Tunawakaribisha sana ndugu na wadau wetu waandishi wa habari toka vyombo mbali mbali kwa kuja na kushiriki nasi katika mkutano wetu huu nuhimu Makao Makuu ya UVCCM leo oktoba 5 2015.
Tumewaita kwa sababu kadhaa muhimu za kisiasa tukiamini na kutegemea mtafikisha ujumbe wetu kwa jamii kama mnavyotimiza wajibu wa kazi zenu ngumu na nzito za kitaaluma za kila siku.
Hata hivyo UVCCM tunawashukuru kwa dhati waandishi wa habari nyote kwa kazi kubwa mnazozifanya za kuihabarisha jamii kuhusu mwenendo bora wenye mafanikio kwa maendeleo ya kampeni zinazofanywa na mgombea wetu wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dk. John Pombe
Magufuli na Mgombea Mwenza wake Ndg. Samia Suluhu Hassan.
Magufuli na Mgombea Mwenza wake Ndg. Samia Suluhu Hassan.
Vile vile tunawapongeza kwa namna ya pekee jinsi mnavyotuhabarisha na kutupasha kuhusu maendeleo ya kampeni za mgombea wetu wa urais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein sambamba na wagombea wetu wa ubunge, uwakilishi na madiwani Tanzania Bara na Zanzibar.
Ndugu waandishi wa habari
Kwa namna moja maendeleo ya kampeni za chama chetu zinakwenda vizuri hasa upande wa Tanzania Bara lakini huko Zanzibar kidogo kumejichomoza vitendo vya kihuni vinavyofanywa na wafuasi wa vyama upinzani.
Kati ya tarehe 15 na 18 Septemba Mwaka huu misafara ya wanachama wa CCM katika maeneo ya Kuyuni, Mtuhaliwa na Chokocho katika Mkoa wa Kusini Pemba, imeshambuliwa kwa kupigwa mawe wakati wakirejea toka kuhudhuria mikutano ya kampeni, baadhi ya watu wamejeruhiwa na kupata majeraha ikiwemo gari moja kuvunjwa kioo cha mbele.
Kitendo hicho ni cha kihuni, UVCCM tunakilaani kwa nguvu zetu zote lakini pia hayo ni matokeo ya hotuba za Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad ambaye mara kadhaa amekuwa akisema mwaka huu vijana wake hatawaonya watakapotaka kufanya jambo lolote, hatawazuia wala kuwaasa.
UVCCM tunamkanya Seif na CUF kuacha mara moja tabia ya kutaka kumshika paka sharubu, paka mara zote huchezewa maeneo mengine ya mwili wake si sharuhu zake, ukimshika sharuhu atakuparamia usoni, kukuparua na pengine hata kudhuru macho yako.
Kufikiwa kwa Maridhiano ya Kisiasa kati ya CCM na CUF huko Zanzibar lengo lilikuwa kuendesha siasa za kiungwana, kistaarabu na kuvumiliana. Kuondosha siasa za mti kwa macho, hasama na kuzika chuki.
Ikiwa CUF wameleweshwa na ustawi wa amani iliopo sasa Zanzibar tokea kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hatutaona muhali, shida wala kikwazo cha kurejea tena katika zama ya vuta nikuvute ile ile iliokuwepo kabla ya kufikiwa maridhiano ya kisiasa.
Ndugu Waandishi wa habari.
Jambo jingine ni kuhusiana na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru jana Septemba 4 mwaka huu kutangaza kuihama CCM huku akitoa matamshi ya kukisakama na kukiponda chama chetu akiwa hana nguvu ya hoja.
Itakumbukwa Agosti 15 mwaka huu Baraza kuu la Taifa la UVCCM lilimvua wadhifa wa Ukamanda Mkuu wa Jumuia yetu baada ya kutoridhishwa na mienendo ya mwanasiasa huyo baada ya jumuiya yetu kumpima na kumlinganisha na mwanasiasa mwenye akili zinazofanana na mbayuwayu.
UVCCM wakati tukitoa uamuzi wetu, wapo baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa walibeza na kuona kama tulimuonea au kumdhalilisha Mzee Ngombale.
