Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema iwapo
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea urais kupitia
chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza mali zake.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza kwenye Viwanja vya
Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia mtu anayetaka kujiunga ACT -
Wazalendo ikiwa atafuata taratibu zilizowekwa na chama hicho.
“Naomba niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama cha kumtengenezea
mtu mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa anataka kugombea
urais kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza wapi amezipata
kama taratibu za chama zinavyosema,” alisema Zitto na kuongeza:
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa ambaye anatajwa kuwania urais
kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT iwapo watakatwa majina yao
katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT - Wazalendo imepewa fedha na Lowassa
ambazo inatumia katika mikutano hiyo kumwandalia nafasi ya kuwania
urais, madai ambayo pande zote zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano huo, Zitto alisema chama
chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na kitampokea yeyote atakayefuata
taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alitangaza mali na madeni yake,
alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga na chama hicho itambidi atangaze
mali zake na kueleza jinsi alivyozipata, kama yeye (Zitto) alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto, msemaji wa Lowassa,
Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho na hakitakuwapo,
hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa) amekuwa akitumikia CCM
maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na anaendelea kutumikia
kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano wa chama hicho walipewa
adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kwa
kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya chama.
Mbali
ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba.
Licha ya muda wa adhabu hiyo kufikia tamati tangu Februari mwaka huu,
chama hicho kilisema kinaendelea kuchunguza mienendo yao na hakijaeleza
hatma yao.
Juzi,ililipotiwa kuwapo kwa mkakati wa chama hicho kukata majina ya
baadhi ya wagombea wanaoaminika kuwa na makundi yanayokihatarisha,
wakilengwa Lowassa na Membe ili kipitishe mgombea asiyekuwa na kundi.

0 comments:
Post a Comment