Wednesday, August 26, 2015

Default Masha adaiwa kutumia uwaziri kupita Ubunge

HATUA ya mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Nyamagana, Mwanza Lawrence Kego Masha kumwekea pingamizi mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai kuwa si raia imezua utata wa kisheria wa mawaziri kuendelea na nafasi zao hata baada ya Bunge la Muungano kuvunjwa.

Mbali na suala la kutokuwa na uraia, mgombea huyo wa CHADEMA, Ezekiah Dibogo Wenje anadaiwa pia kuwa hakuwasilisha kiapo cha kisheria kuthibitisha yale aliyojaza kwenye fomu kama inavyotakiwa pamoja na kushindwa kujaza fomu za kugombea kama inavyotakiwa.

Sababu nyingine zilizotolewa na Masha ni kuwa mgombea Wenje alidai kuwa ni mkazi wa Burola A wakati si kweli kwani hana makazi katika mtaa huo na kwamba mgombea huyo pia amesema uongo juu ya cheo chake katika Nation Media Group kuwa ni meneja wakati ni afisa masoko pamoja na kushindwa kujaza fomu ya kugombea kama inavyotakiwa.

Masha ni Waziri wa Mambo ya Ndani na hatua yake ya kudai kuwa Wenje si raia na kufuatiwa na malalamiko ya Wenje kuwa Masha anamtishia maisha pamoja na kutuma maafisa uhamiaji kwenda kwao Rorya kuchunguza uraia wake imezua hisia kwamba mgombea huyo wa CCM ametumia madaraka yake kufuatilia uraia wa mpinzani wake.

Wenje alisema kwamba Alhamisi iliyopita majira ya jioni alipokea simu ya Masha akimsihi kuondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho kwa madai kuwa sera za kampuni anayofanyia kazi haziruhusu wafanyakazi wake kujiingiza katika siasa. “Aliniuliza kama nazifahamu sera za kampuni ninayofanyia kazi kwani haziruhusu mtumishi kuingia katika siasa na hivyo kunitaka nifikirie kuondoa jina langu na kwamba angenisaidia kurudishwa kazini. Lakini mimi nilikataa na kumwambia siwezi kujitoa kugombea.

“Siku hiyo hiyo saa mbili usiku alinipigia tena simu na kunieleza kuwa atatumia rasilimali zake kuhakikisha ananiwekea pingamizi kwa kuwa mimi si raia. Na kweli maofisa sita wa Serikali walikwenda nyumbani kwetu Rorya na kumbugudhi mama yangu mzazi kwa madai kuwa wanakusanya vielelezo juu ya uraia wangu,” alisema Wenje akieleza kwamba alimwomba Masha aache kutumia vyombo vya dola kwa maslahi yake.

Lakini Masha alikiri kumpigia simu mgombea huyo wa CHADEMA lakini akakana kumtishia pamoja na kutuma maofisa uhamiaji kwenda kufuatilia uraia wake kijijini kwao Rorya na akasema kuwa alimpigia na kumshauri’ kwa nia njema’ kwani siasa si ugomvi.

“Ni kweli nilizungumza naye kwa simu lakini si kwa ugomvi wala kumtishia. Nilimweleza kuhusu sera za kampuni yao kutoruhusu watumishi wake kujihusisha na siasa na kama anazifahamu. Pia nilimwambia kuhusu udanganyifu katika fomu zake na kwamba nilikuwa natarajia kumwekea pingamizi na nitamshinda hivyo bora angeachia ngazi.

“Nilimshauri pia kama ndugu yangu maana siasa si ugomvi, kuwa ukiacha kuchukua fomu nitakuombea usifukuzwe kazi kulingana na sera za chombo chako kwani kitendo cha kujiingiza katika siasa atafukuzwa kazi. Na kweli niliweka pingamizi sasa huko ni kumtishia maisha?

“ Sijamtuma ofisa yoyote kwenda kwake na hili la uraia nimelipata kutoka kwa wapambe wake. Mimi ni mwanasheria siwezi kufanya hivyo,” alisema Masha. Ni kutokana na maelezo hayo ya Masha baadhi ya watu wanadai kuwa ni ngumu kutenganisha kitendo ya maofisa uhamiaji kwenda kufuatilia uraia huo wa Wenje baada ya Masha kumpigia simu kumwomba ajitoe na kwamba angemwekea pingamizi kwani si raia.

“Huyu ni Waziri wa Mambo ya Ndani mwenye dhamana ya mambo ya uraia hivyo kitendo cha yeye kuhoji uraia wa mtu na hapo hapo watu wanaenda kwao Wenje kufuatilia vielelezo vya uraia wake, moja kwa moja unaona kuwa kuna uhusiano fulani kwamba huenda ni maelekezo yake kwa idara ya uhamiaji. “Hapa kuna conflict of interest. Pia inapaswa ujiulize ni kwanini Masha ampigie simu kumwomba ajitoe wakati anajua atamwekea pingamizi.

“ Ni kwanini aseme angemwombea aendelee na kazi yake iwapo angejitoa. Ina maana Wenje alikuwa hajui sera za kampuni anayofanyia mpaka aambiwe na Masha. Au Masha alikuwa na uchungu gani kuona Wenje atakosa kazi mpaka amwombee asifukuzwe. Masha ana uhusiano au mamlaka gani kwa mwajiri wa Wenje mpaka aseme angemwombea asifukuzwe kazi. Huyu ni msomi wa chuo kikuu hawezi kuamua kugombea bila kujua sera za chombo chake,” anasema mkazi mmoja wa jijini Mwanza aliye karibu na sakata hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe .

Watu kadhaa waliozungumza na Raia Mwema wanasema kitendo cha mawaziri kuendelea na nafasi zao kunaleta mgongano wa maslahi kwani waziri anaweza kutumia nafasi yake kujifanyia kampeni. “Hata kama Masha hakuamuru Uhamiaji wafuatilie uraia wa Wenje, ni vigumu kutohusisha vitu hivi kwa sababu bado yuko ofisini hivyo anatumia mamlaka yake kwa maslahi yake binafsi. Ni vyema hili suala likatazamwa upya,” Ramadhani Juma anasema.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Nyamagana Wilson Kabwe alikubaliana na pingamizi la Masha na kusema kuwa Wenje ameshindwa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha kama ni raia pamoja na madai mengine yote sita yaliyotolewa kwenye pingamizi hivyo kumpitisha Masha kama mbunge mteule baada ya kukosa mpinzani.

Chanzo Raia Mwema Toleo la 148

0 comments:

Post a Comment