Sababu 10 kwa nini
John Magufuli atashinda uchaguzi Mkuu wa Urais 2015
1.
Tanzania bara na visiwani yako majimbo ya
uchaguzi 266, CCM imesimamisha wagombea Ubunge katika majimbo yote 266 huku
Chadema na washirika wake wa Ukawa wakiwa wamesimamisha wagombea katika majimbo
211 (138 toka Chadema). Kati ya majimbo hayo 266, CCM tayari imepita bila
kupingwa Jimbo 1. Ukichukua majimbo 265 yaliyobaki na kutoa 211 ambayo
Chadema na washirika wake wamesimamisha wagombea unabaki na majimbo 48 ambayo
CCM haina upinzani wa Chadema wala washirika wake wa Ukawa. Majimbo haya 48 CCM
ina uhakika wa kushinda walau kwa asilimia 90, ushindi huu si kwa Wabunge tu
bali pia kwa mgombea Urais wa CCM.
2.
Watanzania waliojiandikisha kupiga kura mwaka
2015 ni milioni 24.2. Takwimu zinaonyesha CCM ina wanachama hai wapatao milioni
8 wenye kadi na wanaolipia ada zao za uanachama kila mwaka. Kuondoka kwa Edward Lowassa katika Chama Cha
Mapinduzi kunamaanisha Magufuli hatapata kura zote milioni 8 za wana CCM na pia
kihesabu si rahisi wana CCM wote milioni 8 kujitokeza siku ya kupiga kura. Utafiti
unaonyesha kwamba wana CCM watakaopiga kura hawatazidi asilimia 90 ya wanachama
wake (milioni 7.2) huku milioni 7 kati yao wakimpigia kura John Magufuli.
Historia ya CCM inaonyesha ni wanachama wachache sana humpigia kura kada
mwenzao anapohama kugombea nafasi kwa chama kingine, hasa nafasi ya Urais
(Rejea: Uchaguzi wa Urais 1995, mgawanyo wa kura za Augustine Lyatonga Mrema)
3.
Mizunguko ya kampeni huzaa kura za ziada mbali
na zile za wanachama. Tayari inaonyesha kwamba Magufuli anapita karibu kila
kata ya Tanzania akitumia barabara huku upande wa Lowassa na shirikisho la
Ukawa hali ikiwa tofauti, ambako amekuwa akifika sehemu chache akitumia usafiri
wa ndege na helkopta na ni wazi hana stamina ya kuzunguka kwa gari nchi nzima
kutokana na tatizo la kiafya. CCM ina
mizizi kwenye mashina kuanzia ngazi ya nyumba kumi. Mtandao huu wa Chama pamoja
na safari za mgombea wao kila kata ni kiashiria kwamba atafikia wapiga kura
wengi zaidi hasa sehemu za vijijini na ambazo si rahisi kufikika. Tafiti
zinaonyesha huko ndiko kwenye wapiga kura wengi na kuwafikia ni hatua moja
kuelekea kuzipata kura zao na kushinda.
4.
Chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2014
zinaonyesha kwamba CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 80 kwenye nafasi za
uongozi za serikali za vijiji na mitaa. Ikumbukwe kwamba CCM ilipata ushindi
huu licha ya ushindani mkubwa uliokolezwa na sakata la Escrow wakati huo. Hii
inaonyesha kwamba CCM iliweza kushinda hata wakati huo wa changamoto. Ni mwaka
mmoja tu umepita tangu chaguzi hizo zifanyike. Kitafiti, hiki ni kiashiria
kikubwa kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM kama chama kinaenda
kwenye sanduku la wapiga kura kikiwa na rekodi nzuri kuweza kushinda.
5.
Rekodi ya Utendaji ya Magufuli inavutia
Watanzania wengi. Utafiti unaonyesha kwamba wapinzani wake majukwaani mpaka
sasa wanapata wakati mgumu kutaja jina lake moja kwa moja kumuhusisha na
utendaji wa hovyo. Mitandaoni zipo video na nukuu nyingi zikiwemo za Mgombea wa
Ukawa Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wengineo wakisifia
utendaji wa Magufuli. Katika siasa na kampeni, hatua moja kuonyesha mgombea
anashinda ni kushindwa kwa wapinzani wake kumnyooshea kidole moja kwa moja au
kukosa mabaya ya kusema dhidi yake. Asiye na la kukusema vibaya anawapa
wananchi nafasi ya kuona mazuri yako na kushinda.
6.
Suala la afya ya wagombea limekuwa gumzo kubwa
katika uchaguzi wa mwaka huu. Huku ikiwa wazi kwamba Mgombea wa Ukawa Edward
Lowassa anaugua ugonjwa wa Parkinson’s kwa muda mrefu sasa, Magufuli hajawa na
changamoto ya afya. Ugonjwa wa Parkinson’s alio nao Edward Lowassa unaathiri
ubongo wa kati, moyo, mishipa ya fahamu na uwezo wa kufikiri (Afya ya mwili maeneo hayo ni muhimu kiongozi
kuwa nayo). Kwa muda mrefu Lowassa amekuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huu
katika hospitali maarufu ya Franziskus-Krankenhus mtaa wa Budapester jijini
Berlin, Ujerumani. Kiumri Magufuli ana
miaka 55 huku Lowassa akiwa na miaka 63. Wapiga kura huchagua kiongozi kwa
kutazama muonekano na ni wazi kabisa kwamba kwa muonekano na hali ya kiafya ya
Lowassa ni dhoofu na inazidi kudorora siku hadi siku na kuwakatisha tamaa hata
wanaomuunga mkono. Tangu kampeni zianze hakuna mahala ambapo amewahi kuzungumza
kwa zaidi ya dakika 15. Hivyo basi, kwa kadiri siku zinavyoenda Watanzania
watazidi kubaini kwamba Lowassa hana afya ya kuhimili vishindo vya kampeni wala
uwezo wa kumudu majukumu ya Urais.
