WAZIRI Mkuu Mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Majaliwa Kassim
Majaliwa, amesema hakutarajia kama angeteuliwa kushika wadhifa huo,
lakini aliahidi kuwa msikivu, muadilifu na mtendaji mzuri.
Pia amewaahidi wabunge ushirikiano bila kujali itikadi zao na kwamba
atafanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini kuona changamoto
zinazowakabili wananchi, kusikiliza maoni yao na kuyafanyia kazi.
Akizungumza bungeni muda mfupi baada ya Bunge kumthibitisha kwa kura
za ndiyo 258 sawa na asilimia 73.5, alisema hakuwa na maandalizi yote na
hakufahamu kama angeteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa.
“Nimshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kuniamini kwa namna yoyote
ile kulileta jina langu kwa nafasi hii. Nami niliangalia uteuzi huu
kupitia televisheni wakati Spika akifungua zile bahasha tatu,
niwashukuru wabunge wote kwa kunipigia kura nyingi za ndiyo.
“Nitawapa ushirikiano wabunge wote bila kujali vyama, nyote ni
wawakilishi wa wananchi, nitasikiliza ushauri wenu ili tufanye kazi kwa
maslahi ya Taifa letu,” alisema Naibu Waziri huyo wa zamani na kuongeza
kuwa milango yake itakuwa wazi kupokea ushauri kwa namba mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge, mteule
huyo anayetarajiwa kuapishwa na Rais Magufuli, Ikulu ya Chamwino leo saa
nne asubuhi, alisema ana kazi kubwa mbele yake ya kufanya.
“Nilitoka mazoezini asubuhi (jana), nikawa naangalia televisheni ni
Mbunge gani ameteuliwa, hili ni jambo kubwa kwangu, lakini nimelipokea,”
alisema mbunge huyo wa Ruangwa mkoani Lindi.
0 comments:
Post a Comment