
MGOGORO wa vyama viwili vya siasa CUF na CHADEMA ambavyo vinaunda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), katika Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu,
juzi ulichukua sura mpya.
Hali hiyo inatokana na mgombea mmoja wa ubunge wa jimbo hilo kupitia
CUF, Martine Makondo na wafuasi wake, kuvamia uzinduzi wa kampeni za
mgombea ubunge wa CHADEMA, Martine Magire ambapo mgeni alikuwa Mama
Regina Lowassa (mke wa Edward Lowassa).
Mama Lowassa alishindwa kuzindua kampeni hizo kutokana na vurugu kubwa
zilizotokea. Awali mkutano ulikuwa ufanyike kwenye Uwanja wa Michezo
uliopo katika Sekondari ya Lagangabilili.
Dalili za vurugu zilianza kuonekana mapema baada ya wafuasi wa CHADEMA
kudai kuwa, mgombea wa CUF alikuwa amekwenda kwenye mkutano huo na kundi
la vijana ili kuvuruga mkutano.
Baada ya Mama Lowassa kuwasili eneo la mkutano akiwa na Naibu Katibu
Mkuu Baraza la Wanawake wa CHADEMA Taifa (BAWACHA),Kunti Yusuph, mgombea
wa CUF aliwasili eneo hilo akiwa amebebwa na wafuasi wake wakidai
mgombea wao amehujumiwa na mgombeawa CHADEMA na kusababisha jina lake
likatwe na Kamati Kuu.
Wafuasi wa CUF walimpandisha mgombea wao (Makondo), jukwaani ndipo
vikaanza kutokea vijembe kati yao na wafuasi wa CHADEMA wakiimba, kupiga
kelele za kuwataja wagombea wao.
Hali hiyo iliwashangaza viongozi wa CHADEMA na mgeni rasmi (Mama
Lowassa) kwa dakika 15 ndipo walinzi wa chama hicho wakamwondoa eneo
hilo wakihofia usalama wake katika mkutano huo.
Baada ya Mama Lowassa kuondolewa jukwaani, kupanda gari yake na kuondoka
eneo la mkutano, Yusuph alianza kuwatuliza wafuasi wa vyama hivyo bila
mafanikio akaamua kuwatuhumu wananchi, lakini wafuasi walimzomea
wakitaka Makondo arudishwe.
"Tatizo tunafanya siasa kwa ushabiki na matokeo yake ndiyo haya, mimi
sikuja kunadi mahindi kwenye mnada, nimekuja kumwombea kura mgombea
urais wa UKAWA (Edward Lowassa), ubunge na udiwani mtajuana wenyewe
Oktoba 25, mwaka huu," alisema.
Hata hivyo, Yusuph alishindwa kutuliza vurugu hizo na kulazimika
kuondoka eneo hilo chini ya ulinzi wa vijana wa CHADEMA na kuwaacha
viongozi wa mkoa, wilaya waendelee na mkutano lakini hata baada ya
kuondoka, mkutano huo haukuendelea.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gemin Mushy, alisema askari wake
walitumia busara kutomtoa mgombea wa CUF kutokana na mazingira
kutokuruhusu kumkamata.
Chanzo cha mgogoro huo ni Makondo ambaye awali alikuwa CHADEMA, kutimkia
CUF baada ya jina lake kukatwa ingawa alishinda kwenye kura za maoni na
aliyeshinda nafasi ya pili Magire kupewa nafasi hiyo.
0 comments:
Post a Comment