Wakati kukiwa na taarifa kwamba Rais Dk.
John Magufuli, anatarajia kupunguza karibu nusu ya wizara zilizokuwapo
kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, imefahamika kuwa wizara zinazolengwa ni
zile zilizopo Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Chanzo kimoja kutoka serikalini
kimeiambia Nipashe jana kuwa wizara hizo zitaunganishwa kwenye wizara
mpya zitakazoanzishwa na Rais ambaye ameweka mkakati wa kuwa na baraza
dogo la mawaziri.
Wizara zinazotajwa kufyekwa ni Ofisi ya
Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Kazi
Maalum, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Wizara Ofisi
ya Waziri Mkuu na Sera, Uratibu na Bunge.
Nyingine ni Wizara Ofisi ya Rais,
Utawala Bora, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Wizara ya Nchi,
Ofisi Makamu wa Rais Mazingira na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto.
Kadhalika, katika mabadiliko hayo,
wizara nyingine zitaguswa ili kufikia malengo ya kubakia na wizara
chache kutimiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kubana matumizi na
kuinua maisha ya Watanzania.
Chanzo hicho kimebainisha kuwa Rais Dk.
Magufuli atalitangaza Baraza la Mawaziri ndani ya wiki hii ingawa bado
kumekuwa na usiri wa siku halisi atakayotangaza.
Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya
Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, mwaka huu ikiwa na wizara 30.
Vile vile, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete
alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5,
mwaka huu, tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa
Waziri Mkuu wa serikali yake na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge
la 11.
Juzi, chanzo kimoja kililiambia Nipashe
kuwa tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake,
ameshakamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la
mawaziri na kwamba kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote
kuanzia sasa.
Nipashe
0 comments:
Post a Comment