Posted by Williammalecela.com on Friday, May 29, 2015
"Nafasi
ya Urais ni nafasi ya hadhi na heshima kubwa. Unapoiomba hupaswi kufanya
michezo ya kuigiza. Huu utaratibu wa kuratibu watu, kuwasafirisha,
kuwapa posho na ubwabwa waje kukuomba kugombea ni michezo ya kuigiza
ambayo ni aibu kubwa.
Kila mgombea ana uwezo wa kutengeneza watu wa kumuomba kugombea lakini
wengine hatufanyi hivi kwasababu tunaheshimu nafasi tunayoiomba na
tunaamini kwamba haipaswi kutafutwa kwa ulaghai na maigizo.
Ni aibu sana kutumia shida na njaa za watu kisiasa. Ni aibu sana
kukusanya vijana na wazee wa watu na kuwapangia viti na mahema na kuwapa
pesa halafu pesa na kuwapiga picha. Ukiona mtu anatafuta nafasi ya
uongozi kwa ujanja na ulaghai ujue atatawala kwa ujanja na ulaghai.
Viongozi wanaokubalika na watu hawahangaiki kupanga Viti na mahema na
kuwapiga picha watu wanaowakubali. Mgombea anayehaha na kutumia pesa
nyingi kuonyesha anakubalika ukweli ni kwamba hajiamini. Kama
unakubalika huwezi kuratibu makundi na kuyalipa na kuwapiga picha na
kuita waandishi wa habari waje kushuhudia. Hizo ni mbinu za mfa maji.
Naamini Chama changu hakitatishwa na nguvu za maigizo. Tunataka uongozi
safi unaomuogopa mungu. Tunataka uongozi wenye uadilifu na fikra mpya za
kuisogeza mbele Tanzania. Tunataka viongozi watakaomaliza shida za
Watanzania sio wanaozitumia shida hizo kisiasa
Hata Mzee Makamba, pamoja na umri wake wa miaka 75, leo akiwa na pesa za
kumwaga anaweza kutengeneza makundi yakamuombe kugombea Urais.
Ifike mahali katika nchi yetu tuache hii michezo. Tukiendelea na mambo
haya, tunatengeneza taifa linaloendeshwa kwa propaganda tu. Watu
wanaotaka kuomba nafasi ya Urais wanapaswa kuwa na ujasiri na wanapaswa
kujiamini na kusema wanataka nafasi hiyo na wana fikra gani mpya bila
kutumia pesa kuonyesha kwamba wanagombea kwasababu wanahitajika na watu.
Uongozi thabiti na shupavu hautokani na michezo ya kuigiza."
January Makamba

0 comments:
Post a Comment