Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kwamba makao makuu ya wilaya mpya ya Songwe yatakuwa Mkwajuni. “Nimekubali maombi haya kwa sababu yatapunguza gharama za uendeshaji, na kama itashindikana kupata wilaya mpya basi itabidi tuwape Halmashauri ya Songwe,” alisema.
Mkoa wa Mbeya una wilaya nane ambazo zimegawanyika katika tarafa 27, kata 262, vijiji 842 na mitaa 252. Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 2,707,410.
Akizungumzia kuhusu mpango wa maji katika wilaya hiyo, Waziri Mkuu alisema bado kuna changamoto kubwa ya kufikisha maji vijijini ambako upatikanaji wake uko kwenye asilimia 46. “Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa vitatu na mwakani tuna mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11, tunachohitaji ni fedha na usimamizi,” alisema.
Alivitaja vijiji viyakavyopata visima hivyo ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala, Isangawana, Galula, Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile, Bitimanyanga na Mapogoro.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezindua maabara tatu katika shule ya sekondari ya Saza ambazo zimejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya, Bi. Sophia Kumbuli alisema ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu sh. Milioni 268.5 vikijumuisha pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi.
“Kati ya hizo sh. Milioni 23.5 ni za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali na sh. Milioni 245 ni ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji na gesi,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI – Mbimba.
0 comments:
Post a Comment