Friday, November 20, 2015



WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Rais John Magufuli ni Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa (55). Majaliwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akishughulikia Elimu katika Serikali ya Awamu ya Nne, hakuwa miongoni mwa waliokuwa wakitajwa sana na vyombo vya habari na hata wabunge kwamba wangeteuliwa katika nafasi hiyo kubwa.
Lakini baada ya jina hilo kuwasilishwa bungeni, wabunge walithibitisha uteuzi wake kwa kura za Ndiyo 258 sawa asilimia 73.5, ushindi ulioelezwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba ni wa kimbunga. Akisoma matokeo hayo, Katibu wa Bunge, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Dk Thomas Kashililah, alisema kura zilizomkataa zilikuwa 91, sawa na asilimia 25.9. Kwa mujibu wa Dk Kashililah, kura zilizopigwa zilikuwa 351 na kura mbili ziliharibika, ambapo wabunge waliosajiliwa kwa ajili ya Bunge hilo ni 369.
Idadi ya wabunge kikatiba ni 394. Wa pili kutoka Kusini Majaliwa aliyezaliwa Desemba 22, 1960, amekuwa Mbunge wa Ruangwa akitanguliwa na Sigfried Ng’itu (sasa marehemu) na Philip Magani, kuongoza wilaya hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007.
Mbali ya kuwa Naibu Waziri, amewahi kuwa mwalimu wa shule za msingi na sekondari, mkufunzi wa vyuo vya ualimu, Katibu wa Chama cha Walimu ngazi ya Wilaya na Mkoa, mwanamichezo na Mkuu wa Wilaya za Rufiji mkoani Pwani na Urambo mkoani Tabora. Uteuzi wake na hatimaye kuthibitishwa na Bunge, kunampa fursa ya leo kuapishwa na Dk Magufuli kushika wadhifa huo akiwa ni Mtanzania wa 11 kukalia kiti hicho na wa pili kutoka mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Ataapishwa leo saa nne asubuhi katika Ikulu ya Chamwino mjini hapa na atakuwa amefuata nyayo za Rashidi Kawawa kushika wadhifa huo akitokea kusini mwa Tanzania, katika Mkoa wa Lindi, na zaidi Wilaya ya Ruangwa ambayo ni jirani na Liwale alikotokea ‘Simba wa Vita.’ Si hilo tu.
Majaliwa pia anaendeleza rekodi ya siku za karibuni ya Waziri Mkuu kutokea Ofisi ya Waziri Mkuu na hasa Tamisemi, kwani mtangulizi wake na aliyekuwa bosi wake mkuu, Mizengo Pinda aliteuliwa Februari 2008 akiwa Waziri wa Tamisemi, na kabla ya hapo alikuwa Naibu Waziri Tamisemi.
Mbali ya Kawawa na Pinda, mawaziri wakuu wengine waliopita ni Mwalimu Julius Nyerere, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.
Uwasilishaji jina la Waziri Mkuu Kivutio kikubwa jana ilikuwa namna ya kuletwa ukumbini kwa bahasha kutoka kwa Dk Magufuli yenye jina la Waziri Mkuu ambapo ilikuwa tofauti na ilivyokuwa katika awamu zilizopita. Baada ya wabunge kuwasili ukumbini saa tatu asubuhi na kumaliza kusoma dua, Spika Ndugai aliwaeleza kuwa alikuwa hajapata jina la Waziri Mkuu Mteule na kisha akasena anamtuma Katibu wa Bunge, Dk Kashililah kufuatilia bahasha yenye jina hilo.
Aliwataka wabunge kuwa watulivu wakati wakati jina hilo likisubiri na kuahidi kwamba lingewasili ukumbini muda si mrefu. Kadhalika aliahidi kwamba angeifungua bahasha hiyo hapo hapo na kusoma jina la mteule huyo. Hata hivyo, baada ya kupita karibu dakika 20 bila kuwepo dalili ya bahasha hiyo kuletwa ukumbini, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alitaka jambo hilo liahirishwe hadi hapo serikali itakapojipanga kwani ilionekana kama ni kudhalilisha Bunge.
Kauli hiyo ilipingwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliyesema Msigwa ndiye anataka kudhalilisha Bunge kwani utaratibu unaotakiwa kufanywa ndiyo kazi ya Bunge. Mpambe wa Rais aingia na bahasha Wakati wabunge wakiendelea na kusubiri huku wakibadilishana mawazo, aliingia ukumbini Katibu wa Bunge na kwenda moja kwa moja kuzungumza na Spika Ndugai ambaye aliwaeleza wabunge kwamba tayari mambo yalikuwa yameiva na bahasha ingeletwa na mpambe (ADC) wa Rais. Alisema kwa vile mpambe huyo ni askari haikuwa tatizo kuingia ukumbini.
