Saturday, March 28, 2015

Stori: Elvan Stambuli
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Zuberi Kabwe ambaye ametangaza rasmi kuwania ubunge katika majimbo mengine, amelaumiwa na waliokuwa wapigakura wake waliodai amewaacha kwenye mataa, Uwazi Mizengwe limedokezwa.

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Zuberi Kabwe.
Zitto ametangaza kwamba atagombea ubunge kwa tiketi ya chama cha ACT- Tanzania katika majimbo yafuatayo ambayo majina ya wabunge na vyama vyao yamewekwa kwenye mabano; Kahama (James Lembeli, CCM), Kawe (Halima Mdee, Chadema), Segerea (Dk. Makongoro Mahanga, CCM) na Kasulu (Moses Machali, NCCR).

Kwa mujibu wa Zitto, majimbo hayo na mengine manne ambayo hajayataja anaweza kugombea na akapata kura nyingi na kushinda na ndiyo maana alipokuwa akiliaga bunge wiki iliyopita, aliwaambia wabunge kuwa watakutana tena ukumbini humo Novemba, mwaka huu.
Novemba uchaguzi mkuu utakuwa umekwishafanyika na ni wakati ambao wabunge watatakiwa kwenda kuapishwa bungeni.Baadhi ya wapigakura wa Kigoma Kaskazini waliozungumza na gazeti hili, walisema kwamba Zitto amewaacha kwenye mataa kwa sababu kama kweli amefanya vema katika jimbo lake litakuwa ni jambo la ajabu kulihama na kwenda kuongoza kwingine.
"Ukweli ni kwamba ametushangaza. Zitto amekimbia jimbo lake la Kigoma Kaskazini kwa nini? Hajatoa sababu ya msingi, kulikoni?" alihoji Ally Said Ally aliyejitambulisha kwa simu ya kiganjani kama mpigakura wake wa Kigoma.

0 comments:

Post a Comment