Thursday, October 15, 2015



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya 
Mrisho Kikwete amesema kuwa michezo ya Tanzania inadumaa na kushindwa kuendelea kwa sababu ya uongozi mbaya na viongozi ambao wanajali zaidi vyeo kuliko kuendeleza michezo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa sababu kubwa ya pili
inayudumaza michezo katika Tanzania ni kushindwa kwa viongozi kukubali ukweli kuwa wanamichezo lazima walelewe na kuanza kupewa mafunzo wakati bado wadogo na wenye umri wa chini.
Rais vile vile amesema kuwa ili kuweka msingi wa ulezi wa wanamichezo bora wa Tanzania, ametoa “ofa” yake ya mwisho kwa wanamichezo kwa kuwajengea Kituo cha Kulea Vipaji vya Watoto Wadogo kilichojengwa eneo la Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumanne, Oktoba 13, 2015, alipozungumza katika halfa rasmi iliyoandaliwa na wanamichezo wa Tanzania kutambua mengi ambayo kiongozi huyo ameifanyia sekta ya michezo katika miaka 10 ya uongozi wake na kumuaga. Katika halfa hiyo ambayo msimamizi wake mkuu kilikuwa ni Chama cha Waandishi wa Michezo Tanzania (TASWA) kwenye Ukumbi wa Mlimani City mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete ameelezea mapenzi na ushiriki wake katika michezo maishani mwake akisisitiza:

“Kwa rekodi yangu mimi ni mpenzi wa michezo na mwanamichezo. Hivyo nchi yetu isipofanya vizuri katika michezo mbali mbali ni jambo linalonisononesha sana.”
Ameongeza: “Kwa maoni yangu yapo matatizo mawili makubwa katika uendeshaji wa michezo yetu. Tatizo kubwa la kwanza ni viongozi ambao wanaingia katika uongozi wa michezo kwa heshima tu ya kutafuta vyeo na kutunisha CV zao. Wengine wanaitwa wenyeviti, wengine wanaitwa marais. Jambo kubwa hapa siyo kuwa na cheo, isipokuwa ni jambo gani unalifanya kwa kutumia cheo hicho…kwa hakika maelezo ya kwa nini tunaendelea kufanya vibaya katika michezo siyaelewi kabisa mimi.”

Rais Kikwete ametoa mfano wa maamuzi mabaya yanayofanywa na viongozi wa michezo nchini: “Nimesema mimi kuwa Serikali italipia makocha wa michezo. Lakini viongozi wetu wa michezo hata hawaelewi hata maana halisi ya makocha wazuri. Sisi tunaleta makocha wao wanawaondoa. Ukweli ni kwamba ukipata mwalimu mzuri mambo ya michezo yatakwenda vizuri.”

“Hakuna mbadala wa mwalimu mzuri na ndiyo maana Serikali ilisema kuwa italipia makocha. Kama klabu zina walimu wazuri ni dhahiri utapata wachezaji wazuri. Kama huna mwalimu mzuri huwezi kupata timu nzuri…huwezi kuvuna usichopanda.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Matatizo yetu yako kwenye uongozi. Kuna kitu mahali katika uongozi wetu wa michezo hakiendi vizuri. Na hili lazima nyie watu wa michezo mlitafutie majawabu yake. Kazi hiyo haiwezi kuwa ya Rais wa nchi.”

Rais Kikwete ameongeza kuwa tatizo kubwa la pili ni kwamba Tanzania haiwekezi ipasavyo kuendeleza na kulea vipaji vya watoto, tokea wakiwa wadogo. “Klabu zetu hazitaki kuwekeza katika watoto wadogo. Kazi yao ni kupora wachezaji kutoka timu nyingine wakati wote. Mfano mzuri ni jinsi miaka ya 1970, klabu ya Yanga ilivyowekeza katika watoto ambao walikuja kuwa wachezaji hodari sana wa Tanzania.”

Amesema Rais Kikwete: “Nawashukuru kwa kuniaga na kutambua tuliyoyafanya kwa pamoja wakati wa kipindi changu cha uongozi kwenye eneo la michezo. Na mimi nimeamua kutoa “ofa” yangu ya mwisho kwa wanamichezo wa Tanzania kwa kuwajengea Kituo cha kufundisha na kulea vipaji vya watoto wa Tanzania katika michezo mbali mbali”.

Kituo hicho kinachojulikana kama Kikwete Sports Park (KSP) kitafunguliwa rasmi Jumamosi wiki hii, Oktoba 17. Fedha za ujenzi wa Kituo hicho zimetolewa na Kampuni ya Umeme ya Symbion Power na kitaendeshwa na watalaam wa klabu ya soka ya Ligi Kuu ya England, Sunderland ambayo pia itatoa makocha wa soka. NBA ya Marekani itatoa makocha wa mpira wa kikapu.
Imetolewa na:
 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Oktoba, 2015

0 comments:

Post a Comment