7.
Nguvu ya vyama, oganaizesheni na ilani. Magufuli
anatokea CCM ambayo kama nilivyoeleza juu ina nguvu ya kuwepo kila kijiji na
kila nyumba kumi Tanzania; imetoa marais waliotangulia, na hata wapinzani
wametoka katika CCM hiyo hiyo baada ya kukosa nafasi za kugombea kupitia chama
hicho. Kwa miaka mitatu iliyopita Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
amezunguka kila kona ya nchi akikinadi chama chake, hii ni aina ya kampeni
ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa upande wa upinzani hali iko tofauti.
Mgombea wao, Lowassa alikuwa mwanachama wa CCM miezi miwili iliyopita, kuingia
kwake Chadema kumeleta mpasuko huku Katibu Mkuu wake akitokomea kusikojulikana,
na Mwenyekiti wa CUF, Lipumba naye akijiuzulu uongozi kupinga Lowassa
kukaribishwa Ukawa. Hii inaonyesha hali si shwari katika upinzani. Kwa sasa
Ukawa wanaficha mpasuko huo kwa propaganda lakini madhara yatajitokeza kabla ya
siku ya uchaguzi. Moja ya viashiria vya mpasuko katika Ukawa ni kuvunjika kwa
makubaliano ya kuweka mgombea mmoja wa Ubunge katika kila jimbo. Zaidi ya
asilimia 70 ya majimbo yana wagombea Ubunge toka vyama vyote vinavyounda Ukawa.
Kwa mfano Lowassa, kama mgombea Urais wa Ukawa, akienda Ubungo ambapo kuna
wagombea toka Chadema, CUF na NCCR atamnadi mgombea yupi?
8.
Kuondoka kwa Dr Slaa Chadema, tuhuma za Mbowe
kuiuza Chadema kwa Lowassa kwa TZS bilioni 10 (ambazo Dr Slaa amezithibitisha)
na ukawa kuhama kutoka kumuita Edward Lowassa fisadi mkuu wa nchi miaka
michache iliyopita hadi sasa kumfanya kuwa mgombea wao. Hii imewakanganya
Watanzania wengi na wote wanaochukua muda kulitafakari wanazidi kupata maswali
zaidi. Uamuzi wa mpigakura katika hali kama hii ni kuendelea kulipigia kura
zimwi alijualo (CCM) kuliko zimwi jipya asiloelewa (Ukawa).
9.
Matumizi makubwa ya fedha katika kutafuta
madaraka. Mpaka mwisho wa mwezi Agosti 2015 Lowassa alikuwa tayari ametumia
zaidi ya TZS bilioni 106 kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kwanza kutafuta
nafasi kugombea ndani ya CCM na kisha kuhamia Ukawa. Wananchi wengi wanahoji
zinapotoka fedha hizi, wengi wakikumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba
“Mtanzania wa leo hawezi kukununua kabla ya yeye kwanza kununuliwa”. Wananchi
wanahoji namna gani Lowassa anapanga kurejesha fedha hizi iwe zake (pia
wanahoji kazipataje) au za marafiki zake (lengo lao kumpa fedha ni nini).
Magufuli hana kashfa ya namna hii na hata kampeni zake za kuomba kuteuliwa
ndani ya CCM hazikuwa za matumizi ya
fedha kabisa. Kama wananchi watapiga kura kwa kuangalia uadilifu katika kupata
na kutumia fedha, na pia kama watapiga kura wakiamini kwamba Ikulu si mahali pa
kufanya biashara ili mtu arejeshe fedha alizotumia wakati wa kampeni na kuhonga
kupata nafasi basi Magufuli ana nafasi kubwa ya kushinda.
10.
Mzimu wa Mwalimu Nyerere: Mwaka 1995 Mwalimu
Nyerere alisema wazi kwamba Lowassa hafai kuwa Rais wa Tanzania, alikatwa jina
lake kwa haki (video ya Mwalimu akisema haya
iko mitandaoni na ni moja ya video zinazotazamwa kwa wingi wakati huu wa
uchaguzi mkuu) na hakuna maana kuendelea kumjadili na kwamba chama kisonge
mbele. Watu wanaomjua vizuri Lowassa na shughuli anazozifanya wanasema kwa
miaka 20 Lowassa hajabadili zile sifa zilizomfanya Mwalimu kutamka maneno yale
mwaka 1995. Hata alipoomba familia ya Mwalimu Nyerere kumuunga mkono
alipoondoka CCM alijibiwa wazi kwamba yeye hajawahi kuwa chaguo la
Mwalimu. Watanzania bado wanamuheshimu
na kumuamini Mwalimu Nyerere na ni wazi watachagua kiongozi wakifuata wosia
wake. Uadilifu wa Magufuli utamuwezesha kuaminiwa na Watanzania na kushinda
nafasi hii. |
0 comments:
Post a Comment