Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo amemuandikia barua mheshimiwa James Mbatia.
Mtunzi huyo mahiri wa riwaya nchini Tanzania ameandika barua mwenyekiti mwenza huyo wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) kujadili masuala mbali ya kisiasa kuhusiana na
mwanasiasa huyo.Shigongo aliandika barua kupitia ukurasa wake wa
Facebook, inayosomeka kama ifuatavyo;
Salaam
ndugu yangu, Mara ya mwisho tulipoonana ilikuwa ni usiku pale Hospitali
ya Aga-Khan ukiwa mgonjwa, tumaini langu ni kwamba unaendelea vizuri
hasa kwa sababu ninakushuhudia mara kwa mara katika harakati
unazoziendesha chini ya Ukawa. Nimeamua kukuandikia barua hii kwanza
kabisa si kwa lengo la kukushambulia, siwezi kufanya hivyo hata siku
moja.
Nimewahi
kukiri kwa mdomo wangu na maandishi kuwa miongoni mwa watu
ninaowaheshimu sana katika nchi yangu ni James Mbatia, jambo hili kama
hulijui basi naomba ulitambue tangu leo. Siwezi kukushambulia kwa sababu
wewe ni raia mwenzangu wa Tanzania, siwezi kukushambulia kwa sababu
siku zote nimeamini Mbatia ni mzalendo, mtu ambaye kila anapozungumza
huwa naona mawazo yake na yangu kuhusu nchi hii ni kama yanafanana. Mara
zote nimekusikia ukiongea vizuri juu ya taifa letu Tanzania bila kujali
tofauti za kiitikadi, dini wala kabila.
Ninachokifanya
hapa leo ni kukumbushana, hivyo ndivyo tulivyoagizwa kwamba unapomwona
mwenzako anapotea, mkumbushe, badala ya kumwacha aendelee kuelekea
shimoni. Hivyo naomba univumilie sana, ili niongee yaliyomo moyoni
mwangu, mwisho wa siku si lazima uyachukue au uyatilie maanani,
unaruhusiwa kabisa kuyapuuza.
Mwandishi
na mzungumzaji maarufu duniani, Dk. Steve Maraboli aliwahi kusema
maneno yafuatayo na ninaomba nimnukuu; Sisi sote hufanya makosa, sisi
sote tunapambana na jambo fulani, sisi sote hupata majuto sababu ya
mambo tuliyofanya zamani. Lakini pamoja na hayo hatutakiwi kuyaishi
makosa yetu, kuyaishi mapambano yetu, kuyaishi majuto yetu, bali tuelewe
tuko hapa leo, yaani hii ni leo tuna uwezo wa kuibadilisha leo na
hatimaye kuibadilisha kesho!
Maneno
haya ya Maraboli ndugu yangu Mbatia yanathibitisha kabisa kwamba hakuna
mwanadamu asiyekosea, ukishaitwa jina hilo tu (mwanadamu!) lazima huwa
unafanya makosa, lazima huwa una majuto! Mimi hufanya makosa mengi ndugu
yangu, mimi hujuta mara nyingi, ingawa nilishakataa kuishi katika
makosa na kuishi katika majuto. Lengo langu kukuandikia barua hii leo
ndugu yangu James ni kukukumbusha, si kukuhukumu, kwamba siku moja
utakuja kuwa shahidi wa hiki ninachokisema; UMEIUA NCCR-MAGEUZI kwa
kukubali kumezwa na
Chadema
bila wewe kufahamu, huu kwangu ni ukweli, turuhusu wakati uendelee
kusonga mbele ipo siku mimi na wewe tutakutana na kuzungumza. Kwa
kukubali kwako kuwaunganisha wanaNCCR-MAGEUZI na Ukawa, hakika
umekichimbia chama chako kaburi bila kufahamu. Nia ilikuwa njema ya
kuongeza nguvu ili muweze kuing’oa CCM, jambo moja ambalo hukulifahamu
ni kwamba ulikuwa ukishughulika na mwanadamu ambaye mimi siku zote
naamini ni ‘clever’, mtu huyu si mwingine bali ni Freeman Mbowe. Ukitaka
kuamini kwamba
Mbowe
ni ‘clever’ angalia alikoitoa Chadema na alikoifikisha bila kuwa na
digrii hata moja kichwani mwake! Huyu ndiye mtu ambaye ndugu yangu James
Mbatia ulikutana naye, wewe ukiwa ‘intelligent’ lakini ukawa si
‘clever’ na kulitumbukiza tone la NCCR-MAGEUZI kwenye pipa la Chadema,
ndugu yangu hiki ni kifo cha NCCR, amini usiamini.
Kwa
mujibu wa kamusi yangu, kuna tofauti kati ya neno intelligent na
clever. Intelligent ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri juu ya jambo
na kupata jibu, sifa hii ndugu yangu James Mbatia unayo, hakuna ubishi,
Watanzania wote wanajua lakini kwa mujibu wa kamusi yangu, clever ni mtu
mwepesi wa kuelewa, kujifunza na kupata majibu kwa kasi, hata kama
hatumii elimu ya darasani, huyu ndiye Mbowe ambaye mimi na wewe
tunamfahamu.
Ndugu
yangu James, naomba usikasirike, nipe muda niongee na nikupatie taarifa
za wanachama wako huku chini, wanalalamika chama chao kimeuzwa,
mwenyekiti wa chama chao kaweka maslahi binafsi mbele kwa kujiunga na
Ukawa sababu Ukawa wakishinda yeye atapata madaraka, hayo ndiyo
yanayosemwa! Wanadai ukiliangalia bango la Ukawa lenye picha ya Edward
Lowassa mtaani, hauoni kitu chochote cha kuonesha kwamba kuna
NCCR-MAGEUZI katika Ukawa, maana rangi ni ya Chadema, alama ya vidole
viwili ndiyo pekee inayoonekana kwenye bango hilo na Chadema ndiyo chama
pekee kinachotajwa! Sasa swali wanalojiuliza, NCCR-MAGEUZI yao iko
wapi?
Bila
shaka wamemezwa na Chadema. Matarajio yaliyopo sasa hivi ni kwamba
Ukawa itashinda na kuchukua dola, siwezi kuongea sana kuhusu hilo maana
chini ya umoja huo mnazo nguvu, lolote linaweza kutokea! Swali
ninalojiuliza mimi na ambalo pia wewe unatakiwa kujiuliza ni kwamba,
hivi ikitokea CCM ikashinda, itakuwaje kuhusu chama chako NCCR-MAGEUZI?
Utaanza
tena kujenga msingi kuanzia chini? Kama nilivyosema hapo juu, siandiki
haya kukuhukumu bali kukukumbusha na kama kuna uwezekano uanze kuchukua
hatua hivi sasa za kuhakikisha NCCR-MAGEUZI inakuwa hai ndani ya Ukawa,
inaonekana ndani ya Ukawa, badala tu ya wewe kuonekana kwenye runinga
ukijibu hoja au kuongea na waandishi wa habari. Mbatia una akili nyingi
mno, hivyo ndivyo ilivyo familia yako yote, dada yako Ndelakijo Kessy
Mbatia
ni mkali wa hesabu na nilisoma hivi karibuni kwamba yeye ndiye Kaimu
Katibu Mkuu wa NCCR-MAGEUZI kwa hivi sasa, inakuwaje hulioni hili jambo
linalokijia chama chako? Hakika kwa mara ya kwanza umethibitisha kwamba
kumbe mwanadamu anaweza kuwa ‘intelligent’ lakini akawa si ‘clever’.
Tatizo hili ndilo limefanya wafanyabiashara wa kimataifa ambao ni
clever, kuwasainisha viongozi wetu wa Kiafrika mikataba mibovu ingawa
wana elimu kubwa lakini si ‘clever’.
Ndugu
yangu Mbatia, Nakusihi utafakari jambo hili kwa undani, nakuomba sana
udai kuonekana (Visibility) kwa chama chako katika Ukawa, tofauti na
hapo umemezwa na huo ndio utakuwa mwisho wa NCCR-MAGEUZI au utakuwa na
kazi kubwa sana kukirejesha kwenye hali yake baada ya uchaguzi huu
ikitokea mkashindwa. Naomba niishie hapa, nakutakia kila la kheri katika
mapambano yako, Mungu akubariki wewe, familia yako na pia ibariki nchi
yetu Tanzania, katika uamuzi wowote utakaoufanya hapo mbele, nakuomba
uiweke amani ya nchi yetu katikati ya maamuzi yako, hiyo ndiyo sababu
Mungu amekupeleka Ukawa, usikubali kabisa nchi hii iingie katika
machafuko
Wasalaam,
Eric Shigongo James

0 comments:
Post a Comment