakurya ibadilike na kuachana na mila potofu zilizopitwa na wakati.
Inaelezwa kuwa, kwa mujibu wa mila za wakati huo za Wakurya, binti aliyekeketwa akifariki dunia hutupwa kichakani. Hali hiyo inaonekana bado ipo licha ya elimu kutolewa kwa jamii ya Wakurya kwamba mila za aina hiyo hazina nafasi katika dunia ya sasa.
Akizungumza jana, Kamanda Njewike alisema wasichana hao waliokuwa wamefanyiwa tohara walikufa Januari 3 mwaka huu baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 388 AGV katika Kijiji cha Msege, Kata ya Nyarukoba, Tarafa ya Ingwe wilayani hapa.
Dereva wake alikimbia na anaendelea kusakwa. Alisema miili bado imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu.
0 comments:
Post a Comment