Shamma Gwajima (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kushoto ni Raphah Gwajima.
*********
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ametumiwa
waraka mzito na wanaodai kuwa watoto wa kaka yake Gwajima, Faustine
Mathias Gwajima, ambaye kwa sasa ni marehemu, wakimtaka askofu huyo
kumfufua baba yao ndani ya siku 14 la sivyo watamfikisha mahakamani kwa
kile walichokitaja kuwa amewasababishia athari kubwa za kisaikolojia kwa
muda mrefu.
Wakizungumza
mapema leo hii na waandishi wa habari Idara ya Habari Maelezo, Jijini
Dar, watoto hao waliojitambulisha kwa majina ya Shamma Gwajima (18) na
Raphah Gwajima (17) walisema kuwa baba yao ambaye ni kaka wa Askofu
Gwajima alifariki dunia mwaka 2008 mkoani Mwanza kwa maradhi ambapo
Askofu Gwajima wanayemwita baba mdogo alifika msibani hapo na kuwataka
ndugu na marafiki waliokuwa wakiomboleza kifo cha mpendwa wao
wasihuzunike kwa kuwa marehemu hakuwa amekufa bali amelala tu.
“Mchungaji
Gwajima alitukataza tusilie na tusihofu kwa chochote kwa kuwa alikuwa
na uwezo wa kumuombea marehemu hadi afufuke. Kauli hiyo ilitufanya
tuanze kufurahi na akaushika mwili wa marehemu katikati ya umati wa watu
na kuanza kuutikisa akimtaka baba yetu aamke lakini hakuamka,” alisema
Shamma.
Watoto
hao walidai kuwa tangu siku hiyo Gwajima aliondoka kimyakimya na
kuingia mitini na kudai kuwa jambo hilo limewaathiri kihisia na
kisaikolojia na wanajiandaa kumshtaki kutokana na usumbufu
aliowasababishia katika kipindi kigumu cha msiba wa baba yao.
Watoto
hao walienda mbali zaidi na kudai kuwa waliamua kukaa kimya wakiamini
Askofu Gwajima ambaye ni baba yao mdogo anastahili heshima ya kichungaji
mbele za watu, lakini walidai kuwa wanashangazwa na mambo ayafanyayo
hivi karibuni kama vile kuwatukana watumishi wenzake na kutoa siri za
waumini wanaoenda kwake kwa ajili ya kupata huduma za maombezi.
Aidha
walidai kuwa Askofu Gwajima ni tapeli kwa kuwa anatumia huduma ya
kufufua misukule ‘hewa’ kwa maslahi yake binafsi na kuitaka serikali
iingilie kati kumchukulia hatua huku wakiitaka jamii isikubali
udanganyifu wa askofu huyo kwa kuwa kama kweli anafufua watu basi
angemfufua kaka yake.
“Je,
misukule ambayo anatangaza ameifufua, tujiulize kabla ya kufariki
ilikuwa ikiishi wapi? Na, je, kuna vyeti vya kifo vinavyothibitisha kama
watu hao wanaofufuliwa walikufa kweli? Je, ndugu wa hiyo misukule
wapo?” walisema watoto hao na kuongeza kuwa kutokana na kushindwa kwake
kumfufua baba yao, Gwajima amewatelekeza kwa kutowapa msaada wowote
licha ya yeye kuishi maisha ya kifahari.

0 comments:
Post a Comment