Posted by Williammalecela.com on Wednesday, July 08, 2015

 |
TAMKO LA KULAANI KAULI YA MKUU WA MKOA WA MWANZA BWANA STANSLAUS MAGESSA MULONGO
Ndugu wanahabari,
Kwanza nikushukuruni kwa kuitikia wito wangu na kukubali kuja kuungana
nami ili kupitia ninyi Watanzania wajue hasa wale Watanzania wenzangu
wanaotokea Mkoa wa Mwanza.
Siku ya jana binafsi
nilishtushwa mno na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza eti
akitoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi kuzuia watu kwenda Dodoma. Ni
imani yangu kuwa si mimi peke yangu bali Watanzania wengi watakuwa
wameshangazwa na kauli ya Magessa. Ambayo kimsingi ni kuvunja Katiba ya
nchi ambayo yeye amepa kuilinda na kuitetea na ni kauli ya ajabu sana
kutolewa na mtu mwenye nafasi nyeti kama yake.
Nafasi
aliyonayo ni kumwakilisha Raisi hapo Mwanza hivyo vile vile sitaki
kuamini kwamba amefikia hatua ya kutoa kauli ambazo Watanzania tutaishia
kujiuliza maswali mengi hasa tukitaka kujua ni nani hasa aliyemtuma
manake haiwezekani mtu aliyeaminiwa na Raisi kutoa kauli ya vitisho na
yenye kila maana ya kuvunja Katiba ya Nchi jambo ambalo naomba wenzangu
kusimama pamoja nami na kulaani kauli hiyo kwa namna yeyote inayofaa.
Hili ni Taifa letu sote hivyo asitokee mtu akadhani kwamba yeye ni zaidi
ya Watanzania wote ama yeye ni juu ya Katiba na Sheria za Nchi na
kujiamulia kututisha atakavyo.
Ndugu Wanahabari,
Katiba yetu ya mwaka 1977 katika Ibara yake ya 17(1) iko wazi kabisa nanukuu;
“Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika
Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi
na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka
katika Jamhuri ya Muungano.”
Hivyo ndivyo Katiba inavyotamka
kwamba kimsingi Mtanzania kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni
haki yake Kikatiba. Sasa leo ni lazma Magessa atueleze yeye ni kama nani
hata kuzuia Watanzania kutimiza haki yao hiyo ya Kikatiba. Na labda
kama ni mgeni lazma ajue Watanzania hasa wana CCM unapofikia wakati kama
huu wengi wao wanakuwa na shauku ya kwenda Dodoma si tu kwenda
kujumuika na wenzao katika kushuhudia moshi mweupe ukitoka katika Ofisi
za Makao Makuu ya CCM bali pia kufurahi na kujifunza namna chaguzi,
mapendekezo na hata namna ambavyo vikao vinaendeshwa ndani ya CCM.
Hili halijaanza leo na wala halitazamiwi kuisha leo ama kesho kwa
vitisho vya namna hiyo labda Katiba iseme vinginevyo. Kauli za namna hii
ni za kugawa Wananchi na vile vile ni za kuhatarisha Uhuru na Haki zetu
kama Watanzania ambazo Viongozi wetu wamekuwa wakizisimamia kwa umakini
mkubwa mno. Ni wazi kwamba kama kulikuwa na tatizo lolote Vyombo vyetu
vyenye dhamana ya kusimamia Ulinzi na Usalama vingeona hayo na basi wao
ndio wangekuwa na Jukumu la kutoa kauli za namna hiyo na hasa vyombo
vilivyoko Dodoma.
Ndugu Wanahabari,
Vitisho vya
namna hii na kauli za namna hii ni lazma vitawaweka Watanzania njia
panda na kuishia kujiuliza maswali bila majibu ya kwamba ni kwa nini
yote hayo. Na ni kwa nini kauli hiyo itolewe wakati huu. Lakini imekuwa
ajabu kweli kweli kwamba katika Mikoa 31 tuliyo nayo ametokea Mkuu wa
Mkoa mmoja tu aliyetoa kauli ya ajabu isiyo stahiki kabisa kutolewa na
mtu wa namna yake.
Bwana Magessa amekuwa na tabia zake
za peke yake tokea akiwa Arusha hivyo ni lazma sasa ngazi za kinidhamu
ambazo bwana Magessa anawajibika kwazo zione namna ya kushughulika naye
kabla hajaendelea kuwagawa Watanzania kwa kauli zisizo na staha. Haya
mambo hayavumiliki hata kidogo. Watanzania na hasa wana CCM waachwe
waende Dodoma manake kwanza kwa kufanya hivyo mji wa Dodoma nao utakuwa
na mengi ya kunufaika kupitia ugeni huo.
Lakini vile
vile mshikamano wa Watanzania unaendelea kukomaa na watu wanaendelea
kufahamiana. Binafsi sina shaka hata kidogo na vyombo vyetu vya Ulinzi
na Usalama na ndiyo maana wamekaa kimya kwa kuwa wamejipanga na wanajua
Watanzania si watu wa fujo ila wanapenda kushuhudia na kusimamia haki
zao za msingi. Na niseme tu kauli zingine hizi hupelekea kuchochea watu
manake hata wale ambao hawakuwa na nia ya kwenda Dodoma sasa wataenda
ili kushuhudia ni kwa nini wanazuiwa.
Ndugu Wanahabari,
Nalaani kauli hiyo kama Sylvester Yaredi na niendelee kuwaomba wale
wenye mapenzi mema na Taifa hili waungane nami katika kulaani kitendo
hicho na hasa baada ya kumwangalia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na
kutoridhishwa kabisa na kauli yake yenye nia ya kututisha pasi sababu ya
msingi; Dodoma tutakwenda ili kushuhudia Chama chetu kinavyoendesha
vikao vyake na si hivyo tu, bali tunakwenda vile vile ili tuweze kurudi
na Jina la Raisi atayepokea mikoba ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Nimalizie hivi aliwahi kusema Johann Wolfgang “The Coward only threatens when he is safe.”
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Imeandaliwa na;
Mtemi Sylvester Yaredi
(Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa Viti Vitano Bara – Mwanza)
|
0 comments:
Post a Comment