Hamida Hassan na Mayasa Mariwata
UKATILI wa mume! Mama mmoja, Neema Mwita aliyeripotiwa na gazeti hili kuwa aliunguzwa na uji wa moto na mumewe Juma Mwita, amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mama huyo baada ya kumwagiwa uji na kulazwa takriban mwaka mzima kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mara na kushindikana kupona, hivi karibuni aliletwa Muhimbili na Mtangazaji wa Kipindi cha Wanawake Live, Joyce Kiria ambapo amelazwa kwenye Wodi Namba 24, Jengo la Sewa Haji.
Akizungumza kwa tabu mama huyo alisema kuwa licha ya kupata kilema cha maisha, anamshukuru Joyce na gazeti hili na wote waliojitokeza kumsaidia kwani hatua aliyofikia sasa inaridhisha na atapona kwani amefanyiwa upasuaji baada ya kuondolewa nyama kwenye paja.
Neema alipatwa na janga hilo baada ya kuchuma mahindi shambani kitendo kilichomchukiza mumewe aliyeamua kumuunguza kwa uji uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya kusongea ugali.
“Naomba msaada kwani ndugu zangu hawana uwezo, licha ya kwamba Napata chakula cha hospitali kuna huduma nyingine zinahitaji fedha,” alisema mama huyo.
Kwa yeyote anayependa kumsaidia mama huyo awasiliane naye kwa namba ya simu 0656151072 au 0756768305, kutoa ni moyo.
0 comments:
Post a Comment