Dar/Mashirika. Hali bado si shwari Burundi. Vituo vitano vya
redio ikiwamo ya Taifa na ile ya African Public Radio (RPA) kilichokuwa
kimefungwa na Serikali ya Burundi vilishambuliwa jana huku kukiwa kukiwa
hakuna taarifa za uhakika za nani anayeitawala nchi hiyo kwa sasa.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Meja
Jenerali Godefroid Niyombare kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunziza
wakati akiwa Tanzania katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa
kikatiba wa Burundi.
RPA ilipigwa kombora la roketi ikielezwa kuwa askari wanaomtii Rais Nkurunziza ndiyo waliotekeleza shambulizi hilo.
Kituo hicho cha RPA kilifungwa na Serikali baada
ya kuanza harakati za kumpinga Nkurunziza lakini kilianza kurusha
matangazo yake juzi na usiku wa kuamkia jana kikapigwa kombora hilo.
Mbali na kituo hicho, vituo vya redio vilivyolipuliwa vinaelezwa kufanya harakati za kuipinga Serikali.
Vituo hivyo vilishambuliwa usiku wa kuamkia jana
muda mfupi baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha redio na televisheni
ya Rema, vinavyohusishwa na chama tawala.
“Tunalaani mashambulizi kwa vyombo vya habari
inatakiwa waandishi waachwe wafanye kazi zao,” alisema Mwenyekiti wa
Umoja wa Waandishi wa Habari Burundi, Alexandre Niyungeko.
Alisema hakufahamu hasa ni nani aliyeshambulia
vituo hivyo na kwamba yamefanyika wakati jeshi liliahidi ulinzi katika
maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, taarifa zilizochapishwa na Gazeti la
Jeune Afrique zilisema vituo vya redio vilivyolipuliwa ni vitano, viwili
vikilipuliwa na polisi, kimoja na waasi wanaomuunga mkono Jenerali
Niyomare na viwili vikichomwa na waandamaji.
Nkurunziza atuma ujumbe
Rais Nkurunziza alituma ujumbe kwenye mtandao wa
Twitter akiwataka wananchi wake kutulia kwa kuwa jeshi limezima
majaribio yote ya mapinduzi.
Hata hivyo, Rais Nkurunziza ameendelea kubaki Dar
es Salaam hasa baada ya kutangazwa kufungwa kwa mipaka ukiwamo Uwanja wa
Ndege wa Bujumbura.
Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Burundi, Leontine
Nzeyimana alithibitisha kuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza yupo
Tanzania.
Nzeyimana aliyasema hayo jana akiwa katika Hoteli
ya Serena ambako wakuu wa nchi za Afrika Mashariki walikutana kwa ajili
ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi.
“Bado yupo, lakini baadaye anaweza kuondoka,” alisema kwa kifupi waziri huyo bila kubainisha eneo alipo Rais huyo.
Baadaye Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Laurent
Kavakure alisema jijini Dar es Salaam kwamba Rais Nkurunziza
alitarajiwa kuondoka jana kurudi nyumbani na Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, Salvatory Rweyemamu alisema jana kwamba kiongozi huyo
alishaondoka nchini.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa
vikiwamo vya Burundi, vimekuwa vikihoji aliko Rais Nkurunziza ambaye
alielezwa kuondoka baada ya mkutano wa usuluhishi juzi na kurejea Dar es
Salaam baada kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Juzi, Meja Jenerali Niyombare alitangaza kuwa jeshi limemtimua Nkurunziza na kuunda Serikali ya mpito kuongoza nchi hiyo.
Mara baada ya taarifa hiyo, Nkurunziza hakuweza
kuhudhuria mkutano Ikulu na baadaye ilielezwa kuwa anaondoka kurudi
Burundi. Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa alilazimika kurejea
nchini kutokana na sababu za kiusalama.
Alipoulizwa jana, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Tanzania, Bernard Membe alisema hajui alipo kiongozi huyo
akisema hataki kuzungumzia suala la alipo kiongozi huyo na kwamba
viongozi wa Afrika Mashariki watakutana tena Jumatatu ya wiki ijayo
kujadili hali halisi ya Burundi.
Mapigano makali Bujumbura
Kumekuwa na mapigano makali ya kurushiana risasi
Bujumbura kati ya majeshi na vikundi vinavyopingana nalo na wanajeshi
takriban watano wameelezwa kuuawa.
Mwandishi wa BBC, Maud Jullien alisema mapigano hayo yalikuwa yanalenga kuiteka Televisheni ya Taifa.
Wakazi wa Burundi wameamka huku wakiwa na sintofahamu kuhusu nini kinaendelea baada ya kuelezwa kuwepo kwa mapinduzi.
Usiku wa manane, Mnadhimu Mkuu wa Majeshi, Prime Niyongabo,
alitangaza kwenye Redio ya Taifa kuwa mapinduzi yaliyotangazwa na Meja
Jenerali Niyombare yameshindwa.
Hata hivyo, kambi ya Niyombare ilisisitiza kuwa
mapinduzi yamefanyika na wanaendelea kushikilia mamlaka za Serikali
ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Majeshi yagawanyika
Mara baada ya matangazo ya mapinduzi juzi,
viongozi wa Jeshi linalomtii Rais Nkurunziza walitangaza kupitia Redio
ya Taifa kuwa hali iko shwari lakini mmoja wa wapinzani wa Nkurunziza
aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), kwamba majeshi ya
Serikali yanajaribu kupotosha.
Katika gazeti la Jeune Afrique imeripotiwa kwamba
pande zinazopingana nchini Burundi juzi usiku zilisema; “Tumekubaliana
kwamba usiwepo umwagaji damu ya Warundi. Sote tumeafikiana kuwa kisiwepo
kipindi cha tatu – itabaki namna ya kuangalia utaratibu wa kufikia
hayo.”
Wasomi wainyooshea kidole EAC
Akizungumzia hali ya machafuko hayo, Wakili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Abdallah Safari alisema iwapo wananchi
hawamtaki Nkurunziza hana budi kujitoa katika uongozi kama katiba
inavyosema.
“Kisheria, haki si lazima itendeke, lakini ni
lazima ionekane ikitendeka. Watu kama wanamtaka wasingeandamana, hali
ingekuwa shwari,” alisema Profesa Safari.
Alionyesha wasiwasi wake kuhusu uamuzi uliotolewa
na viongozi wa Afrika Mashariki na kusema wengi wanafanana na Nkurunziza
na ni vigumu kuwa upande wa wananchi.
Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Ushauri wa
Kitaalamu wa Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, Dk Kitojo Wetengere
alisema mgogoro wa Burundi ni wa kujitakia kwa sababu Nkurunziza
amekaidi katiba na makubaliano ya Arusha.
Alisema hata kama ana hoja zinazomwezesha
kuendelea kuongoza lakini angepima joto la wananchi kuangalia hali
ikoje... “Lakini katika hili, EAC ina nafasi kubwa ya kuumaliza mgogoro
huu kwa sababu Burundi ni majirani zetu na pia Tanzania inaathirika kwa
kupokea wakimbizi wengi.”
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga
Baregu alisema mgogoro wa Burundi umeonyesha umuhimu wa nguvu ya umma
kwani jeshi lisingeweza kuipindua Serikali iwapo wananchi
wasingeandamana... “Ujumbe ni kwamba, wananchi wakiamua jambo hakuna
anayeweza kupinda kwa sababu hata hao wanajeshi wasingeweza kuchukua
uamuzi huo bila wananchi.”
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Peter Elias, Florence Majani
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Peter Elias, Florence Majani

0 comments:
Post a Comment