SIMBA itanufaika na mauzo ya mshambuliaji wake nyota wa zamani, Mbwana Samata endapo atauzwa na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imefahamika.
Kwa sasa, Samata ambaye anaichezea TP Mazembe pamoja na Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu, yuko majaribio katika klabu ya PFC CSKA ya Moscow ya Urusi.
Akizungumza jana na gazeti hili, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema kwamba katika mkataba wa mauziano wa klabu hiyo ya Msimbazi na klabu hiyo ya Lubumbashi, walikubaliana kuwa endapo Samata atauzwa kwa klabu yoyote ile, Simba itanufaika kwa kupewa asilimia 30 ya bei ya kumnunua mshambuliaji huyo.
“Katika mkataba wa mauziano wa Samata na Simba kwenda TP Mazembe ambao uko CAF (Shirikisho la Soka Afrika) na pia Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa), ni kwamba popote atakapouzwa Samata, Simba itapewa asilimia 30 ya fedha za mauzo hayo,” alisema Rage akiwa Dar es Salaam.
Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), aliongeza: “Na hii ni mara pili kwa mujibu wa mkataba, yaani kama akiuzwa kwa Real Madrid na kisha baadaye kwenda Manchester United, Simba itafaidika na mauzo hayo.”
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Simba alisema kwa msingi huo, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba hawana budi kumwombea dua njema Samata ili afuzu majaribio yake ili klabu hiyo inufaike na mauzo hayo.
Samata aliuzwa kwenda TP Mazembe yenye makao makuu yake katika Jiji la Lubumbashi, DRC, Juni 2011 kwa gharama ya Dola za Marekani 100,000 (wakati huo Sh milioni 150), na amekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu hiyo maarufu barani Afrika inayomilikiwa na bilionea Moise Katumbi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika tovuti ya klabu hiyo ya Moscow, Samata yuko huko kwa maja ribio, lakini ameshindwa kucheza mechi mbili za kirafiki nchini Hispania kutokana na kuumia kifundo cha mguu.
Mechi hizo zilitarajiwa kufanyika jana na nyingine leo kujiandaa na nusu ya pili ya msimu wa 2014/15 nchini Urusi ambayo kwa sasa ligi zimesimama kupisha majira ya baridi.
Jana, PFC CSKA ilicheza dhidi ya Sion ya Uswisi, na ilitarajiwa kuwakosa wachezaji wake George Shennikov ambaye hajisikii vizuri, Georgi Milanov anayeugulia paja na Svetoslav St George na Dmitri Efremov walioumia mazoezini juzi.
Taarifa ya klabu hiyo ilieleza kuwa pia juzi katika uchunguzi wa kitabibu, iligundulika kuwa Samata ameumia kifundo cha mguu hivyo asingeweza kucheza mechi hizo za kirafiki.
Mechi hizo zinafanyika kwenye Uwanja wa Pinatar Arena, na leo wanatarajiwa kukabiliana na FSV Frankfurt ya Ujerumani. Katika mechi ya jana, waliishinda bao 1-0.
Timu ya PFC CSKA ni ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Urusi ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 17. Timu inayoongoza ligi hiyo ni Zenit St Petersburg yenye pointi 41 kwa mechi hizo 17.
HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment