RAIS
mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa
wafungwa 4,160 katika kuaga na kukabidhi madaraka ya Serikali kwa Rais
wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Dk Magufuli
aliapishwa jana kuwa Rais wa Tano wa Tanzania katika sherehe zilizofana
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Kikwete akimaliza miaka yake
10 ya kuongoza nchi kama ilivyoelekezwa na Katiba.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam, kati ya
wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na wafungwa 3,293
watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya
vifungo vyao vilivyobaki.
“Ni mategemeo ya Serikali
kwamba wafungwa watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana
na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na watajiepusha na utendaji
makosa ili wasirejee tena gerezani,” alisema Chikawe katika taarifa
hiyo.
Chikawe aliwataja walionufaika na msamaha huo
kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya
punguzo la kawaida linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya
Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1
(i-xix).
Aliwataja wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa
wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wako kwenye
hatua ya mwisho ambao watathibitishwa na waganga chini ya Mganga mkuu wa
mkoa au wilaya.
Pia wazee wenye umri zaidi ya miaka
70, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na
watoto wanaonyonya na wasionyonya na walemavu wa mwili na akili na
ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga.
Kwa mujibu
wa Chikawe, msamaha hautawahusu wafungwa wenye adhabu za kunyongwa,
waliohukumiwa kunyongwa na adhabu hiyo baadaye kubadilishwa kuwa kifungo
cha maishaau kifungo gerezani.
Wengine ni wafungwa
waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za
kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na utoaji rushwa,
unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka, kulawiti au
kujaribu kutenda makosa hayo.
Aidha, makosa mengine
ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo ni makosa ya kuwapa mimba
wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo,
matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa vifungo na Rais.
“Wengine
ni waliopatikana na hatia kwa kuwazuia watoto kupata masomo, utekaji
watoto, usafirishaji binadamu, ukatili dhidi ya albino, usafirishaji
nyara za Serikali na ujangili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mengine
ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za
Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na
wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole Sheria
Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 ya Mwaka
2002.

0 comments:
Post a Comment