TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kitendo kilichofanywa na mgombea
urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa kuwataka waumini wa
madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye, kamwe hakikubaliki.
Imesisitiza
kuwa kitendo hicho, kinawagawa Watanzania na kuwapa mwelekeo wa
kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa Kifungu cha
2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015,
kinachosema “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa
kura kwa misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.” Onyo hilo la NEC
lilitolewa jana na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva ikiwa ni
muda mfupi tangu CCM ilipoitisha mkutano wa waandishi wa habari,
kuzungumzia suala hilo, huku ikiitaka NEC kuchukua hatua dhidi ya
ukiukwaji wa kanuni wa mgombea huyo wa Chadema.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, NEC imewakumbusha wagombea na vyama
kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo
walikubali kuyafuata kwa kutia saini Julai 27, mwaka huu. Ilisema
inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya
kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.
“Kitendo
kilichofanywa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Edward Lowassa kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya
Kilutheri kumchagua yeye hakikubaliki,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuzingatia Kifungu cha 2.1
(k) cha Maadili kinachoelekeza vyama au wagombea kutotumia majengo ya
Ibada kufanya kampeni, na pia vyama au wagombea kutowatumia viongozi wa
dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.
“Tunatumia
fursa hii tena kuwaasa viongozi wa madhehebu yote ya dini kutoruhusu
vyama au wagombea au wanachama wa vyama vya siasa kutumia nyumba za
Ibada kufanya kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.” Jaji
Lubuva alisema mbali ya hilo, Lowassa na viongozi wengine wa Chadema
wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na kwamba
Tume itasababisha machafuko, bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni
hatari.
“Kauli
hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za hatari sana kipindi
kama hiki, kwa sababu maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea, ambayo
wagombea wote na vyama vya siasa walipewa, yana maelekezo kuhusu
utaratibu mzima wa kupiga na kuhesabu kura katika ngazi ya kituo,
kujumlisha kura katika ngazi ya kata, jimbo na taifa.
Akifafanua
utaratibu ulivyo, Jaji Lubuva alisema taratibu zote hizo hushuhudiwa na
Mawakala wa Vyama vya Siasa na Wagombea, ambapo kura zikihesabiwa ngazi
ya Kituo, mawakala hupewa nakala ya matokeo katika fomu Na. 21A Kura za
Urais, 21B Kura za Mbunge na 21C Kura za Udiwani. Alisema katika ngazi
ya Jimbo, hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika nakala la
Fomu 21A za Urais na 21B za Mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa katika
fomu 24A kwa Rais na 24B Mbunge na Nakala ya matokeo wanapewa mawakala
wa vyama na wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya
jimbo.
Kwa upande
wa ngazi ya Taifa, alisema Tume hujumlisha matokeo ya kura za Rais mbele
ya wagombea na mawakala wa vyama na kutangaza matokeo. Aliongeza kuwa
katika hatua hizo, Chadema wanapaswa kueleza wizi unafanyika wapi? “Jana
Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema Taifa) naye amesema kuwa Tume
inaegemea Chama Tawala, hivyo itasababisha uvunjifu wa amani. Hili nalo
ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.
“Wakati
wote Tume haiegemei wala kupendelea chama chochote katika kazi zake.
Mbowe anajua hivyo, chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea kura halali
zote na ndiyo maana hata wabunge wa vyama vingine walitangazwa. Alisema
viongozi wote hasa wakuu wanaogombea Urais, yafaa wawe waangalifu
katika matamshi yao, vinginevyo matamshi ya aina hiyo yanaweza kujenga
msingi wa vurugu baadaye.
“Tume
ya Taifa ya Uchaguzi inakumbusha vyama vya siasa vijielekeze kwenye
kutumia muda mwingi kuelezea Sera za vyama vyao ili ziweze kupimwa na
wapiga kura, badala ya kuchochea uhasama kati yao na Serikali na Tume ya
Uchaguzi. Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, NEC haitasita kukifikisha chama au
mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake
;na anaposhindwa Kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa chama au mgombea
husika, ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa mhusika.
CCM
yaja juu Saa chache kabla ya tamko la NEC la kulaani kitendo cha
Lowassa kudaiwa kuomba kura kanisani, ikielezwa amewataka waumini wake
kusali ili kanisa la KKKT litoe rais wa nchi kwa mara ya kwanza, CCM
nayo ililaani kauli hiyo na kuitaka NEC kuchukua hatua.
CCM
kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye aliyezungumza jijini Dar es Salaam jana, ilisema inalaani
matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa kwa misingi ya udini, ukanda,
ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ili kutafuta madaraka.
Alisema:
“Katika hali ya kushangaza na kusikitisha tarehe 6/09/2015, Siku ya
Jumapili mjini Tabora, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Chadema, Edward Lowassa aliamua kutumia udini kuomba kura.
“Lowassa
akihudhuria ibada katika Kanisa la Kilutheri (KKKT) mjini Tabora
amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii
akidai kuwa kwa kuwa toka nchi ipate Uhuru hajawahi kutokea rais kutoka
dhehebu la Kilutheri, hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.”
Nape
alisema kauli hiyo ya Lowassa, licha ya kuwa ni kinyume na Sheria za
Uchaguzi, kinyume na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizosainiwa na
vyama vyote, lakini ni kinyume na mila na desturi za Kitanzania katika
kuhakikisha Taifa linabaki kuwa moja, lenye umoja, amani na mshikamano.
Akinukuu
mazuio yanayopinga kile kilichofanywa na Lowassa, Nape alisema;”Kwa
mfano Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015,
yaliyotolewa na Tangazo la Serikali Namba 294 la tarehe 27/7/2015 chini
ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 Ukurasa
wa 5 Kifungu 2.1 (k) kinasema;
“Viongozi
wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao wahakikishe kuwa majengo
wanayotumia kufanya kampeni si ya Ibada. Vile vile vyama vya siasa
vihakikishe kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya
vyama vya siasa au wagombea wao.”
Nape
alisema lakini katika maadili hayo hayo, ukurasa wa saba Kifungu cha
2.2 (i) kinasema; ”Vyama vya siasa au wagombea hawaruhusiwi kuomba
kupigiwa kura kwa misingi ya udini, ukabila, jinsia au rangi.”
Akizungumzia
kauli ya rais kutokana na Walutheri, Nape alisema matamshi hayo ni
uthibitisho tosha kuwa Lowassa, chama chake cha Chadema na vyama
vinavyomuunga mkono chini ya Ukawa ni wabaguzi, wachochezi na waroho wa
madaraka wasiojali masilahi mapana ya nchi na kwamba kwao madaraka ni
muhimu kuliko nchi.

0 comments:
Post a Comment