Aliingia kwa mwendo wa kikakamavu akiambatana na maaskari wa Bunge na kwenda kumkabidhi Spika kisha kupiga saluti na kuondoka eneo hilo la ukumbi. Ndugai alimuita Katibu wa Bunge aliyefungua bahasha hiyo kubwa iliyokuwa imefungwa ambapo pia kulikuwa na bahasha nyingine mbili, kabla ya mwisho ndogo kuwa na barua ya Rais kwa Spika yenye jina la mteule wake.
Ilipofika saa tatu na dakika 35 asubuhi, Spika Ndugai aliwaeleza wabunge kwamba barua hiyo ilielekezwa kwake na kwamba ilihusu uteuzi wa Waziri Mkuu. Kisha akasoma ujumbe wa barua hiyo ambao alisema umeandikwa kwa mkono wake Rais, yaani hakuchapishwa.
“Mimi John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania nimemteua (alisita kusoma, kisha wabunge wakaangua kicheko), Mheshimiwa Mbunge wa Ruangwa, Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema Ndugai na kuibua shangwe kwa wabunge.
Baadaye wabunge walipumzika ili kutoa fursa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa wasifu wa mteule huyo, lakini pia kumwezesha Katibu wa Bunge, kuandaa utaratibu wa kura kwa wabunge, kwani ingekuwa ngumu kuandaa wakati hawakuwa wakifahamu nani atateuliwa.
Mwanasheria Mkuu asoma wasifu wake Baada ya Bunge kurejea tena saa tano asubuhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju alisoma wasifu wake ili kutoa hoja ya kuomba Bunge limthibitishe Majaliwa kuwa Waziri Mkuu. "Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina masharti yanayoelekeza kwamba Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zidi bungeni.
"Au, kama hakuna chama chenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Mbunge atakayeteuliwa kushika wadhifa huo, hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa Azimio litakaloungwa mkono na kura za wabunge walio wengi," alisema Mwanasheria Mkuu huyo.
Alisema kwa vile tayari Rais amemteua Majaliwa, ambaye ni Mbunge wa Ruangwa na pia anatoka CCM yenye wabunge wengi sharti hilo linakidhi matakwa ya katiba. “Naamini kwa dhati kwamba waheshimiwa Wabunge mtakubaliana na mimi kwamba Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa ni mtu muadilifu, asiyekuwa na makuu, mwenye hekima na busara nyingi.
“Msikivu wa hali ya juu na mchapakazi hodari atakayemudu majukumu yake ipasavyo katika zama hizi za uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu halali ya kila mwananchi maarufu Hapa Kazi Tu,” alisema.
Alisema mteule huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu, ni mtu mwenye uwezo wa kuchambua kwa kina na kupima hoja mbalimbali. Pia alisema uwezo wake mpana wa mambo katika kufikia maamuzi umejidhihirisha katika utumishi wake wa umma wa muda mrefu kama mwalimu wa shule za msingi na sekondari, mkufunzi wa vyuo vya ualimu, Katibu wa Chama cha Walimu ngazi ya Wilaya na Mkoa, mwanamichezo na Mkuu wa Wilaya za Rufiji na Urambo. Sehemu nyingine alikoonesha umahiri wake wa kazi ni katika Ubunge, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akishughulikia elimu katika Serikali ya Awamu ya Nne.
“Kwa sababu hiyo, Majaliwa Kassim Majaliwa ana uzoefu wa utendaji wa kazi wa kutosha na kwa utumishi wake katika Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Masaju na kuongeza kuwa pia Waziri Mkuu mteule alikuwa kocha wa timu ya Bunge SC. Alisema sifa hizo ni kuthibitisha anao uwezo wa kuyabeba na kuyahimili majukumu yote yanayoendana na wadhifa wa kazi na Mamlaka ya Waziri Mkuu.
“Baada ya maelezo haya sasa, kwa unyenyekevu, heshima na taadhima kubwa, naliomba Bunge lako tukufu lithibitishe uteuzi wa Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Ruangwa, uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ili awe Waziri mkuu kwa kupitisha Azimio la Bunge,” alisema Masaju.

0 comments:

Post a Comment