Nataka nieleze bayana kuwa kabla ya kumvua ukamanda wa UVCCM tulimtathmini, tulimchambua na kumkuta tayari amepotea njia na kumkuta kwa hiari yake akiamua kujivika joho la utumwa na kujitolea kumtumikia shetani ili kujaza tumbo lake na si uaminifu tena kama alivyokuwa akiheshimika hapo awali tokea enzi za TANU na ASP kabla ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi mwaka 1977.
Mwanasiasa huyo ametoa porojo huku akipapatua kwa lengo la kutaka kuionyesha hadhira kuwa CCM si chama makini akisahau katika uhai na maisha yake yote amekuwa akisema hakitatokea chama bora nchini, kuishinda na kitakacholingana na CCM.
Tokea akiwa kijana mdogo kabisa Mzee Kingunge amekuwa mwanachama wa jumuiya yetu hadi kufikia kuwa Katibu Mkuu wa Pafmeca Youth iliokuwa na Makao makuu yake nchini Algeria
Kilichotokea ni kwamba Mzee Kingunge ameshindwa kuheshimu matokeo ya mchuano wa nguvu ya hoja ndani ya chama chetu huku akitaka kulazimisha fikra zake ndizo zionekane sahihi na za wenzake zikikosa maana na umuhimu wowote.
Kimsingi huo si uungwana katika dhana ya siasa, huo ni uimla na ufashisti usiokubalika katika siasa za kileo. Alifikiri CCM ni mtu, umbo na uso wake, si taasisi pia akidhani mtu mwenyewe ni yeye na si wengine au maamuzi yatokanayo na vikao vya kikatiba akiviona havina maana wala uzito kuliko fikra na utashi wake binafsi.
Anaposema taratibu za kumpata mgombea zilikiukwa sijui ana maana ipi wakati yeye hakuwa mjumbe wa NEC, Kamati Kuu ya CCM na wala Mkutano Mkuu wa Taifa.
Chama chetu hakiwezi kuendeshwa kinyume na taratibu za Katiba ya CCM kama anavyodai na kufikiri Mzee Kingunge hasa katika mchakato wa kumpata mgombea wa chama chetu kwa nafasi ya urais.
Mzee Kingunge toka awali amekataa kujiegemeza katika kuamini na kusimamia taratibu za kumsaka na kumpata mgombea wetu wa urais kulingana na sifa za msingi badala yake akimtaka mtu hata kama mgombea huyo ameopungukiwa sifa na vigezo vya kuwa mgombea bora wa urais na mwenye sifa zinazolingana na hadhi ya chama chetu.
Lilipokatwa jina la Edward Lowassa Mzee Kingunge akawa mbogo, asiejenga nguvu ya hoja ila akiandaa mipango na mazingira ya kukitishia nyau chama chetu ili kimuogope na kuyaridhia matakwa yake.
Mzee Kingunge ameshindwa kuelewa na kukubali ukweli kama urais ni taasisi adhim yenye staha na hakutaka aamini kama urais si kama mchezo wa bao au karata ila ni vigezo, sifa njema na amana kwa mgombe mhusika katika jamii inayomtazama na kumtegemea
Anaposema taratibu CCM zimekiukwa, hazikuwa sahihi na kinyume na demokrasia, tunamuuliza hivi kilichofanyika chadema hadi kumpa mgombea wa urais ndiyo mchakato makini wa demokrasia anayoitamani?
UVCCM tunaungana na kukubaliana na uamuzi wa vikao vya chama chetu uliofuatwa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na katiba yetu katika kumpata na kumteua mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea urais wa Zanzibar.
Chama chetu kitabaki kuwa ni imara daima, kitahimili na kukabiliana na misukosuko na dhoruba za kisiasa na kwamba wakati wote tunaamini hakuna mwanachama au kiongozi mmoja ambaye ni muhimu au bora kuliko mwingine
Mzee Kingunge amewahi kutoka dini na kusema hakuna mungu haikuwa lolote, sasa amehama CCM si jambo la ajabu, hata akiamua kusaliti na kujitoa kwenye kabila lake bado atahesabika ni Mtanzania wala hayupo mtu atakaemshtua au kumshangaa.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
"KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI "
SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU UVCCM
0 comments:
Post a Comment