Posted by Williammalecela.com on Monday, November 16, 2015
Kauli ya Ole Medeye itazamwe
JANA
chombo kimoja cha habari kilimkariri Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye, akisema kuwa kampuni moja
imewahi kumpa dola za Marekani 800,000 (sawa na takriban shilingi
bilioni moja) za hongo ikitaka atoe upendeleo katika kugawa eneo.
Kilichotufanya
hadi kufikia hatua ya kuandika tahariri hii ni kitendo cha naibu waziri
huyo kutoi taja kampuni iliyotaka kumpa hongo hiyo, eneo ambalo
lilihusika na hatua ambazo aliichukulia.
Kauli
hiyo imetushangaza kwa sababu, Ole Medeye kama kiongozi, anafahamu
kwamba kitendo kilichofanywa na kampuni hiyo ni kosa na yeye kukaa bila
kuchukua hatua pia ni kosa.
Sisi
Tanzania Daima tunajiuliza, kama Ole Medeye ambaye ni mfano wa kuigwa
amelichukulia jambo hilo kimzaha, je, anatoa somo gani kwa watu wengine?
Sote
tunafahamu ya kwamba kuna migogoro mingi ya ardhi katika nchi yetu
ambayo inahitaji mapinduzi ya kweli katika kuishughulikia.
Wakati
tukiwa katika wimbi la migogoro hiyo, inashangaza kusikia bado kuna
watu ambao wanataka kupitia njia za mkato ili kunyang’anya haki za watu
wengine kwa kupewa upendeleo.
Cha
ajabu, naibu waziri anayeongoza wizara nyeti ya serikali analiacha
jambo hilo lipite hivi hivi bila kuchukua hatua stahiki, ili uwe mfano
kwa watu wengine wenye tabia na mwenendo wa kampuni iliyotaka kumpa
hongo ya shilingi bilioni moja.
Sisi
Tanzania Daima kama chombo huru cha habari, tunaamini njia sahihi ya
kuanza kupunguza migogoro ya ardhi inayoikabili nchi yetu sasa hivi ni
kuanza kupambana na rushwa.
Tunasema hayo kwa sababu rushwa imekuwa ni kikwazo kikubwa kinachochangia migogoro mingi ya ardhi.
Kuna
baadhi ya watu leo hii wamepokonywa haki yao ya kumiliki ardhi kwa
sababu tu kuna mtu mwenye pesa aliwarubuni viongozi nao wakabariki
dhambi hiyo.
Kutokana
na hilo, kwanza, tunamtaka naibu waziri kuiweka hadharani kampuni
anayodai kwamba ilitaka kumpa hongo ya sh bilioni moja.
Pili,
tunahitaji kusikia hatua ambazo ataichukulia, na asipofanya hivyo
tutakosa imani naye kama naibu waziri wa Ardhi ambaye kwa nafasi yake
anaweza kushughulikia migogoro ya ardhi kwa mamlaka makubwa, hasa katika
eneo la rushwa ambalo limekuwa kikwazo kikubwa.
Tatu,
tunaamini Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesikia
kauli ya naibu waziri huyo wa Ardhi na tunaamini itachukua hatua
zinazostahili ili kuisaidia wizara katika kushughulikia migogoro ya
ardhi inayoanzia kwenye rushwa.
Tunaamini
Naibu Waziri Ole Medeye kama kweli kwa kushirikiana na Waziri wake,
Anna Tibaijuka, wanataka kuleta mageuzi katika wizara hiyo ambayo baadhi
wanaiita ya migogoro ya ardhi, atoe ushirikiano wake kwa kuitaja
kampuni hiyo na nyingine kama zipo ambazo hajazisema, zilizoonesha kutoa
hongo kwa nia ya kunyang’anya haki za wengine ili ziweze kuchukuliwa
hatua.
Ole
Medeye asipofanya hivyo, tutakosa imani na yeye kama kiongozi aliyepewa
wadhifa na mamlaka ya kushughulikia mambo ya ardhi na maendeleo ya
makazi kutekeleza wajibu wake kwa malengo yaliyokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment