Tuesday, October 13, 2015

Nanyumbu. Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa juzi alianza kuruka na chopa katika kampeni za mwisho za kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli na alitumia fursa hiyo kumvaa aliyekuwa waziri wake mkuu kwa miaka 10, Frederick Sumaye.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika juzi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mangaka, Nanyumbu, Mkapa alisema kauli ya Sumaye kuwa Serikali ya CCM haijafanya lolote kwa miaka 50 ni ya kusikitisha kwa kuwa ni upotoshaji wa makusudi.
Mkapa aliyejitokeza ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki kampeni za CCM tangu aliposhiriki uzinduzi wa kampeni hizo Agosti 23, mwaka huu, alisema Oktoba 25 unafanyika uchaguzi kutafuta amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama ambaye akitoa amri inatekelezwa mara moja ambaye ni Dk John Magufuli wa CCM.
Mkapa ambaye aliwasili kwa chopa katika uwanja huo, alisema kitendo cha mawaziri wakuu kudai kuondoa umaskini kwa siku 100 wakati wamedumu serikalini zaidi ya miaka 13 na hawajafanya hivyo ni kuwalaghai vijana kwa maslahi binafsi.
Alimgusia pia mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, Edward Lowassa, kuwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere amekuwa akikatwa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa sababu mbalimbali zikiwamo za ukiukwaji wa maadili.

Magufuli na mafisadi
Katika hatua nyingine, mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa kuteuliwa kwake kugombea urais kupitia chama hicho kumesababisha mafisadi kukihama.
Dk Magufuli alieleza hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mpilipili, Manispaa ya Lindi.
Alisema rekodi yake ya utendaji na uadilifu ndani ya Serikali umewafanya mafisadi wenye uchu wa madaraka, waliogombea urais na kushindwa ndani ya chama hicho, wajiondoe kwa kuwa wanajua kwamba hapendi ufisadi, wazembe na wala rushwa.

Amnadi Nape
Magufuli aliwataka wananchi wa Mtama kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Nape Nnauye ili awaletee maendeleo, huku akilaani kitendo cha kundi la watu ambao alisema wanatumia fedha nyingi kumkwamisha.
“Ndugu zangu kuna kundi la mafisadi wamejipenyeza jimboni Mtama, wanamwaga fedha ili Nape asishinde kuwa mbunge wa jimbo hili, nawaomba fedha pokeeni, kura mpeni Nape,” alisema Magufuli.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Magufuli ni mtu sahihi kwa nafasi, hivyo aliwaomba wanaCCM kumpa kura.

Sendeka akerwa kudeki barabara
Akiwa katika mkutano wa kumnadi mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan mjini Geita, mjumbe wa kamati ya kampeni ya chama hicho, Christopher Ole Sendeka alilaani kitendo cha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kuruhusu vijana kusafisha barabara ya lami ili msafara wake upite.
Juzi mjini Musoma na jana Jijini Mwanza walijitokeza vijana na kupiga deki barabara ili Lowassa apite, wakisema hawataki apate mafua.
Sendeka jana alikemea kitendo hicho katika mikutano kadhaa mkoani Geita akisema, “Lowassa anatumia umaskini wa vijana wetu kuwalipa fedha ili wamwage maji kwenye barabara ya lami kusafisha barabara msafara wake upite. Huo ni utumwa si utumwa?” aliuliza Sendeka na kujibiwa na wananchi kwa sauti, “Ni utumwa.”
“Namtaka Lowassa asitumie nafasi yake ya ugombea urais kudhalilisha utu wa vijana kwa sababu ya fedha zake, tena ambazo hakuzipata kihalali kuwalipa vijana wetu eti wakamsafishie barabara ya lami apite,” alisema.
Sendeka alisema kitendo hicho cha aibu kimeona matairi ya gari la Lowassa yana thamani kuliko utu wa vijana.
“Kama kweli hakufadhili mpango huo wa kulipa vijana wafanye hivyo kwa nini hakuwakataza alipoona wanamwaga maji ili msafara wake upite,” alihoji.

Samia na wachimbaji wadogo
Kwa upande wake, Samia alisema Serikali ya awamu ya tano itahakikisha wachimbaji wadogo wa mkoa huo wanapata maeneo ya uchimbaji.
“Tutapitia upya leseni za maeneo ya uchimbaji zilizotolewa sasa na kuangalia maeneo ambayo yapo wazi ili tuyagawe kwa wachimbaji wadogo,” alisema Samia.
“Tutatoa mafunzo na ruzuku kwa wachimbaji hao kama njia ya kuwawezesha kielimu na kiuchumi ili waweze kuendesha shughuli zao za uchimbaji.”
Samia alisema pia akiingia madarakani atatatua kero za maji, umeme, barabara, elimu na afya ya wakazi wa jimbo hilo.

Imeandikwa na Suzan Mwillo, Mwanja Ibadi, Amini Yassin na Amini Yasin.

0 comments:

Post a Comment