Jenifa
15th November 2015
Ubinafsi wa CHADEMA makao makuu waikosesha CHADEMA Jimbo la Kyela
Katika majimbo yaliyoniuma kwa CHADEMA kuyakosa ni pamoja na Jimbo la Kyela, kule kwa Mwakyembe.Nilishiriki kufanya utafiti kwa niaba ya timu ya mzee Lowassa juu ya nani angeliweza kulichukua hilo Jimbo kwa niaba ya CHADEMA. Mapendekezo yetu yalionyesha Mwakyembe alikuwa hakubaliki Kyela na hata kura za maoni CCM alishinda kwa kuiba baada ya kubebwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya pamoja na katibu wake.
Katika utafiti wetu ilionyesha George Mwakalinga ambaye ndiye mpinzani mkubwa wa Mwakyembe Jimbo la Kyela alikuwa na nafasi kubwa sana ya kumshinda Mwakyembe. Pia Mwenyekiti wa halmashauri ya Kyela kwa jina la Kipija alikuwa anafuatia kwa Mwakalinga. Mwakalinga alikuwa anakubalika ndani ya makundi yote ya wana CCM lakini pia wana CHADEMA walikuwa wanamkubali na kumwogopa kama angepitishwa na CCM.
Pia mzee Apson Mwang'onda ambaye anatokea Kyela, alifanya utafiti wake na kufanana na wa kwetu. CHADEMA Mbeya nao wakaja na utafiti wao ambao ulikuwa unaonyesha Mwakalinga angelishinda Jimbo la Kyela kama CHADEMA wangempitisha.
Mzee Lowassa na timu yake ili kujiridhisha, wakaongea na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mwakipesile, naye akawashauri kama wanataka kushinda jimbo la Kyela asubuhi wamshawishi Mwakalinga ahamie CHADEMA. Ikishindikana basi Kipija anaweza ingawaje sio kama Mwakalinga.
Wakati huo huo CHADEMA wakawa wamemchagua Mwanyamaki kwenye kura za maoni kuwa mgombea. Uchaguzi wa Mwanyamaki ulileta malalamiko mengi kutoka kwa wagombea wenzake kwamba alitumia rushwa na ushahidi wa MPESA ukaonyeshwa. Wagombea wenzake wakakata rufaa makao makuu na kusisitiza hawatamuunga mkono. Pia ikaonekana Mwanyamaki ni kabila la Mkisi ambalo kwa Kyela sio rahisi kupata uongozi. Wanyakyusa wana ukabila sana hasa kuhusu Wakisi. Mwang'onda na Mwakipesile wakasema wanavyojua wao Mkisi hawezi kushinda Kyela.
Baada ya kujiridhisha, timu ya Lowassa ikawasiliana na Mwakalinga ambaye ndani ya CCM alikuwa anamuunga mkono Lowassa wakati wa mchakato wa urais ndani ya CCM. Pia Mwakalinga anafahamiana na mzee Mwang'onda. Hivyo ikawa rahisi kuongea naye na kumwomba ahamie CHADEMA na aunge mkono mabadiliko. Mwakalinga akasema yeye kabla hata ya kuombwa alikuwa ameamua kuhamia CHADEMA baada ya kuchoshwa na udanganyifu wa CCM Wilaya ya Kyela. Akahakikishiwa na mzee Mwang'onda na timu nzima ya mzee Lowassa kwamba ahamie CHADEMA na atapewa nafasi ya kugombea ubunge. Jina lake likapelekwa CHADEMA ili Kyela iwe kwenye majimbo ambayo wangempa mzee Lowassa kwa ajili ya wanachama waliohamia CHADEMA kutokea CCM. CHADEMA makao makuu wakaridhia na kusema hata utafiti wao unaonyesha ndiye mtu anakubalika zaidi jimbo la Kyela.
Lakini kumbe baadhi ya watu makao makuu hawakufurahishwa kwa sababu ya uhusiano binafsi na Mwanyamaki. Mnyika, Kubenea na Mrema wakamwambia Mwanyamaki kisirisiri akatae na kwamba watamsaidia ili yeye aendelee kugombea Kyela. Wakati kwenye mikutano wakawa wanasema jimbo la Kyela ni la mzee Lowassa, chini chini wakawa wanajiandaa kumtangaza Mwanyamaki kugombea ubunge. Wagombea ubunge wa chadema Kyela walioshindwa wakaandika barua makao makuu kuonyesha wao wataunga mkono Mwakalinga akiteuliwa kuwa mgombea.
Mnyika na kundi lake wakampa fomu Mwanyamaki kimya kimya bila kuishirikisha timu ya mzee Lowassa na wakampa barua ya utambulisho ili akachukue fomu wilayani Kyela. Baada ya kuhakikisha Mwanyamaki yuko Kyela, wakatangaza majina na jimbo la Kyela kumtangaza Mwanyamaki. Hii ilileta ugomvi mkubwa kati ya timu ya mzee Lowassa na CHADEMA makao makuu chini ya Mnyika. Mzee Mwangonda alichukia sana na kuamua kuhusika kwenye kampeni za urais tu, ubunge kuwaachia akina Mnyika.
Matokeo yalipotoka Mwanyamaki akashindwa na Mwakyembe kwa kura elfu tatu. Kuwa Mkisi lilikuwa jambo kubwa kwa wapiga kura wa vijijini. Kila mtu ikawa angelikuwa Mwakalinga. Pamoja na kushindwa ubunge tumeshindwa madiwani kwa CHADEMA kuchukua viti 9 na ccm 24. CHADEMA tumeshinda kata za mjini tu ambako ukabila sio tatizo sana. Na pia kiti kimoja cha udiwani vijijini kutoka kata anayotoka Mwakalinga.
Ubishi na ubinafsi wa kujuana wa akina Mnyika umetukosesha jimbo muhimu sana. Sababu kubwa ni Mwanyamaki kakijenga sana chama na ni rafiki yao hapa Dar. Kuna faida gani kumweka mtu ambaye hawezi kushinda? Leo hii tungelikuwa na kiti kimoja zaidi na halmashauri ya wilaya ya Kyela ingelikuwa mikononi mwa CHADEMA na ruzuku zaidi. CHADEMA makao makuu tumewaangusha wananchi wa Kyela ambao wamechoka na Mwakyembe na waliamua kumtoa. Hili tatizo limetokea pia kwenye majimbo mengine ambako sababu za kukijenga chama kwa muda mrefu zilitumika badala ya uwezo wa mtu. Tujifunze haya yasiendelee kutokea huko mbeleni.
Source:- Jamiiforums
Duh! Huyu dada ni muongo hakuna mfano. Kwakifupi naomba hiyo Jeni ajue kuwa tofauti ya kura za Mwakyembe na Mwanyamaki ni 5000 na sio 3000 kama alivyodai.
ReplyDeleteLakini alikuwa akijaribu kuwadanganya wadau kuwa Mwakalinga ndiye ambaye angefaa na katika kujustify usemi huu ameamua kwa makusudi kudanganya kuwa kata ya kijijini ambayo CDM wameshinda ni nyumbani kwa Mwakalinga, hii si kweli CDM wameshinda udiwani kata ya Ngonga wakati Mwakalinga kwao ni Kata ya Katumba songwe. Watu wa Kyela hawajamchoka Mwakyembe. Lakini haiingii akilini kuwa Mwakyembe aliyepata kura zaidi ya 16000 kwenye Uchaguzi wa ndani ya chama aliziiba kura Zote ukilinganisha na 4000 za Mwakalinga. Tatizo ni kuwa tafiti zinafanywa mtandaoni na sio field. Dada acha kudanganya umma.