UNAPOTAJA jina la Ja Rule kwa watu wa Hip Hop, Pop na R&B watakuwa wanalijua vizuri japokuwa miaka ya hivi karibuni umaarufu wa msanii husika umepungua.
Ja Rule, rapa mzaliwa wa Kitongoji cha Queens jijini New York, alihojiwa na kituo kimoja cha redio mapema wiki hii, amefunguka mambo mengi kuhusu safari yake ya kisanii:
Kutojiunga Roc-A-Fella Records
Hii ni lebo ambayo ipo chini ya Jay Z, wakati Ja Rule anatoka kimuziki, Jay Z alikuwa maarufu na alimuomba asaini katika lebo yake hiyo lakini Ja Rule alikataa, hapa anafafanua:
“Sikutaka kusaini katika lebo ambayo kulikuwa na staa au mastaa ambao wanapewa kipaumbele kuliko wengine, ndiyo maana sikujiunga na Roc-A-Fella. Hata Jay nilimwambia kuwa siwezi kujiunga kwenye lebo yake wakati mimi nataka kuwa mkubwa zaidi yake.
“Najua hiyo inatokea kwa wasanii wengi, wanavipaji lakini wanafunikwa na wale wanaokuwa juu yao ambao ndiyo wanapewa kipaumbele kuliko wao, kama ilivyo kwa Drake (yupo chini ya Young Money).”Kweli baada ya kukataa kusaini lebo hiyo, Ja Rule alifanya kazi na watu wengine na akawa msanii mkubwa.
Fast & Furious
Hii ni filamu iliyoteka soko la filamu za Hollywood, imekuwa na mfululizo wa matoleo saba mpaka sasa, Ja Rule alishiriki katika toleo la kwanza la filamu hiyo, baada ya hapo hakuonekana tena, badala yake wakaonekana wasanii wengine, Tyrese na Ludacris.
“Baada ya toleo la kwanza kutoka, nilipata ofa kutoka kwa dairekta John Singleton ili nishiriki toleo la pili, lakini wahusika wengi hawaku-onekana kuwa ‘serious’, mipango ikawa inaenda hovyo-hivyo tu. Waandaaji walinipa ofa ya dola 500,000 wakati huohuo nilikuwa na ratiba ya ziara ya muziki ambayo ingeniingizia dola milioni 13 au 14, hapo unadhani ningechagua kwenda wapi!
“Ila sasa nipo tayari kushiriki kama nitapata ofa nzuri, najua Vin Diesel (mshiriki wa Fast & Furious) ataniita kwa kuwa awali yeye ndiye aliyeniambia nisishiriki kutokana na mambo kwenda hovyo.”
0 comments:
Post a Comment