TAARIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI KWA VYOMBO VYA HABARI - JUMAPILI OKTOBA 11, 2015. Tunapenda kuwataarifu wanachama wetu na umma wa Watanzania kuhusu masuala yafuatayo: Mwenendo wa Kampeni za CCM
Mgombea Urais wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, na Mgombea Mwenza,
Ndugu Samia Hassan Suluhu, wameendelea kufanya kampeni katika maeneo
mbalimbali nchini.. Hadi jana, tarehe 10.10.2015, Dkt. Magufuli
alikuwa amekwishatembelea Mikoa 22 na Majimbo 203. Amekwishafanya
mikutano mikubwa rasmi 240 na mikutano 865 ya kusimamishwa na wananchi
njiani, hasa wananchi wa vijijini. Dkt. Magufuli amekuwa akitumia
usafiri wa barabarani, ambapo hadi sasa ametembea kilomita 31,467 kwa
barabara kuu, barabara za mikoa, barabara za wilaya, barabara za mlisho (feeder roads), na barabara za mijini na vijijini.
Watu wengi wamekuwa wanajitokeza kwenye mikutano yetu. Lakini la muhimu
zaidi ni hamasa na matumaini wanayopata baada ya kumuona jukwaani na
kumsikiliza Dkt. Magufuli. Wananchi wanapoondoka kwenye mikutano yetu ya
kampeni wanakuwa wamepata fursa ya kumsikia mgombea wetu kwa kitambo
kinachotosheleza, wamemuelewa, wameelewa sera za CCM na wameshawishika kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi.
Tunaingia katika ngwe ya mwisho ya kampeni zetu. Tangu kampeni zianze
hadi sasa, ushindi wa CCM unajidhihirisha. Hata hivyo, katika
kujihakikishia ushindi na kuongeza kiwango cha ushindi, katika ngwe hii
ya mwisho, tumeanza kampeni nzito. Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu
Abdulrahman Kinana, ameanza ziara ya kampeni katika majimbo 64.
Vilevile, viongozi wengine wa CCM, akiwemo Rais na Mwenyekiti wa CCM
Mstaafu Mzee Benjamin William Mkapa, nao wataanza safari za kuzunguka
nchi nzima kumuongezea kura Dkt. Magufuli na wagombea wetu wa Ubunge na Udiwani. Tutatumia helikopta nne kwa ajili ya shughuli hii. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wataendelea kutumia usafiri wa gari hadi mwisho wa kampeni, isipokuwa pale tu itakapokuwa hakuna budi.
Maandalizi ya Kuleta Mabadiliko ya Haraka na ya Kweli. Pia, tunapenda
kutoa taarifa kwamba, mgombea wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, ameunda
jopo la wanataaluma na wataalamu huru magwiji wazalendo wa uchumi,
biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu,
asasi zisizo za kiraia, na sekta binafsi, kwa ajili ya maandalizi ya
kufanya mabadiliko makubwa Serikalini kuanzia siku ya kwanza atakayokuwa
madarakani. Dkt. Magufuli amelipa jopo hili majukumu yafuatayo:
1. Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi,
ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili atoe
maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa; 2. Kuchunguza na
kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua
za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa; 3. Kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali;
4. Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi
zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila
kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa. 5. Kupitia sheria
zote za nchi na kuorodhesha Sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka
ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa
Watanzania; 6. Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
7. Kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na kutengeneza rasimu za
mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wakuu
atakaowateua mara baada ya kuapishwa. 8. Kupendekeza njia za haraka
za kumaliza kero za watumishi wa umma,hasa walimu, askari, madaktari na
wauguzi, ili aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma
mabadiliko ya kweli. 9. Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa
utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa
upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika; 10. Kupendekeza
muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa
shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini. Dkt. Magufuli ameazimia kuanza kazi mara moja kwa bidii kubwa na maarifa mapya. Imetolewa na:- January Makamba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM 11 Oktoba 2015 |
0 comments:
Post a Comment