Na Mwandishi wetu
Organizesheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBO) imeliomba Baraza la Sanaa nchini (Basata) kutengua adhabu ya miaka miwili ya kuyafungia mashindano ya urembo ya Miss Tanzania ili kuokoa kupotea kwa sura ya nchi katika mashindano ya dunia (Miss World).
Rais wa TPBO, Yasin “Ustadh” Abdallah amesema jana kuwa adhabu ya miaka miwili ni kubwa sana kulinganisha na makosa yaliyoainishwa na Basata mpaka kufikia hatua ya kuyafungia mashindano hayo ambayo ni mashindano makubwa kwa wanawake nchini tena yenye kuleta ajira na sifa kwa nchi.
Abdallah alisema kuwa Basata ilipaswa kuangalia athari zitokanazo na hatua hiyo na kuweka utaifa mbele kuliko kuififisha tasnia ya urembo nchini chini ya uratibu wa Hashim Lundenga. Alisema kuwa hakuna mbadala wa Lino katika kuandaa mashindano hayo na kuifanya Tanzania iendelee kujitangaza kimataifa.
“Mashindano ya urembo makubwa kama Miss Tanzania yameleta faida kubwa sana hapa nchini, mastaa kibao wa nchi kama Jokate Mwegelo, Wema Sepetu, Hoyce Temu, Happiness (Millen Magese), Brigitte Alfred, Jacqueline Ntuyabaliwe, Irene Owoya, Anti Ezekiel, Miriam Odemba, Richa Adhia, Nancy Sumari na wengine kibao wanaotamba hapa nchini wametokana na mashindano hayo,” alisema Abdallah.
“Karibu warembo wote hapo juu wameifaidisha nchi kwa kuitangaza, mfano Jokate atatoa ajira 500 baada ya kusaini mkataba wa mabilioni na kampuni ya Kichina, Wema anatoa ajira kwa kupitia filamu, Uwoya, Anti Richa wote hao wapo katika filamu na kutoa ajira,” alisema.
Alifafanua pia warembo kama Brigitte ameweza kujenga bweni la Maalbino huko Shinyanga kupitia urembo, Hoyce Temu anasaidia jamii na amekuwa maarifu kupitia mashinadno hayo na Millen ambaye ni mwanamitindo maarufu Afrika na Marekani.
“Hii ndiyo kazi ya Sanaa, kwenye ngumi, ukifungia promota mmoja, wengine watafanya, kwenye urembo ni tofauti, nani atafanya baada ya Lundenga? Adhabu ni kubwa na ninaomba Wizara husika kuangalia upya, kwani baada ya kumfungia, wangeweza kumweka katika uangalizi kwani kosa hili ni la kwanza kwa miaka 21 tokea aanze kuandaa,” alisema.
Alisema kuwa Tanzania itapotea kabisa katika tasnia ya urembo duniani na sifa walizoleta akiba Nancy (Aliposhinda taji la Miss World Africa mwaka 2005) na Brigitte alipotwaa taji la urembo wenye malengo maalum (Beauty with Pirpose) zitatoweka katika ramani ya mashindano hayo.
Alifafanua kuwa ngalau Miss Tanzania imethubutu kufanya vizuri katika mashindano ya dunia kuliko michezo mengine kwani ahat wao katika ngumi wameshindwa kushawishi wanawake kushiriki ipasavyo tofauti na akina Lundenga.
“Kila mwaka warembo 30 wanashindana, ukichukua kuanzia vitongoji, wilaya, mikoa, kanda ni mamia ya warembo wanapata fursa hiyo na wengine ‘kutoka’ kimaisha, leo hawa tutwapoteza, mawakala na wadhamini nao watapokea, hasara itakuwa ya nani, kwani Lino anaweza kufanya kazi nyingine na akapata kipato chake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment