Posted by Williammalecela.com on Tuesday, May 12, 2015
Magufuli: Nagombea urais
WAZIRI
wa Ujenzi, John Magufuli, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania
Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Raia Mwema linafahamu.
Gazeti hili limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kutoka ndani na nje
ya nchi kwamba Mbunge huyo wa Chato tayari amewaambia rafiki zake wa
karibu kuhusu hilo ingawa hataki suala hilo lisababishe “aache kuchapa
kazi” ndani ya serikali na chama.
Uthibitisho wa wazi kuhusu hatua hii ya Magufuli ulikuwa wakati wa msiba
wa mtoto mkubwa wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, Fidel,
uliotokea Januari mwaka huu, ambapo waziri huyo anadaiwa kumuarifu
kiongozi huyo wa chama cha Cord kuhusu suala hilo.
Vyanzo vya Raia Mwema vimeeleza kwamba Raila na Magufuli ni marafiki
wakubwa na ndiyo maana Mtanzania huyo aliamua kutumia nafasi hiyo
kumueleza mwenzake yaliyo ya moyoni.
“Utakumbuka alipofariki baba mzazi wa Magufuli, Raila alikuja msibani.
Hawa ni marafiki wa muda mrefu. Sasa kule kwenye msiba mheshimiwa
aliamua kumueleza mwenzake. Hili mimi nalifahamu,” kilieleza chanzo
hicho cha gazeti hili.
Jina la Magufuli limekuwa likitajwatajwa kama miongoni mwa majina ya
watu wanaofaa kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu, ingawa amekuwa hana spidi kwenye suala hilo kama walivyo
baadhi ya wanasiasa wengine ndani ya CCM.
Wiki mbili zilizopita, Raia Mwema lilibashiri kwamba Magufuli ni mmoja
wa wanasiasa ambao wanaweza kupitishwa na CCM kumrithi Kikwete kutokana
na sifa yake ya uadilifu na uchapakazi.
Wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 38 ya CCM yaliyofanyika
mjini Songea, Ruvuma, mwanzoni mwa mwezi huu, Kikwete alisema wapo
viongozi wazuri ndani ya chama hicho wenye sifa lakini hawataki nafasi
hiyo na wanatakiwa kushawishiwa.
Kauli hiyo ilitafsiriwa na wengi kama kuwaandaa wana CCM na jina la
mgombea ambaye hatajwitajwi kwa sasa; huku majina ya Augustino
Ramadhani, Dk. Augustine Mahiga na Magufuli yakitajwa.
Katika mazungumzo na mmoja wa wasaidizi wa Kikwete wiki mbili
zilizopita, Raia Mwema liliambiwa kwamba kuna mambo makubwa matatu
ambayo yamewafanya baadhi yao kudhani Kikwete alikuwa akimzungumzia
Magufuli kwenye hotuba yake ya Songea.
Mosi, ni ukweli kwamba katika ziara ambazo Kikwete amekuwa akifanya
ndani ya nchi, Magufuli amekuwa akionekana kama waziri anayeonekana
kuheshimiwa na Watanzania.
“Mfano ambao Kikwete amewahi kuusema kwetu unahusu mkutano mmoja wa hadhara uliofanyika Mwanza
mwaka jana. Watu wa kule walikuwa wakizomea na kuonyesha alama za Chadema.
"Lakini alipopanda jukwaani Magufuli mkutano wote ulitulia. Mpaka
Kikwete alipopanda jukwaani, mkutano ulikuwa umetulia. Nadhani Kikwete
ameona kwamba labda huyu ndiye mwana CCM ambaye Watanzania wanamuamini,"
alisema.
Wakati aliporejea kutoka kwenye matibabu nchini Marekani mwishoni mwa
mwaka jana, Kikwete alitamka hadharani kwamba alitaka kutangaza mapema
kuhusu ugonjwa wa kansa uliokuwa ukimsumbua, lakini ni Magufuli
aliyemkataza kufanya hivyo wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri.
Mwaka juzi, Magufuli pia aliwashangaza watu wakati alipopishana
hadharani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu suala la magari ya
mizigo kupita katika barabara yakiwa yamezidi mizigo.
"Ile ilikuwa ni ishara kwamba Magufuli alikuwa akiamini nguvu iliyo juu
ya Pinda. Katika hali ya kawaida, si rahisi kwa waziri wa kawaida
kutofautiana na Waziri Mkuu hadharani," kilisema chanzo kingine cha
gazeti hili.
Msaidizi huyo wa Kikwete alilieleza pia Raia Mwema kwamba katika mojawapo ya misiba ya karibuni zaidi
iliyoikumba familia ya Rais, Magufuli alikuwa waziri pekee ambaye alilala msibani kijijini Msata.
"Kama walivyo wenzake, Magufuli anaonekana ni mchapa kazi na mtu ambaye
hahusishwi na masuala ya ufisadi ingawa kuna wanaonong'ona kuhusu suala
la uuzaji wa nyumba za serikali," Raia Mwema liliambiwa.
Katika kuchagiza hilo, jarida la The Indian Ocean linalochapwa na
taasisi inayoheshimika barani Afrika ya Africa Intelligence, katika
toleo lake la Februari 13, 2014, limemtaja Magufuli kama kipenzi cha
Kikwete na mtu ambaye anaweza kumuunga mkono.
Jarida hilo ambalo hufanya uchambuzi wa masuala mbalimbali ya nchi
zilizo katika mwambao wa bahari ya Hindi barani Afrika, limefanya
uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM haswa
baada ya kashfa ya akaunti ya Escrow.
Wiki ijayo, tutachapa ripoti kamili ya jarida hilo kwenye gazeti hili
Chanzo: Raia Mwema
0 comments:
Post a Comment